Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani yaishambulia tena Iran, Trump aahidi mashambulizi makali zaidi

Mashambulizi hayo yamefanyika saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuahidi kuishambulia Iran kwa "nguvu kubwa", kufuatia shambulio ambalo Tehran inadaiwa kulenga wanajeshi wa Marekani walioko Mashariki ya Kati.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu & Ambia Hirsi

  1. Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, azirai mahakamani

    Kizza Besigye, kiongozi wa upinzani nchini Uganda, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika mji mkuu Kampala baada ya kuanguka na kupoteza fahamu wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake ya uhaini.

    Besigye, mwenye umri wa miaka 70, amekuwa kizuizini tangu mwezi Novemba 2024.

    Wakili wake mkuu alikamatwa mwezi uliopita na kushtakiwa kwa madai ya kushindwa kuripoti vitendo vya uhaini na anazuiliwa na polisi hadi sasa.

    Besigye ambaye hali yake ya afya inaonekana kuwa dhaifu, alikuwa akipinga uamuzi wa mawakili wa serikali kuteuliwa kumwakilisha mahakamani, kabla ya kuanguka na kupoteza fahamu. Walinzi wa gereza walimkimbiza hospitalini.

    “Bado amepoteza fahamu. Hawezi kuzungumza, na haitikii hata akidungwa sindano ili kupima mwitikio wa maumivu,” mkewe, Winnie Byanyima, ambaye anaongoza shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana ugonjwa wa UKIMWI (UNAIDS), amechapisha kwenye mtandao wa X.

    Siku ya Jumatano katika Mahakama Kuu ya Kampala, mashahidi waliokuwa mahakamani walisema Besigye alipaza sauti mara kadhaa akisema “wacheni” kuhusu suala la uwakilishi wake wa kisheria kabla ya kuanguka.

    Besigye alipelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Mulago, hospitali kubwa zaidi ya umma nchini Uganda, lakini alikataa kutibiwa na wahudumu wa afya wa serikali.

    Mkewe Byanyima alisema kupitia X kuwa “Hatutaruhusu afisa yeyote wa serikali kumgusa.”

    Mkewe anataka Besigye aruhusiwe kupata matibabu kutoka kwa daktari wake binafsi katika kliniki ya kibinafsi, badala ya kutibiwa katika kituo cha afya cha serikali.

    Kitengo cha ICU ambako Besigye anatibiwa, kimezingirwa na maafisa wa usalama . Ripoti zinaeleza kuwa dada yake, ambaye pia ni daktari wake binafsi, ameweza kuruhusiwa kumwona.

    Wakili mkuu wa Besigye, Erias Lukwago, yuko gerezani baada ya kukamatwa na jeshi mwezi uliopita.

    Wakili wake mwingine Martha Karua kutoka nchini Kenya, alizuiwa kuingia nchini Uganda baada ya kusafiri kwenda huko mwezi uliopita kumwakilisha Besigye.

    Mwanawe Besigye, Adam Ampa, amemwomba Rais Yoweri Museveni na mwanawe, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mkuu wa jeshi la Uganda, kuwa na huruma na kumuachilia baba yake kwa misingi ya kibinadamu.

    Besigye, ambaye amewania urais dhidi ya Rais Yoweri Museveni mara nne, alitekwa nyara nchini Kenya mwaka wa 2024.

    Soma pia:

  2. Hatutafungua Mlango bahari wa Hormuz - Iran

    Jeshi la Iran (IRGC) limetangaza kuwa Mlango bahari wa Hormuz hauwezi kufunguliwa tena iwapo vitisho na kauli za vita bado zinatolewa na viongozi wa Marekani, pamoja na kuingilia harakati za meli katika eneo hilo.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Iran, IRNA, jeshi hilo limesema,“Vitisho na uingiliaji vimeifanya hali kuwa ngumu na tata zaidi.”

    Taarifa hiyo pia ilisema, bila kuitaja nchi yoyote kwa jina, kwamba nchi zinazohusika kuisaidia Marekani katika mashambulizi yake yatakabiliwa vikali.

    Hapo jana CENTCOM ilitangaza kwamba IRGC hawana mamlaka ya kuamua njia ambayo meli zinapaswa kutumia katika Mlango bahari wa Hormuz.

    Soma pia:

  3. Watu 3 wauawa, 2 wajeruhiwa katika shambulio la Marekani katika kisiwa cha Qeshm, Iran

    Shirika la habari la Iran, Fars News Agency, limeripoti kuwa watu watatu wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa katika mashambulizi ya Marekani yaliyofanyika asubuhi ya leo katika Kisiwa cha Qeshm.

    Kulingana na maafisa wa afya, mama, baba na mtoto wao mwenye umri wa miaka miwili waliuawa katika shambulio lililolenga nyumba yao katika eneo la Chahtangu, mjini Qeshm.

    Kulingana na BBC Persian, watoto wengine wawili waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walijeruhiwa na wamepelekwa hospitalini kupokea matibabu.

    Soma pia:

  4. Kenya power yatangaza kurejea kwa umeme baada ya huduma hiyo kukatika maeneo mengi nchini Kenya

    Shirika la kusambaza umeme nchini Kenya, Kenya Power, imetangaza kuwa umeme umerejea kikamilifu kwa wateja wake wote walioathiriwa na kukatika kwa huduma za umeme katika maeneo mbalimbali nchini Kenya usiku wa jana.

    Katika taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo mapema leo asubuhi, kampuni hiyo ilisema umeme umerejeshwa kikamilifu.

    “Tunafurahi kuwafahamisha kwamba usambazaji wa umeme ulirejeshwa kikamilifu kwa wateja wote walioathirika”

    Kupotea kwa kwa umeme kulishuhudia jijini Nairobi,maeneo ya pwani ya Kenya, Kati mwa Kenya na Bonde la Ufa.

    Kampuni hiyo katika taarifa yake ilidokeza kuwa kulikuwa na hitilafu za kimitambo, lakini imethibitisha kuwa huduma ya umeme sasa imerejea katika maeneo yote yaliyoathirika.

  5. Watu 8 wafariki ikiwemo watoto baada ya Urusi kuishambulia Ukraine

    Watu nane, wakiwemo watoto wawili, wamefariki katika mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyorushwa na Urusi nchini Ukraine.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amesema kwamba Urusi inajiandaa kwa “shambulizi kubwa”, na kuwataka wananchi kuzingatia tahadhari na ving’ora vya mashambulizi ya anga.

    Mapema leo asubuhi, jeshi la Ukraine limeripoti mashambulizi kadhaa ya makombora na ndege zisizo na rubani katika maeneo mbalimbali nchini humo.

    Mashambulizi hayo yamefanyika baada ya Zelensky kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump mjini Washington DC wiki hii, ambapo aliiomba Marekani kuipa Ukraine leseni ya kutengeneza mfumo wa makombora ya kuzuia mashambulizi ijulikanayo kama Patriot.

    Wasichana wawili wenye umri wa miaka 5 na 12 ni miongoni mwa watu sita waliofariki katika kijiji kilicho karibu na mji wa Kryvyi Rih, katikati mwa Ukraine, baada ya kombora la balistiki kulenga nyumba yao.

    Watu wengine wanane wamejeruhiwa, wakiwemo watoto wawili, huku maafisa wakionya kuwa idadi ya waliojeruhiwa na waliopoteza maisha inaweza kuongezeka.

    Mjini Kyiv, mtu mmoja alifariki na moto kuzuka katika majengo matatu yasiyo ya makazi usiku kucha, Meya wa mji huo Vitali Klitschko alichapisha kwenye Telegram.

    Soma pia:

  6. Jeshi la Marekani lasema limelenga kambi za kijeshi za Iran katika wimbi jipya la mashambulizi

    Kituo kikuu cha kundesha oparesheni za kijeshi nchini Marekani CENTCOM, kimetangaza kumaliza mashambulizi yake dhidi ya Iran yaliyofanyika mapema leo asubuhi, ambayo yalikuwa yakijibu mashambulizi ya makombora ya Iran dhidi ya wanajeshi wa Marekani nchini Jordan.

    Mashambulizi hayo yalimalizika karibu mwendo wa saa kumi na moja asubuhi kwa saa za Iran.

    Kulingana na taarifa ya CENTCOM, mashambulizi hayo yalilenga maeneo walioko wanajeshi wa Iran (IRGC), yakiwemo vituo vya uongozi wa kijeshi, maeneo ya kuhifadhi makombora na ndege zisizo na rubani, vituo vya ufuatiliaji na ulinzi wa pwani, pamoja na uwezo wa kijeshi wa majini nchini Iran.

    CENTCOM imesema lengo la mashambulizi hayo lilikuwa kupunguza zaidi vitisho kutoka Iran na washirika wake dhidi ya wanajeshi wa Marekani na meli za kibiashara za mataifa jirani.

    Hata hivyo, mamlaka za eneo la Qeshm zimesema leo asubuhi nyumba moja yenye angalau wakazi watatu katika kisiwa hicho ililengwa katika mashambulizi hayo. Mamlaka hizo pia zilitoa picha zinazoonyesha waokoaji wakijaribu kuwafikia watu waliokuwa wamenaswa chini ya vifusi.

    Soma pia:

  7. Idadi ya waliofariki kwa tetemeko la ardhi yafikia 30 nchini Japan

    Idadi ya watu waliofariki baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililotokea kusini magharibi mwa Japan imeongezeka hadi 30, kulingana na mamlaka za taifa hilo.

    Waokoaji bado wanaendelea na shughuli za kutafuta manusura baada ya tetemeko lenye ukubwa wa 6.8 katika kipimo cha Richter kushuhudiwa katika mkoa wa Kumamoto, katika kisiwa cha Kyushu, siku ya Jumanne na kusababisha uharibifu mkubwa wa nyumba na miundombinu.

    Maelfu ya wakazi waliolazimika kuondoka kwenye makazi yao sasa wanaishi katika vituo vya muda vya kuwahifadhi waathirika.

    Kulingana na utabiri wa hali ya hewa, joto katika mkoa huo unaweza kufikia nyuzi joto 39 katika siku zijazo, huku maafisa wamewataka manusura na waokoaji kuchukua tahadhari dhidi ya kiharusi cha joto.

    Zaidi ya mitetemeko 100 ya kufuatia tetemeko kuu imerekodiwa tangu tetemeko la kwanza lilipotokea. Baadhi ya wakazi wameamua kulala kwenye magari yao kwa hofu ya kutokea kwa mitetemeko mingine.

    Soma pia:

  8. WAFCON 2026: Kenya na Tanzania kusaka heshima Morocco

    Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) inaendelea leo huku macho yakielekezwa kwa timu za Afrika Mashariki, ambapo Kenya itashuka dimbani leo Alhamisi dhidi ya Senegal, wakati Tanzania itacheza kesho Ijumaa dhidi ya Burkina Faso.

    Kenya itavaana na Senegal kwenye Uwanja wa Olympic mjini Rabat, ikisaka ushindi wake wa kwanza katika Kundi A baada ya kupoteza mechi ya ufunguzi 4-0 dhidi ya wenyeji Morocco.

    Kwa upande wa Tanzania, Twiga Stars itacheza na Burkina Faso kuanzia katika Uwanja wa Larbi Zaouli mjini Casablanca, ikiwa na lengo la kuendeleza mwanzo mzuri baada ya kushinda mchezo wake wa kwanza 2-1 dhidi ya Afrika Kusini.

    Mbali na mchezo wa Kenya, leo pia kutakuwa na pambano kali la Kundi A kati ya wenyeji Morocco na Algeria, litakaloanza mjini Rabat.

    Katika michezo iliyochezwa Jumatano, Ghana ilianza kampeni yake kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde katika Kundi D.

    Nayo Cameroon iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mali katika mchezo mwingine wa Kundi D.

    Matokeo ya mechi za ufunguzi kwa Kenya na Tanzania

    Ushindi wa Tanzania dhidi ya Afrika Kusini umeiweka Twiga Stars katika nafasi nzuri ya kusaka tiketi ya hatua ya robo fainali, huku Kenya ikihitaji matokeo mazuri dhidi ya Senegal ili kujiweka katika mazingira ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

  9. Liverpool yaandaa ofa ya kwanza kumsajili Barcola kutoka PSG

    Liverpool imeongeza juhudi zake za kumsajili winga wa Paris Saint-Germain (PSG), Bradley Barcola, na inajiandaa kuwasilisha ofa yake ya kwanza kwa klabu hiyo ya Ufaransa.

    Barcola, mwenye umri wa miaka 23, ametajwa kuwa chaguo kuu la Liverpool katika harakati za kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mohamed Salah, aliyeondoka mwishoni mwa msimu uliopita.

    PSG inasema thamani ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa ni pauni milioni 145.

    Iwapo usajili huo utakamilika kwa kiasi hicho, utavunja rekodi ya uhamisho ghali zaidi kuwahi kufanyika nchini Uingereza. Hata hivyo, viongozi wa Liverpool wana matumaini ya kufikia makubaliano kwa ada inayokaribia pauni milioni 100.

    Barcola amebakiza miaka miwili katika mkataba wake na PSG, lakini inaelezwa kuwa yuko tayari kuhamia Liverpool akitafuta changamoto mpya, baada ya nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa Ufaransa kupungua.

    Awali, Liverpool ilikuwa ikimwania winga wa RB Leipzig Yan Diomande, lakini sasa mchezaji huyo anatarajiwa kujiunga na Real Madrid.

    Barcola alikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichofika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia la 2026.

  10. Marekani yashambulia tena Iran, Trump aahidi mashambulizi makali zaidi

    Jeshi la Marekani limesema limefanya mashambulizi mapya dhidi ya Iran usiku wa Alhamisi, likisema ni hatua ya kujibu shambulio lililolenga wanajeshi wake walioko Mashariki ya Kati mapema wiki hii.

    Haya ni mashambulizi ya kwanza ya Marekani dhidi ya Iran katika takriban wiki moja.

    Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti milipuko karibu na Kisiwa cha Qeshm na mji wa Abadan, kusini mwa nchi hiyo.

    Shirika la habari la serikali ya Iran, IRNA, limemnukuu afisa wa jimbo la Hormozgan akisema kuwa vikosi vya uokoaji vinaendelea kuwatafuta watu wawili wanaodaiwa kufunikwa na vifusi baada ya kuangukiwa na nyumba katika Kisiwa cha Qeshm.

    Mashambulizi hayo yamefanyika saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuahidi kuijibu Iran kwa "nguvu kubwa", kufuatia shambulio ambalo Tehran inadaiwa kulenga wanajeshi wa Marekani walioko Mashariki ya Kati.

    Siku ya Jumatano, jeshi la Marekani na lile la Jordan yalisema yalizuia makombora yaliyokuwa yamerushwa kuelekea Jordan, yakidai yalitoka Iran na yalilenga maeneo yenye wanajeshi wa Marekani.

    Katika taarifa yake, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema mashambulizi hayo ni "jibu kali" kwa kile ilichokiita mashambulizi ya Iran dhidi ya wanajeshi wa Marekani yaliyodhibitiwa siku iliyotangulia.

    Wakati huo huo, tovuti ya habari ya Marekani Axios, ikimnukuu afisa wa Marekani ambaye haikumtaja kwa jina, ilisema Washington ilikuwa imeanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Iran.

    Awali akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya White House, Trump alisema Marekani itaishambulia Iran "kwa nguvu kubwa".

    "Sasa ni zamu yetu," alisema Trump, huku akiongeza kuwa bado kuna uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano siku zijazo, lakini akasisitiza kuwa, "tutaishambulia kwa nguvu sana."

  11. Habari na karibu kwenye habari zetu za moja kwa moja