Kusitishwa ghafla kwa mashambulizi kati ya Marekani na Iran; vyombo vya habari vinasemaje?

Chanzo cha picha, X/CENTCOM/
Siku mbili baada ya kusitishwa kwa ghafla kwa mashambulizi ya kulipizana kati ya Marekani na Iran, ripoti zimeibuka zikidai kuwa kusitishwa huko kulikuwa uamuzi wa moja kwa moja wa Rais Donald Trump.
Ingawa maafisa wa Ikulu ya White House bado hawajatoa maelezo rasmi kuhusu sababu za kusimamishwa kwa mashambulizi hayo, vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa vimeripoti kwamba Donald Trump ameamua kutoongeza makali ya mzozo na Iran "kwa sasa" baada ya kufanya mkutano na washauri wake wakuu siku ya Ijumaa.
Gazeti la The New York Times, likinukuu maafisa wawili waliofahamu yaliyofanyika katika mkutano huo, liliripoti kwamba kupungua kwa akiba ya makombora ya kuzuia mashambulizi ya anga ya Patriot pamoja na silaha nyingine za ulinzi wa anga za Marekani katika Mashariki ya Kati kulikuwa miongoni mwa sababu kuu zilizopelekea uamuzi huo.
Afisa mmoja mwandamizi wa Marekani aliliambia The New York Times kwamba, "Wanajeshi watatu wa Marekani waliuawa Ijumaa iliyopita nchini Jordan baada ya kombora la masafa marefu la Iran kupenya mifumo ya ulinzi wa anga ya Marekani iliyokuwa ikijibu wimbi la makombora na ndege zisizo na rubani ."
Kwa mujibu wa The New York Times, sababu nyingine zilizozingatiwa na utawala wa Trump ni pamoja na uwezekano wa vita kuenea katika eneo la Mashariki ya Kati, kuongezeka kwa tofauti kati ya Washington na washirika wake wa Kiarabu wa Ghuba, athari mbaya kwa uchumi wa dunia, kuzorota kwa mzozo wa nishati, na kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi.
Kwa mujibu wa The New York Times, katika mkutano wa washauri wakuu wa Ikulu ya White House ambao unadaiwa kusababisha mabadiliko ya msimamo wa Rais Trump, Makamu wa Rais J.D. Vance na Jenerali Dan Kaine, Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Marekani , walieleza wasiwasi kuhusu kuongeza ukubwa wa vita dhidi ya Iran.
CNN iliripoti taarifa kama hiyo, ikisema kwamba Jenerali Kaine alisema katika mkutano wa Ijumaa kwamba jeshi lilikuwa na uwezo wa kutekeleza chaguo zilizopo, lakini alionya kuhusu madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na hatua hizo.
Operesheni imekwisha?
Katika maoni pekee yaliyotolewa hadi sasa kutoka kwa serikali ya Marekani, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu ya White House, Steven Chong, alisema katika taarifa:
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Rais Donald Trump amesisitiza mara kwa mara kwamba anapendelea suluhisho la kidiplomasia, lakini ikiwa Iran itaendelea na shughuli zake za kigaidi katika Mlango bahari wa Hormuz au dhidi ya washirika, machaguo yote bado yako mezani."
Mabadiliko ya mkakati wa kijeshi wa Marekani yamekuja wakati ambapo wasiwasi kuhusu kuenea kwa vita ulikuwa tayari umeongezeka kwa kiwango kikubwa.
CNN iliripoti kwamba Donald Trump, huku akisema alikuwa akifikiria kufanya shambulio kubwa dhidi ya Iran katika siku za karibu, aliwaagiza wajumbe wa Marekani wanaohusika na mazungumzo "kuendelea kuzungumza."
Chombo hicho kiliongeza kuwa chanzo chenye ufahamu wa suala hilo kikisema kwamba hatua hiyo inaonesha kuwa rais wa Marekani amekabiliana na ukweli kwamba machaguo yake ya kijeshi ni machache bila kutuma wanajeshi katika ardhi ya Iran.
Vyanzo kadhaa viliiambia CNN kwamba watu wachache katika watu wa karibu wa Trump au ndani ya Pentagon waliamini kwamba chaguo zilizokuwepo za kuongeza mzozo zingezalisha matokeo aliyokuwa akiyatarajia.
Kuhusiana na maendeleo hayo, msemaji wa jeshi la Iran, Mohammad Akraminia, alipoulizwa kwenye televisheni ya taifa ya Iran kama hali ya sasa ilimaanisha "kusitisha mapigano kwa upande mmoja kutoka Marekani," alisema:
"Marekani inapitia kudhoofika kwa uwezo wake wa kufanya maamuzi ya kimkakati. Haina mkakati ulio wazi. Hili linaonekana katika maamuzi ya rais na utendaji wa CENTCOM."
Hata hivyo, akizungumzia mwitikio wa Iran kwa matukio ya hivi karibuni, msemaji huyo wa jeshi alisema kwamba kwa kuwa mkakati wa Iran katika kipindi hiki cha vita umekuwa wa "kulipiza kisasi," baada ya Marekani kusitisha mashambulizi yake katika siku mbili zilizopita, "sisi pia tulisitisha operesheni zetu."
Alisema kwamba kwa kuwa malengo ya Marekani hayajafikiwa katika hatua hii ya vita, inaonekana Wamarekani wanatafuta mkakati mpya ambao huenda ukawa wa "kujiondoa kwenye vita."
Hata hivyo, msemaji huyo wa jeshi la Iran alisisitiza kwamba matokeo ya ziara ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, nchini Marekani siku ya Jumatatu pia ni muhimu.
Alisema Marekani inaweza kufanya "operesheni kubwa ya anga" kutokana na shinikizo kutoka Israel. Hakukataa uwezekano wa shambulio la ardhini, lakini alisisitiza kwamba Iran ina mipango kwa kila aina ya hali.
Ziara ya Netanyahu, hata hivyo, imefanyika wakati ambapo tovuti ya Axios iliandika katika ripoti yake kwamba kusitishwa kwa operesheni za kijeshi dhidi ya Iran kulikuwa jambo lisilotarajiwa kwa baraza la usalama la Israel na jeshi la Israel.
Kwa mujibu wa Axios, Israel ilikuwa imejiandaa kwa "shambulio kubwa la Marekani" ambalo lingeweza kusababisha Israel kujibu kwa mashambulizi yake, lakini ghafla waliarifiwa kwamba Donald Trump hakuwa ameidhinisha mashambulizi zaidi.
Kuhusiana na hilo, Shirika la Habari la Anadolu, shirika rasmi la habari la Uturuki, lilinukuu vyanzo katika serikali ya Pakistan vikisema kwamba Pakistan na Qatar zimeongeza mawasiliano baada ya kupokea majibu kutoka Iran na Marekani kuhusu mpango wa kumaliza vita.
Kwa mujibu wa ripoti hizo, Pakistan na Qatar zimezitaka Iran na Marekani kurudi kwenye makubaliano yaliyokuwepo kabla ya kuvunjika kwake na kuanza tena mazungumzo yaliyokwama.















