Kutoka Ukraine hadi Zanzibar: Mgahawa uliozaliwa kutokana na vita

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Miaka minne iliyopita, Alla Nikolaieva alifika Zanzibar kwaajili ya likizo. Hakujua kwamba safari hiyo ingegeuka kuwa mwanzo wa maisha mapya, maelfu ya kilomita kutoka nyumbani kwake nchini Ukraine.

Alla, ambaye kabla ya vita alikuwa mhadhiri na baadaye Mkuu wa Kitivo (Dean) katika Chuo Kikuu cha Udaktari cha Kharkiv nchini Ukraine, alijikuta akishindwa kurejea nyumbani baada ya Urusi kuvamia Ukraine tarehe 24 Februari mwaka 2022.

Mji wake wa Kharkiv, ulioko karibu na mpaka wa Urusi, ulikuwa miongoni mwa miji ya kwanza kushambuliwa.

"Nilikuja Zanzibar kwa ajili ya likizo, lakini nilipaswa kurudi nyumbani tarehe 2 Machi. Vita vilipoanza, sikuweza tena kurudi," anaiambia BBC.

Maisha yalibadilika ghafla

Alla alikuwa amekuja Zanzibar kuwatembelea mabinti zake mapacha, ambao wanaishi nchini Tanzania na ambao waliwasili nchini humo kupitia programu ya kubadilishana wanafunzi wa udaktari miaka kumi iliyopita.

Anasema alipitia kipindi kigumu sana pale vita vilipoanza.

"Ilikuwa ni wakati ambapo nilikuwa na msongo mkubwa wa mawazo. Marafiki zangu, familia yangu na wanafunzi wangu wengi wameathirika tangu wakati huo," anasema.

Mbali na kuacha kazi yake, Alla pia aliacha nyuma marafiki, jamaa na maisha aliyoyazoea kwa miaka mingi.

Anasema baadhi ya wanafunzi wake wa zamani walipoteza maisha kutokana na vita.

"Mmoja wa wanafunzi wangu alikuwa amehitimu tu kabla ya kufariki mwaka 2022. Wanafunzi wetu wengi walifariki katika vita hivi."

Mwanzo wa maisha mapya Zanzibar

Binti yake, Nuru, anasema familia iliona kuwa njia pekee ya kumsaidia mama yao ni kuanza upya.

"Mama alikuwa analia kila siku, akiangalia taarifa za habari na kuwasiliana na ndugu zake Ukraine. Tuliamua kuwa ni bora tuanze maisha hapa na kujenga kitu kipya," anasema.

Mwezi Juni mwaka 2022, familia hiyo ilifungua mgahawa wa vyakula vya Kiukraine unaoitwa Milky Way katika eneo la Jambiani, Zanzibar.

Jina hilo, Alla anasema, lina maana ya kipekee.

"Nyota tunazoziona Zanzibar ni zilezile tunazoziona Ukraine. Nyota hizo zinaunganisha nchi zetu kila usiku."

Ladha ya Ukraine katika fukwe za Zanzibar

Katika mgahawa huo, wageni hupata fursa ya kuonja vyakula vya asili vya Ukraine, ikiwemo borscht, supu maarufu ya beetroot, pamoja na varenyky, dumplings yani aina ya ndazi lililopikwa na mvuke kwa mbinu za upishi za Ukraine.

Anasema mwanzoni watu wengi hawakuelewa vyakula hivyo.

"Walikuwa wanauliza, 'Hii ni supu gani?' Lakini baada ya kuonja, walisema ni tamu sana."

Mbali na watalii kutoka mataifa mbalimbali, mgahawa huo pia umekuwa sehemu ya kukutana kwa tamaduni za Ukraine na Tanzania.

"Tunataka kuunganisha tamaduni za Ukraine na Tanzania. Watu wa nchi hizi mbili wanafanana kwa ukarimu na upendo," anasema.

Kujifunza maisha ya "pole pole"

Alla anasema maisha ya Zanzibar yamemfundisha kuishi kwa utulivu.

"Ukraine kila kitu ni haraka, haraka. Lakini hapa ni pole pole, hakuna matata. Watu ni wakarimu sana."

Anasema mwanzoni ilikuwa changamoto kuishi katika nchi mpya, hasa kwasababu hakuwa anazungumza Kiingereza wala Kiswahili.

Lakini kwa msaada wa mabinti zake, wafanyakazi na majirani, taratibu alizoea maisha mapya.

Leo hii, mgahawa wake unaajiri Watanzania na umegeuka kuwa daraja la kitamaduni kati ya Ukraine na Zanzibar.

"Tunaiombea Ukraine amani"

Licha ya kuijenga Zanzibar kama makaazi mapya, Alla anasema bado anaikumbuka sana Ukraine.

"Tunawakumbuka marafiki zetu, mji wetu na nchi yetu. Hatujui kesho itakuwaje, lakini tunamuomba Mungu tuione kesho."

Hajui kama siku moja atarudi kuishi Ukraine.

"Tunapenda Kharkiv yetu, lakini tusubiri vita viishe, halafu tutaona."

Kwa sasa, kupitia chakula, ukarimu na kumbukumbu za nyumbani, Alla anaendelea kuiweka Ukraine hai katika kona moja ya Zanzibar, huku akisubiri siku ambayo nchi yake itapata amani tena.