Moja kwa moja, Marekani yaishambulia tena Iran, Trump aahidi mashambulizi makali zaidi
Mashambulizi hayo yamefanyika saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuahidi kuishambulia Iran kwa "nguvu kubwa", kufuatia shambulio ambalo Tehran inadaiwa kulenga wanajeshi wa Marekani walioko Mashariki ya Kati.
Jeshi la Iran (IRGC) limetangaza kuwa Mlango bahari wa Hormuz hauwezi kufunguliwa tena iwapo vitisho na kauli za vita bado zinatolewa na viongozi wa Marekani, pamoja na kuingilia harakati za meli katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Iran, IRNA, jeshi hilo limesema,“Vitisho na uingiliaji vimeifanya hali kuwa ngumu na tata zaidi.”
Taarifa hiyo pia ilisema, bila kuitaja nchi yoyote kwa jina, kwamba nchi zinazohusika kuisaidia Marekani katika mashambulizi yake yatakabiliwa vikali.
Hapo jana CENTCOM ilitangaza kwamba IRGC hawana mamlaka ya kuamua njia ambayo meli zinapaswa kutumia katika Mlango bahari wa Hormuz.
Watu 3 wauawa, 2 wajeruhiwa katika shambulio la Marekani katika kisiwa cha Qeshm, Iran
Chanzo cha picha, IRIB
Shirika la habari la Iran, Fars News Agency, limeripoti kuwa watu watatu wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa katika mashambulizi ya Marekani yaliyofanyika asubuhi ya leo katika Kisiwa cha Qeshm.
Kulingana na maafisa wa afya, mama, baba na mtoto wao mwenye umri wa miaka miwili waliuawa katika shambulio lililolenga nyumba yao katika eneo la Chahtangu, mjini Qeshm.
Kulingana na BBC Persian, watoto wengine wawili waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walijeruhiwa na wamepelekwa hospitalini kupokea matibabu.
Kenya power yatangaza kurejea kwa umeme baada ya huduma hiyo kukatika maeneo mengi nchini Kenya
Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika
la kusambaza umeme nchini Kenya, Kenya Power, imetangaza kuwa umeme umerejea kikamilifu
kwa wateja wake wote walioathiriwa na kukatika kwa huduma za
umeme katika maeneo mbalimbali nchini
Kenya usiku wa jana.
Katika
taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo mapema leo asubuhi, kampuni hiyo ilisema
umeme umerejeshwa kikamilifu.
“Tunafurahi kuwafahamisha kwamba usambazaji wa
umeme ulirejeshwa kikamilifu kwa wateja wote walioathirika”
Kupotea
kwa kwa umeme kulishuhudia jijini Nairobi,maeneo ya pwani ya Kenya, Kati mwa
Kenya na Bonde la Ufa.
Kampuni hiyo katika taarifa
yake ilidokeza kuwa kulikuwa na hitilafu za kimitambo, lakini imethibitisha kuwa huduma ya umeme
sasa imerejea katika maeneo yote yaliyoathirika.
Watu 8 wafariki ikiwemo watoto baada ya Urusi kuishambulia Ukraine
Chanzo cha picha, Reuters
Watu nane, wakiwemo watoto wawili, wamefariki katika mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyorushwa na Urusi nchini Ukraine.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amesema kwamba Urusi inajiandaa kwa “shambulizi kubwa”, na kuwataka wananchi kuzingatia tahadhari na ving’ora vya mashambulizi ya anga.
Mapema leo asubuhi, jeshi la Ukraine limeripoti mashambulizi kadhaa ya makombora na ndege zisizo na rubani katika maeneo mbalimbali nchini humo.
Mashambulizi hayo yamefanyika baada ya Zelensky kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump mjini Washington DC wiki hii, ambapo aliiomba Marekani kuipa Ukraine leseni ya kutengeneza mfumo wa makombora ya kuzuia mashambulizi ijulikanayo kama Patriot.
Wasichana wawili wenye umri wa miaka 5 na 12 ni miongoni mwa watu sita waliofariki katika kijiji kilicho karibu na mji wa Kryvyi Rih, katikati mwa Ukraine, baada ya kombora la balistiki kulenga nyumba yao.
Watu wengine wanane wamejeruhiwa, wakiwemo watoto wawili, huku maafisa wakionya kuwa idadi ya waliojeruhiwa na waliopoteza maisha inaweza kuongezeka.
Mjini Kyiv, mtu mmoja alifariki na moto kuzuka katika majengo matatu yasiyo ya makazi usiku kucha, Meya wa mji huo Vitali Klitschko alichapisha kwenye Telegram.
Jeshi la Marekani lasema limelenga kambi za kijeshi za Iran katika wimbi jipya la mashambulizi
Chanzo cha picha, CENTCOM
Kituo kikuu cha kundesha oparesheni za kijeshi nchini Marekani CENTCOM, kimetangaza kumaliza mashambulizi yake dhidi ya Iran yaliyofanyika mapema leo asubuhi, ambayo yalikuwa yakijibu mashambulizi ya makombora ya Iran dhidi ya wanajeshi wa Marekani nchini Jordan.
Mashambulizi hayo yalimalizika karibu mwendo wa saa kumi na moja asubuhi kwa saa za Iran.
Kulingana na taarifa ya CENTCOM, mashambulizi hayo yalilenga maeneo walioko wanajeshi wa Iran (IRGC), yakiwemo vituo vya uongozi wa kijeshi, maeneo ya kuhifadhi makombora na ndege zisizo na rubani, vituo vya ufuatiliaji na ulinzi wa pwani, pamoja na uwezo wa kijeshi wa majini nchini Iran.
CENTCOM imesema lengo la mashambulizi hayo lilikuwa kupunguza zaidi vitisho kutoka Iran na washirika wake dhidi ya wanajeshi wa Marekani na meli za kibiashara za mataifa jirani.
Hata hivyo, mamlaka za eneo la Qeshm zimesema leo asubuhi nyumba moja yenye angalau wakazi watatu katika kisiwa hicho ililengwa katika mashambulizi hayo. Mamlaka hizo pia zilitoa picha zinazoonyesha waokoaji wakijaribu kuwafikia watu waliokuwa wamenaswa chini ya vifusi.
Idadi ya waliofariki kwa tetemeko la ardhi yafikia 30 nchini Japan
Chanzo cha picha, Afp by Getty
Idadi ya watu waliofariki baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililotokea kusini magharibi mwa Japan imeongezeka hadi 30, kulingana na mamlaka za taifa hilo.
Waokoaji bado wanaendelea na shughuli za kutafuta manusura baada ya tetemeko lenye ukubwa wa 6.8 katika kipimo cha Richter kushuhudiwa katika mkoa wa Kumamoto, katika kisiwa cha Kyushu, siku ya Jumanne na kusababisha uharibifu mkubwa wa nyumba na miundombinu.
Maelfu ya wakazi waliolazimika kuondoka kwenye makazi yao sasa wanaishi katika vituo vya muda vya kuwahifadhi waathirika.
Kulingana na utabiri wa hali ya hewa, joto katika mkoa huo unaweza kufikia nyuzi joto 39 katika siku zijazo, huku maafisa wamewataka manusura na waokoaji kuchukua tahadhari dhidi ya kiharusi cha joto.
Zaidi ya mitetemeko 100 ya kufuatia tetemeko kuu imerekodiwa tangu tetemeko la kwanza lilipotokea. Baadhi ya wakazi wameamua kulala kwenye magari yao kwa hofu ya kutokea kwa mitetemeko mingine.
WAFCON 2026: Kenya na Tanzania kusaka heshima Morocco
Chanzo cha picha, CECAFA
Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) inaendelea leo huku macho yakielekezwa kwa timu za Afrika Mashariki, ambapo Kenya itashuka dimbani leo Alhamisi dhidi ya Senegal, wakati Tanzania itacheza kesho Ijumaa dhidi ya Burkina Faso.
Kenya itavaana na Senegal kwenye Uwanja wa Olympic mjini Rabat, ikisaka ushindi wake wa kwanza katika Kundi A baada ya kupoteza mechi ya ufunguzi 4-0 dhidi ya wenyeji Morocco.
Kwa upande wa Tanzania, Twiga Stars itacheza na Burkina Faso kuanzia katika Uwanja wa Larbi Zaouli mjini Casablanca, ikiwa na lengo la kuendeleza mwanzo mzuri baada ya kushinda mchezo wake wa kwanza 2-1 dhidi ya Afrika Kusini.
Mbali na mchezo wa Kenya, leo pia kutakuwa na pambano kali la Kundi A kati ya wenyeji Morocco na Algeria, litakaloanza mjini Rabat.
Katika michezo iliyochezwa Jumatano, Ghana ilianza kampeni yake kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde katika Kundi D.
Nayo Cameroon iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mali katika mchezo mwingine wa Kundi D.
Matokeo ya mechi za ufunguzi kwa Kenya na Tanzania
Ushindi wa Tanzania dhidi ya Afrika Kusini umeiweka Twiga Stars katika nafasi nzuri ya kusaka tiketi ya hatua ya robo fainali, huku Kenya ikihitaji matokeo mazuri dhidi ya Senegal ili kujiweka katika mazingira ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Liverpool yaandaa ofa ya kwanza kumsajili Barcola kutoka PSG
Chanzo cha picha, Getty Images
Liverpool imeongeza juhudi zake za kumsajili winga wa Paris Saint-Germain (PSG), Bradley Barcola, na inajiandaa kuwasilisha ofa yake ya kwanza kwa klabu hiyo ya Ufaransa.
Barcola, mwenye umri wa miaka 23, ametajwa kuwa chaguo kuu la Liverpool katika harakati za kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mohamed Salah, aliyeondoka mwishoni mwa msimu uliopita.
PSG inasema thamani ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa ni pauni milioni 145.
Iwapo usajili huo utakamilika kwa kiasi hicho, utavunja rekodi ya uhamisho ghali zaidi kuwahi kufanyika nchini Uingereza. Hata hivyo, viongozi wa Liverpool wana matumaini ya kufikia makubaliano kwa ada inayokaribia pauni milioni 100.
Barcola amebakiza miaka miwili katika mkataba wake na PSG, lakini inaelezwa kuwa yuko tayari kuhamia Liverpool akitafuta changamoto mpya, baada ya nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa Ufaransa kupungua.
Awali, Liverpool ilikuwa ikimwania winga wa RB Leipzig Yan Diomande, lakini sasa mchezaji huyo anatarajiwa kujiunga na Real Madrid.
Barcola alikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichofika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia la 2026.
Marekani yashambulia tena Iran, Trump aahidi mashambulizi makali zaidi
Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la Marekani limesema limefanya mashambulizi mapya dhidi ya Iran usiku wa Alhamisi, likisema ni hatua ya kujibu shambulio lililolenga wanajeshi wake walioko Mashariki ya Kati mapema wiki hii.
Haya ni mashambulizi ya kwanza ya Marekani dhidi ya Iran katika takriban wiki moja.
Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti milipuko karibu na Kisiwa cha Qeshm na mji wa Abadan, kusini mwa nchi hiyo.
Shirika la habari la serikali ya Iran, IRNA, limemnukuu afisa wa jimbo la Hormozgan akisema kuwa vikosi vya uokoaji vinaendelea kuwatafuta watu wawili wanaodaiwa kufunikwa na vifusi baada ya kuangukiwa na nyumba katika Kisiwa cha Qeshm.
Mashambulizi hayo yamefanyika saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuahidi kuijibu Iran kwa "nguvu kubwa", kufuatia shambulio ambalo Tehran inadaiwa kulenga wanajeshi wa Marekani walioko Mashariki ya Kati.
Siku ya Jumatano, jeshi la Marekani na lile la Jordan yalisema yalizuia makombora yaliyokuwa yamerushwa kuelekea Jordan, yakidai yalitoka Iran na yalilenga maeneo yenye wanajeshi wa Marekani.
Katika taarifa yake, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema mashambulizi hayo ni "jibu kali" kwa kile ilichokiita mashambulizi ya Iran dhidi ya wanajeshi wa Marekani yaliyodhibitiwa siku iliyotangulia.
Wakati huo huo, tovuti ya habari ya Marekani Axios, ikimnukuu afisa wa Marekani ambaye haikumtaja kwa jina, ilisema Washington ilikuwa imeanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Iran.
Awali akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya White House, Trump alisema Marekani itaishambulia Iran "kwa nguvu kubwa".
"Sasa ni zamu yetu," alisema Trump, huku akiongeza kuwa bado kuna uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano siku zijazo, lakini akasisitiza kuwa, "tutaishambulia kwa nguvu sana."