Mfahamu mshukiwa wa ufyatuaji risasi kwenye hafla ya Chakula cha Waandishi wa White House iliyohudhuriwa na Trump

Chanzo cha picha, @REALDONALD TRUMP / TRUTHSOCIAL
Mtu aliyekamatwa na polisi baada ya ufyatuaji risasi usiku wa kuamkia Jumamosi kwenye hoteli iliyokuwa ikiandaliwa Chakula cha Waandishi wa White House sasa ametambuliwa, kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana na mtandao wa Marekani CBS, mshirika wa BBC, baada ya kushauriana na vyanzo vya polisi.
Mshukiwa ni Cole Tomas Allen, 31, mkazi wa Torrance, kitongoji cha kusini magharibi mwa Los Angeles, California.
Baada ya kuzuiliwa na maafisa wa usalama ndani ya hoteli ya Washington Hilton, ambako tukio hilo lilikuwa likifanyika, aliambia mamlaka kwamba alitaka kuwapiga risasi maafisa wa utawala wa Trump, vyanzo viwili viliiambia CBS.
Ikinukuu vyanzo hivi, CBS pia ilionyesha kuwa kati ya risasi tano na nane zilifyatuliwa.
Video ya kamera ya usalama iliyotolewa na Trump inaonyesha mtu akiwatoroka maafisa wa usalama, kisha wakageuka na kumfukuza.
Katika kikao na wanahabari siku ya Jumamosi, polisi waliripoti kwamba maafisa wa usalama na mshukiwa walifyatuliana risasi, bila kutaja ni risasi ngapi zilifyatuliwa kutoka kila upande.
Mkuu wa polisi wa muda wa Washington, Jeffery Carroll, alisema kuwa mshukiwa hakujeruhiwa na risasi hizo, lakini alipelekwa hospitali kwa ajili ya kutathminiwa.
Mshukiwa huyo alikuwa mgeni katika hoteli ya Washington Hilton, ambapo chakula cha jioni cha wanahabari hao kilikuwa kikiandaliwa, Carroll alisema, akiongeza kuwa "alikuwa na bunduki, bastola na visu kadhaa."
"Kwa sasa, kila kitu kinaonekana kuashiria kuwa ni mtu aliyekuwa pekee," mkuu wa polisi alisema.
Baadaye, Trump alichapisha picha ya karibu ikimuonyesha mwanamume mtanashati akiwa chini, mikono yake ikiwa imefungwa mgongoni, akiwa amezungukwa na maajenti wa Secret Service.
Baadaye, picha ziliibuka zikionyesha maajenti wa FBI na polisi wakipekua eneo katika anwani ya California inayoaminika kuhusishwa na mshukiwa huyo.

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hadi kufikia 2020, Allen alifanya kazi kwa muda katika kampuni ya kufundisha huko Torrance inayoitwa C2 Education, na mnamo Desemba 2024 alitawazwa kuwa"mwalimu bora wa mwezi".
Haijulikani ikiwa bado anafanya kazi katika kampuni hiyo. Wilaya ya Shule ya Torrance Unified iliiambia CBS kwamba Allen hajawahi kuajiriwa na wilaya yao.
Rekodi za wapiga kura wa Kaunti ya Los Angeles zinaonekana kuashiria kuwa hakuwa na upendeleo wa chama kilichosajiliwa.
Kulingana na rekodi ya Tume ya Shirikisho ya Uchaguzi, ambayo BBC Thibitisha iliweza kufikia, mnamo Oktoba 2024 Allen alichangia $25 (£18) kwa jukwaa la uchangishaji la ActBlue, pesa ambazo zilikusudiwa kwa kampeni ya urais ya Kamala Harris.
Allen anajielezea kwenye LinkedIn kama mhandisi wa mitambo, msanidi wa mchezo wa video, na mwalimu.
Kulingana na wasifu wake, alisomea uhandisi wa mitambo katika Taasisi ya Teknolojia ya California (Caltech), kabla ya kuhitimu shahada ya uzamili ya sayansi ya kompyuta kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la California mnamo 2025.
Caltech aliithibitishia CBS kupitia barua pepe kwamba Allen alihitimu kutoka Caltech mnamo 2017, lakini hakutoa maelezo zaidi.
Jeanine Pirro, mwendesha mashtaka wa serikali ya jimbo la Washington, alisema kuwa mshukiwa anakabiliwa na mashtaka mawili: matumizi ya bunduki wakati wa uhalifu wa kutumia nguvu na kushambulia wakala wa serikali kwa silaha hatari.
Aliongeza kuwa atashtakiwa rasmi Jumatatu katika mahakama ya shirikisho.
Mwanasheria Mkuu wa Marekani Todd Blanche aliiambia CNN kwamba "itabaki kuonekana" ikiwa mashtaka zaidi yatafunguliwa dhidi ya mshukiwa, akiongeza kuwa "hakika" anaweza kushtakiwa kwa jaribio la mauaji kulingana na ushahidi.











