Je, vita vya Iran vimemaliza akiba ya Marekani ya makombora ya kuzuia mashambulizi ya anga?

Chanzo cha picha, Getty Images
Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, ameamua kuahirisha mpango wa kupanua mashambulizi dhidi ya Iran, huku mjadala ukizidi kushika kasi mjini Washington kuhusu kiwango cha akiba ya makombora ya kuzuia mashambulizi ya anga na risasi za mifumo ya ulinzi wa anga ya Marekani.
Magazeti ya The New York Times na The Wall Street Journal, yakinukuu maafisa wa Marekani, yaliripoti kuwa suala la akiba ya silaha pamoja na juhudi za kuendeleza diplomasia ni miongoni mwa mambo yaliyotiliwa maanani kabla ya uamuzi huo kufikiwa.
Hata hivyo, The New York Times iliripoti kuwa mojawapo ya wasiwasi mkubwa wa maafisa wa Marekani ni kupungua kwa akiba ya makombora ya kuzuia mashambulizi ya anga yanayotumika kulinda kambi za kijeshi za Marekani na maslahi yake pamoja na washirika wake katika Mashariki ya Kati dhidi ya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Iran.
Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la The Wall Street Journal, Trump alikanusha madai kuwa Marekani inapungua akiba ya silaha, akisema: "Tuna akiba kubwa zaidi ya risasi kuliko nchi nyingine yoyote duniani, kubwa zaidi hata kuliko tunavyohitaji."
Wasiwasi huo hauhusiani na vita vya sasa pekee. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, jeshi la Marekani limetumia akiba hiyo katika operesheni mbalimbali kwa wakati mmoja, ikiwemo kukabiliana na mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu, kuisaidia Israel kujihami dhidi ya makombora ya Iran, kuipatia Ukraine msaada wa kijeshi, na kulinda makumi ya maelfu ya wanajeshi wa Marekani walioko Mashariki ya Kati.
Matokeo yake ni kwamba baadhi ya makombora ya kisasa na yenye gharama kubwa zaidi ya kuzuia mashambulizi ya anga yametumika kwa kasi ambayo, kwa mujibu wa baadhi ya wataalamu na taasisi za utafiti, hata viwanda vikubwa vya ulinzi nchini Marekani haviwezi kuyazalisha upya kwa haraka.
Pentagon haitoi taarifa kuhusu kiwango cha akiba ya silaha zake kwa sababu za kiusalama. Hata hivyo, maafisa wa Marekani wameendelea kukanusha ripoti zinazodai kuwa akiba ya makombora na risasi imepungua kwa kiwango kinachotia wasiwasi. Aidha, Waziri wa Ulinzi wa Marekani aliwahi kuelezea madai hayo kuwa ni "propaganda zinazotolewa na vyombo vya habari."
Kwa mujibu wa The Wall Street Journal, Kamanda wa Kikosi cha Marekani katika Mashariki ya Kati (CENTCOM), Admiral Brad Cooper, anaamini kuwa licha ya kupungua kwa akiba ya makombora ya kuzuia mashambulizi ya anga, Marekani bado ina uwezo wa kuendeleza operesheni zake za kijeshi. Anaeleza kuwa kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya Iran kunaweza kudhoofisha uwezo wa Tehran kurusha makombora, jambo ambalo litapunguza hitaji la kutumia makombora mengi zaidi ya kujihami.
Kadiri mjadala kuhusu akiba ya makombora ya Marekani unavyozidi kushika kasi, ndivyo maswali yanavyoibuka kuhusu kiwango ambacho vita vya hivi karibuni, hususan mzozo na Iran, vimeathiri uwezo wa nchi hiyo kujilinda dhidi ya mashambulizi ya makombora, na iwapo sekta yake ya ulinzi inaweza kuzalisha kwa haraka silaha zinazotumika vitani.
Majibu ya maswali hayo yanaweza kuwa muhimu si tu kwa mustakabali wa mzozo kati ya Marekani na Iran, bali pia kwa utayari wa Washington kukabiliana na migogoro mingine inayoweza kuzuka katika maeneo mbalimbali duniani.

Chanzo cha picha, BRENDAN SMIALOWSKI/AFP via Getty Images
Vita vya Iran vilikuwa na athari gani kwa akiba ya Marekani ya makombora ya kuzuia mashambulizi ya anga?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Shinikizo kwenye akiba ya makombora ya Marekani ya kuzuia mashambulizi ya anga halikuanza na vita vya hivi karibuni dhidi ya Iran pekee. Hata hivyo, hali hiyo ilifikia kiwango ambacho, kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, kilikuwa miongoni mwa sababu zilizoathiri uamuzi wa Ikulu ya Marekani kuhusu iwapo iendeleze au ipanue operesheni zake za kijeshi.
Kwa hakika, kabla ya kuanza kwa mgogoro wa moja kwa moja na Iran, mifumo ya ulinzi wa anga ya Marekani ilikuwa tayari ikikabiliana na mashambulizi ya Wahouthi katika Bahari ya Shamu kwa miezi kadhaa; baadhi ya akiba ya makombora ya aina ya Patriot ilikuwa imetolewa kwa Ukraine, na meli za Marekani pia zilikuwa zimetumia makombora ya kuzuia mashambulizi ya aina ya SM-3 na SM-6 wakati wa mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel mwaka 2024.
Baada ya kuzuka kwa vita vipya, Iran, mbali na kuishambulia Israel, ilifyatua mamia ya makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani kuelekea kambi za Marekani na nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi. Mashambulizi hayo yalizuiwa kwa kiasi kikubwa na mifumo ya Patriot, THAAD na mfumo wa Aegis uliowekwa kwenye meli za kivita za Marekani.
Hata hivyo, kuzuia makombora ya balistiki ni gharama kubwa. Kelly Grieco, mtafiti katika Taasisi ya Stimson, aliambia BBC kuwa, kulingana na taratibu za kawaida, makombora mawili ya kuzuia mashambulizi hufyatuliwa dhidi ya kila kombora la balistiki linalokuja ili kuongeza uwezekano wa kuliharibu; iwapo hayo mawili yatashindwa, kombora la tatu linaweza kufyatuliwa.
Kwa sababu hiyo, hata kama kiwango cha mafanikio ni kikubwa, matumizi ya makombora hayo ya kuzuia mashambulizi huongezeka kwa kasi zaidi kuliko idadi ya makombora yanayokuja.
Bi. Grieco anasisitiza kuwa idadi halisi ya makombora hayo yaliyopo ni siri na kwamba makadirio yote yanatokana na taarifa zilizopo, ikiwa ni pamoja na mikataba ya mauzo ya silaha na nyaraka za bajeti. Hivyo, hakuna takwimu yoyote iliyochapishwa inayoweza kuchukuliwa kuwa ya uhakika kabisa.
Hata hivyo, makadirio ya taasisi mbalimbali huru yanaonyesha mwelekeo unaofanana. Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa (CSIS) kinakadiria kuwa katika siku 39 za kwanza za Operesheni Epic Fury, Marekani ilitumia zaidi ya nusu ya akiba yake ya kabla ya vita ya makombora muhimu ya kuzuia mashambulizi, yakiwemo Patriot na THAAD. Kwa mujibu wa tathmini hiyo, mfumo wa THAAD ndio uliobeba mzigo mkubwa zaidi wa operesheni hizo.
Kwa hakika, hata kabla ya vita vya hivi karibuni, matumizi ya makombora hayo yalikuwa yamefikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika historia ya hivi karibuni ya jeshi la Marekani.
Siku mbili baada ya kumalizika kwa vita vya siku 12 mnamo mwaka wa 2025, Jenerali Dan Keene, Mwenyekiti wa Jopo la Wakuu wa Majeshi ya Marekani, alitangaza kuwa operesheni ya kulinda Kituo cha Jeshi la Anga cha Udeid nchini Qatar dhidi ya shambulio la makombora ya Iran ilikuwa "operesheni kubwa zaidi ya hatua moja ya mfumo wa Patriot ya kudungua makombora katika historia ya jeshi la Marekani" kufikia wakati huo.
Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na taasisi ya uchambuzi ya JINSA ("Jewish Foundation for National Security Affairs of America"), takriban makombora 30 ya mfumo wa Patriot yalifyatuliwa ili kudungua makombora 14 ya balistiki ya Iran yaliyolenga kituo cha Udeid, hatua iliyogharimu kiasi kinachokadiriwa kuwa dola milioni 111.
Kulingana na makadirio ya Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa (Center for Strategic and International Studies), Marekani ilikuwa na takriban makombora 360 ya kuzuia mashambulizi ya aina ya THAAD, 2,330 ya aina ya Patriot, 410 ya aina ya SM-3, na 1,160 ya aina ya SM-6 kabla ya kuanza kwa vita vya hivi karibuni dhidi ya Iran.
Makadirio haya yanatokana na hesabu zilizofanywa na waandishi wa ripoti hiyo kwa kutumia data za bajeti na ununuzi kutoka Wizara ya Ulinzi ya Marekani.
Taasisi hiyo pia inakadiria kuwa katika kipindi cha siku 39 cha mashambulizi ya anga na makombora kabla ya kusitishwa kwa mapigano, Marekani ilitumia kati ya makombora 190 na 290 ya THAAD, 1,060 na 1,430 ya Patriot, 130 na 250 ya SM-3, na 190 na 370 ya SM-6.
Ikiwa makadirio haya ni sahihi, makombora ya THAAD ndiyo yaliyoathirika zaidi, huku takriban nusu hadi sehemu nne kati ya tano ya akiba yake ya kabla ya vita ikitumika. Yanafuatiwa na makombora ya Patriot, ambayo inakadiriwa kuwa akiba yake imepungua kwa asilimia 45 hadi 60.
Kwa upande wa makombora ya SM-3, kiwango kilichotumika kinakadiriwa kuwa kati ya theluthi moja na theluthi mbili ya akiba ya awali, na kwa makombora ya SM-6, makadirio ni kati ya sehemu moja kati ya sita na karibu theluthi moja.
Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa kinasisitiza kuwa takwimu hizi zinatokana na taarifa zinazopatikana hadharani, nyaraka za bajeti, mikataba ya ununuzi, na makadirio ya wataalamu na si takwimu rasmi za serikali ya Marekani lakini zinatoa picha ya shinikizo ambalo vita dhidi ya Iran vimeweka kwenye akiba ya mifumo ya ulinzi dhidi ya makombora ya Marekani.
Kwa nini si rahisi kubadilisha makombora haya?
Kabla ya vita vya hivi karibuni dhidi ya Iran, jeshi la Marekani lilikuwa limehitimisha kuwa uwezo wake wa kuzalisha makombora ya kuzuia mashambulizi (interceptor missiles) haukuendana na mahitaji ya baadaye.
Mnamo tarehe 16 Aprili 2025, Bodi ya Kusimamia Mahitaji ya Jeshi iliongeza mara nne idadi inayohitajika ya makombora ya kisasa ya Patriot ya kuzuia mashambulizi (PAC-3 MSEs), kutoka takriban 3,300 hadi zaidi ya 13,700.
Uamuzi huu ulifanywa wakati ambapo vita nchini Ukraine, ongezeko la oda kutoka kwa washirika wa Marekani, na hofu kuhusu uwezekano wa migogoro kutokea kwa wakati mmoja barani Ulaya, Mashariki ya Kati, na Asia ya Mashariki vilikuwa vimeongeza shinikizo kwenye akiba ya mifumo ya ulinzi dhidi ya makombora ya Marekani.
Kufuatia kuanzishwa kwa Operesheni Epic Fury dhidi ya Iran mnamo tarehe 28 Februari, matumizi makubwa ya makombora hayo ya kuzuia mashambulizi yaliongeza hofu hizo na kuharakisha mipango ya kuongeza uzalishaji.
Mnamo Januari 2026, Wizara ya Ulinzi ya Marekani na kampuni ya Lockheed Martin zilitia saini makubaliano ya miaka saba ya kupanua uwezo wa uzalishaji, na mnamo Aprili mwaka huo, mkataba mkuu wa kwanza wenye thamani ya dola bilioni 4.7 ulitolewa chini ya mpango huo.
Mkataba huo unalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa kila mwaka wa makombora ya kisasa ya Patriot ya kuzuia mashambulizi kutoka takriban 600 kwa mwaka hadi takriban 2,000 kufikia mwisho wa mwaka 2030.

Chanzo cha picha, Reuters
Suala si vita vya Iran pekee
Kupungua kwa akiba ya vizuizi vya Marekani haimaanishi kwamba nchi hiyo imepoteza uwezo wa kuendelea na shughuli dhidi ya Iran. Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa kilisema katika ripoti mwishoni mwa Aprili kwamba Marekani bado ina risasi za kutosha katika matukio yanayowezekana kwa vita vinavyoendelea na Iran.
Hata hivyo, wasiwasi mkubwa wa Washington, kwa mujibu wa CSIS, unahusu kile kinachoweza kutokea baada ya mzozo wa sasa. Taasisi hiyo inaeleza kuwa iwapo mgogoro mwingine mkubwa utazuka kabla akiba iliyopungua haijarejeshwa, Marekani inaweza kujikuta ikikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa silaha muhimu.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa utengenezaji upya wa baadhi ya makombora ya kisasa ya kuzuia mashambulizi unahitaji muda mrefu. Aidha, kurejesha akiba katika kiwango kinachotosha kwa mzozo mkubwa unaoweza kuhusisha taifa lenye uwezo mkubwa wa kijeshi kama China kutahitaji muda zaidi.
Wasiwasi huo pia ulijitokeza wakati Ikulu ya White House ilipokuwa ikitafakari uwezekano wa kuanzisha tena mashambulizi makubwa dhidi ya Iran. Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, Mwenyekiti wa Jopo la Wakuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Dan Keene, aliwaonya maafisa wa utawala kuwa ingawa jeshi lina uwezo wa kuanzisha operesheni nyingine kubwa, hatua hiyo ingeweza kupunguza kwa kiwango kikubwa akiba ya makombora ya kuzuia mashambulizi yaliyopo chini ya Amri Kuu ya Jeshi la Marekani.
Gazeti hilo pia liliripoti kuwa maafisa wa Marekani walihofia kuwa mashambulizi mapana zaidi dhidi ya Iran yangeweza kusababisha jibu kali kutoka Tehran, jambo ambalo lingeongeza shinikizo kwa mifumo ya ulinzi wa anga inayolinda kambi za Marekani nchini Jordan, Kuwait, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu.















