Waridi wa BBC: 'Kunyimwa haki ya kulea mwanangu, haikuzima shauku yangu kuwa muongoza watalii'

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

'Maisha yangu yalibadilika baada ya kupata mtoto nikiwa bado sijamaliza elimu yangu ya sekondari'.

Badala ya kupata msaada na ushirikiano kutoka kwa mzazi mwenzangu nilikumbana na maneno ya kukatisha tamaa.

Aliniambia kuwa sikuwa na uwezo wa kumlea mtoto huyo wala kufanya kazi kwa sababu alikuwa bado mdogo.

Glory Thobias 39 anasema kauli hiyo ilifungua ukurasa mpya wa maumivu, mapambano na maamuzi magumu katika maisha yake.

Licha ya jitihada zake za kupigania haki ya kukaa na mwanawe, ndoto hiyo haikutimia. Mzazi mwenzake aliondoka na mtoto huyo, akimuacha Glory akiwa na simanzi na maswali mengi yasiyo na majibu.

Mzigo wa maumivu ya kumkosa mtoto wake ulimsukuma kutafuta njia ya kujituliza na kujitafakari.

Glory anasema alifunga safari kwa mara ya kwanza 2013 kuelekea Mlima Kilimanjaro, safari ambayo mwanzoni aliiona kama njia ya kupunguza machungu yaliyokuwa moyoni.

Hata hivyo, Glory hakujua kuwa hatua hiyo ingekuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa ambayo yangelibadili kabisa maisha yake.

Niligundua kuwa wanawake waongoza watalii hawapo au ni wachache sana, wenyeji wangu mlimani waliniambia 'wanawake hawawezi kazi za huku si rahisi',pia mazingira ya kulala wakati mwingine ni ya kuchanganyika na wanaume hufanya wanawake kuonekana waliokosa maadili.

Nilipofanya utafiti wa haraka niliambiwa kuwa kazi ya uongozi wa watalii ni ngumu na si kila mtu anaweza kuifanya.

'Ukweli niliona wanaume wanaofanya kazi ya kuongoza watalii wana afya njema kama yangu, wana nguvu kama zangu, kwanini nisijaribu kuupima uwezo wangu?anasimulia Glory

Maneno hayo yalinifanya nifikirie sana, hasa niliposikia kauli kuwa mwanamke hawezi kuwa "fit wife" endapo atajihusisha na kazi hiyo.

Hapo ndipo nilipoamua moyoni mwangu kwamba sitaki kuishi kwa kuogopa maneno ya watu, bali nina ndoto zangu ninazotaka kuzitimiza.

Kwa mujibu wa serikali ya Tanzania sekta ya utalii inachangia ajira zaidi ya milioni 1.5 nchini Tanzania, lakini wanawake ni wachache kutokana na mitazamo ya mfumo dume inayodhani kuwa kazi za utalii, hasa za kuongoza watalii zinafaa zaidi kwa wanaume.

Glory Thobias, ambaye sasa anajivunia kuwa mmoja wa wanawake wanaowawezesha wasichana wa kaskazini mwa Tanzania, alijitambua kuwa ana uwezo mzuri wa lugha ya Kiingereza, jambo lililompa matumaini ya kupata kazi katika sekta ya utalii.

Glory anasema alimshirikisha baba yake ambaye mara zote aliamini katika uwezo wake licha ya changamoto alizopitia.

Baba alinirudisha shule,nilipomaliza Arusha sekondari alinihimiza kuendelea na masomo yaliyonipatia ujuzi wa kuongoza watalii.

Glory alichagua kusoma tabia za wanyama kwa kuwa alitamani kuwafahamu zaidi viumbe hao wa porini. Baadaye, alikutana na muongoza watalii aliyemweleza kuwa kampuni yao ilikuwa inatafuta waongoza watalii wa kike.

Alituma maombi na baadaye akaitwa kazini. Ingawa hakuwa na leseni ya kupanda milima mwanzoni, alifanya kazi kwa bidii hadi kampuni ikamtafutia leseni na kumfanya kuwa msaidizi wa uongozi wa watalii.

'Baadhi ya watu hudhani wanawake hawawezi kukabiliana na mazingira magumu ya porini'

Siku yake ya kwanza kazini ilikuwa ya msisimko mkubwa.

Alijawa na furaha ya kupata ajira na pia alikumbuka maneno yote ya kukatishwa tamaa aliyowahi kuambiwa.

Watalii wengi walivutiwa kumwona mwanamke akiongoza safari, jambo lililompa moyo na kuimarisha imani yake katika uwezo wake.

'Kila nikisikia watalii wananishangaa au kunizungumzia vizuri,nilijiskia vizuri' ilinifanya nifanye kazi yangu kwa kujituma' anasema Glory

"Nimegusa maisha ya wanawake 46 na kuwapa fursa katika sekta ya utalii. Haya yote nimefanikiwa kuyafanya baada ya kupata ufadhili kutoka kwa mtalii raia wa Marekani ambaye aliguswa na kazi yangu alipokuja kutembelea Mlima Kilimanjaro," anasema Glory Thobias.

Glory anakumbuka kuwa safari hiyo ndiyo iliyobadili maisha yake. Mtalii huyo aliugua ghafla akiwa mlimani na kulazimika kuondolewa mlimani na kupelekwa kupatiwa matibabu, huku watoto wake waliokuwa na umri wa miaka 13 na 14 wakibaki nyuma na baba yao kuendelea na safari chini ya uangalizi wa Glory.

Tukio hilo lilimgusa sana mtalii huyo aliyekuwa raia wa Marekani na kumuahidi Glory mualiko wa kwenda Marekani na kumuwezesha kutimiza ndoto yake katika .

Ahadi hiyo ilitimia, na baadaye akamlipia mafunzo katika chuo cha American Chamber of Commerce, hatua iliyompa maarifa na mtazamo mpana zaidi kuhusu biashara na uongozi.

"Ninafurahi kufanya kazi niliyoambiwa sitoweza," anasema Glory kwa kujiamini. Anaeleza kuwa watalii wengi hupendelea waongoza watalii wa kike kwa sababu wanawake wana uwezo mkubwa wa kusikiliza na kuelewa mahitaji ya wageni.

Hata hivyo, anakiri kuwa wanawake wengi katika taaluma hiyo hukumbana na changamoto ya kutoaminika. "Mara nyingi watu hudhani wanawake hawawezi kukabiliana na mazingira magumu ya porini, hasa wanapoonekana wakipiga kelele wanapokutana na wanyama wakali," anasema.

Mimi ni mfano hai, elimu ya wanyama imenisaidia kuwa na utulivu hata ninapokutana nao nikiwa katika shughuli zangu za kuongoza watalii mbugani.

'Dubu aliyepanda juu ya gari niliyokuwa nikiendesha hakutudhuru wala hatukuzua taharuki kutokana na kufahamu kanuni na taratibu kadhalika kuwaelewa wanyama na tabia zao ninapoongoza watalii mbugani' anasimulia Glory akitabasamu

'Wanawake wana uwezo mkubwa wa kusikiliza na kuelewa mahitaji ya wageni'

Mbali na kuwa muongoza watalii wa milimani, Glory Thobias ameanzisha jukwaa maalumu linaloitwa Serengeti Queens, ambalo linahudumia watalii wanawake wanaotembelea Tanzania.

Glorya anasema 'wanawake hupata mazingira salama na yenye msaada ambapo wanaweza kushirikishana uzoefu, maarifa na kuhamasishana ili kufikia nafasi za juu katika sekta ya utalii' ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Lengo la Serengeti Queens ni kuongeza ushiriki wa wanawake katika kuongoza watalii.

Kwa sasa, kati ya waongoza watalii wapatao 6,000 nchini Tanzania, wanawake ni wachache bado,alieleza Glory.

Aidha, chini ya wanawake 10 ndio wanaoweza kuendesha magari ya safari za utalii kutoka Arusha hadi Serengeti na kurudi.

'Ninajivuna kuwa miongoni mwa wenye uwezo huo'

Kutokana na hali hiyo, Glory na wenzake wamejiwekea lengo la kuongeza wanawake kutoka chini ya asilimia 1 hadi angalau asilimia 2 ya idadi ya waongoza watalii wanaume ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo.

Glory hushirikiana na vikundi mbalimbali vya wanawake vinavyotetea haki na maendeleo ya waongoza watalii wa kike.

Glory anasema kwamba kwa ujasiri, mshikamano na kujituma, wanawake wanaweza kuvunja vikwazo vya kijinsia na kufanikiwa katika sekta ambazo kwa muda mrefu zilionekana kuwa za wanaume pekee.

Kwa mtazamo wake, sekta ya utalii inahitaji wanawake wengi zaidi. "Sio kazi rahisi, lakini wanawake wanaweza kutoa mchango wa kipekee. Mimi nilisoma tabia za wanyama, elimu ambayo inanisaidia kuwaelewa vizuri. Twiga ni mnyama mzuri sana. Niliwahi kuchapisha video nikiwa natembea huku twiga akinifuata nyuma, na sikuwa na hofu."

Anajivunia kupitia kugusa maisha ya wasichana kutoka jamii zinazozunguka hifadhi kujifunza na kujiajiri.

"Kama msichana anaweza kufanya shughuli za nyumbani, basi kazi hizi za porini anaweza kuzifanya kwa ubora zaidi.

Ninaamini baada ya muda watakuwa waongoza watalii wazuri kama mimi. Hii ndiyo namna yangu ya kurudisha kwa jamii yangu," anasema Glory