Mlango Hormuz: Hatari ya mabomu ya baharini ni ipi na kwa nini kuyaondoa ni vigumu?

Asilimia 20 ya usambazaji wa mafuta na LNG duniani hupitia Mlango wa Hormuz.

Chanzo cha picha, Ian Forsyth/Getty Images

Maelezo ya picha, Asilimia 20 ya usambazaji wa mafuta na LNG duniani hupitia Mlango wa Hormuz.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Suala la mabomu ya baharini yanayodaiwa kuwekwa wakati wa vita kati ya Iran na Marekani limeibuka tena katika mjadala wa kimataifa.

Alhamisi, Rais wa Marekani Donald Trump alisema ameliagiza Jeshi la Wanamaji la Marekani kuharibu mara moja boti zozote za Iran zitakazobainika kuweka mabomu katika Mlango wa Hormuz.

Takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi ya kimiminika duniani hupita kupitia mlango huo wa Hormuz, huku Iran ikitajwa kuudhibiti kwa kiasi kikubwa.

Wakati huo huo, Marekani imekuwa ikisisitiza kuwa inaweza kuufungua mlango huo kwa kutumia nguvu za kijeshi na kuondoa mabomu hayo ya baharini yanayodaiwa kuwekwa.

Hapa tunaeleza mabomu ya baharini ni nini, yanavyofanya kazi, hatari yake, na kwa nini ni vigumu sana kuyaondoa.

Mabomu ya baharini ni nini?

Picha ya mazoezi ya jeshi la wanamaji la IRGC mnamo Februari 16, 2026. Zoezi hilo lilifanyika katika Ghuba ya Uajemi na Mlango wa bahari wa Hormuz.

Chanzo cha picha, Press Office of Islamic Revolutionary Guard Corps / Handout/Anadolu via Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ya mazoezi ya jeshi la wanamaji la IRGC mnamo Februari 16, 2026. Zoezi hilo lilifanyika katika Ghuba ya Uajemi na Mlango wa bahari wa Hormuz.

Mabomu ya baharini ni vifaa vya kulipuka vinavyowekwa chini ya maji kwa lengo la kuharibu manowari na meli.

Hutumika kuzuia meli za adui kuingia katika eneo fulani la bahari au kuzikwamisha.

Teknolojia hii ni ya zamani, ikiwa ilianza kutumiwa na China katika karne ya 14 dhidi ya maharamia.

Matumizi yake ya kwanza Marekani yalikuwa wakati wa Mapinduzi ya Marekani, ambapo mapipa yaliyojazwa baruti yalielea baharini na kulipuka yalipogongana na meli.

Tangu wakati huo, mabomu ya baharini yametumika katika karibu kila vita vya majini duniani, ikiwemo Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia, Vita vya Korea, Falklands na Vita vya Ghuba.

Mtaalamu wa ulinzi Rahul Bedi anasema mabomu ya baharini yana uwezo wa kujilipua yenyewe bila kudhibitiwa moja kwa moja.

Anasema: "Haya ni mabomu yanayolenga shabaha. Yanaitwa 'mabomu ya akili' kwa sababu yanaweza kutofautisha kati ya meli za mafuta, za kivita au za kibiashara na kulipuka kwa kulenga aina fulani ya meli."

Aina za mabomu ya baharini

Wanajeshi wa Ujerumani wakiwa na migodi ya bahari katika Bahari ya Kaskazini mnamo 1842, wakati wa Vita vya Kidunia vya pili

Chanzo cha picha, Roger Viollet via Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Ujerumani wakiwa na migodi ya bahari katika Bahari ya Kaskazini mnamo 1842, wakati wa Vita vya Kidunia vya pili

Kwa mujibu wa Kituo cha Robert Strauss cha Usalama na Sheria, kuna aina tatu kuu za mabomu ya baharini:

Mabomu ya mguso hulipuka meli inapoyagusa moja kwa moja au kukaribia sana.

Mabomu ya kisasa zaidi huitwa mabomu ya vihisishi ambayo hayahitaji mguso wa moja kwa moja, bali hutumia vihisi kama sumaku, sauti, shinikizo au mawimbi ya chini ya maji kugundua meli.

Aina ya tatu ni mabomu yanayodhibitiwa kwa mbali, ambayo hulipuliwa na mtu anayeyaongoza.

Jinsi yanavyowekwa baharini

Kuna mbinu kadhaa za kuyaweka baharini:

  • Mabomu yanayoelea hufuata mkondo wa maji.
  • Mabomu yaliyofungwa nanga hubaki karibu na uso wa maji na hulipuka meli inapoyagusa.
  • Mabomu ya chini ya bahari huwekwa sakafuni mwa bahari na hulipuka kwa kutumia vihisi.
  • Pia kuna mabomu madogo yanayoitwa limpet ambayo huwekwa moja kwa moja kwenye mwili wa meli na kuzimwa kwa muda uliopangwa kabla ya kulipuka.

Ukweli kuhusu mabomu ya ardhini ya Iran huko Hormuz

Kwa mujibu wa Marekani, Iran imeweka kati ya mabomu 5,000 hadi 6,000 katika Mlango wa Hormuz.

Ripoti nyingine zinasema mabomu kadhaa yamewekwa katika kipindi cha vita kwa kutumia boti za mwendo kasi.

Hata hivyo, wataalamu wanasema hakuna uhakika kamili kuhusu hali halisi.

Rahul Bedi anasema: "Kwa sasa hakuna anayejua hali halisi ya Mlango wa Hormuz. Kuna mkanganyiko mkubwa. Hata hatujui maeneo halisi ya meli za Marekani au Iran."

Anasema hata kama mabomu hayo yamewekwa kwa wingi kama inavyodaiwa, tayari mlango huo umegeuzwa kuwa eneo la kimkakati lenye hatari kubwa.

Kwa nini kuyaondoa ni vigumu?

Mabomu ya baharini ni rahisi kuweka lakini ni vigumu sana kuyaondoa.

Yanaweza kuwa juu ya maji, chini ya maji au sakafuni mwa bahari, na mengine yanaweza kubadilisha nafasi kutokana na mikondo ya maji.

Iran yenyewe haijui mabomu yake yako wapi, kwani huenda yaliwekwa kwa haraka.

Au eneo la kila mabomu huenda halijarekodiwa au mabomu mingine yaliachwa kwa makusudi kupeperuka.

Rahul Bedi anasema, "Kuondoa mabomu ya ardhini ni kazi ngumu sana na inachukua muda mwingi. Iran pia inajua hili. Hakuna anayejua kwa uhakika ni mambomu mangapi yametegeshwa huko Hormuz, lakini Iran kwa sasa imedumisha faida ya kisaikolojia kwa kuzungumza juu ya utegaji wa mabomu ya baharini hapa."

Hata baada ya kusafishwa, eneo linaweza kubaki hatarini tena.

Wataalamu wanasema kuna njia mbili kuu za kuyaondoa: kusafisha kwa kuvuta vifaa maalum na kutafuta kwa kutumia sonar na roboti.

Mustakabali wa India kuhusu mabomu

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa mujibu wa Rahul Bedi, India haijawahi kutumia mabomu ya baharini katika vita.

Anasema India ilikuwa na meli maalum za kuondoa mabomu za tangu wakati wa enzi za kisovieti lakini sasa hazipo za kutosha, na juhudi za kupata mpya zimechelewa.

"Katika kipindi cha miaka mitatu au minne iliyopita, India imejaribu kupata kandarasi hiyo. Mazungumzo yalikuwa yakiendelea na Korea Kusini na Italia, lakini hakuna kilichokamilishwa."

"Wafagiaji wa mabomu ni meli maalumu. Vifaa vyake vimeundwa kutambua mabomu. Wana zana maalum za kuziondoa."

Anasema meli hizo ni za kipekee zenye vifaa maalum vya kugundua na kuondoa mabomu ya baharini.

Kwa ujumla, mabomu ya baharini yanabaki kuwa silaha hatari lakini pia ngumu sana kudhibiti au kuondoa, na hivyo kufanya maeneo kama Mlango wa Hormuz kuwa na umuhimu mkubwa wa kimkakati duniani.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid