Kombe la Dunia 2026: Mwaka huu ni mashindano kwa ajili ya matajiri pekee?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Marekani, Mexico na Canada zinatakuwa wenyeji wa mashindano ya Kombe la Dunia 2026. Timu 48 zitachuana katika viwanja 16 kutafuta mshindi wa mashindano hayo makubwa zaidi ya soka.

Lakini kumezuka malalamiko makubwa kuhusu gharama za kwenda uwanjani na kutazama mashindano haya. Mashabiki hasa nchini Marekani, wanalalamika juu ya bei kubwa ya tiketi.

Ndiposana, wanasheria wakuu wa Serikali wa jimbo la New York na New Jersey nchini Marekani wameanzisha uchunguzi rasmi kuhusu utendaji wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni (Fifa).

Mwanasheria mkuu wa New Jersey Jennifer Davenport anasema mchakato huo unatokana na "mkanganyiko, uhaba usio wa kweli viti na bei za juu za tiketi."

Anasema kutakuwa na "uchunguzi wa kina wa mwenendo wa Fifa" huku shirikisho hilo linaloongoza la mpira wa miguu duniani likiitwa kutoa maelezo rasmi.

Davenport alitoa tangazo la pamoja na mwanasheria mkuu wa New York Letitia James na idara ya ulinzi wa watumiaji na wafanyakazi ya Jiji la New York (DCWP).

Kilio cha mashabiki wa soka kimeshika kasi ulimwenguni kutokana na kupanda kwa bei za tiketi za Kombe la Dunia 2026. Mfumo mpya ulioanzishwa na FIFA umezua mtafaruku mkubwa.

Shida iko wapi?

Bei za tiketi za mashindano sio tu kwamba ni kubwa kuliko Makombe ya Dunia yaliyopita, pia kwa mara ya kwanza, FIFA imeanzisha bei inayobadilika, na kusababisha bei kuwa juu sana kwa michezo mingi ya Kombe la Dunia.

Mfano ni kwa mechi ya fainali, iliyopangwa kufanyika New Jersey Julai 19. Awali FIFA iliuza tiketi kwa gharama kubwa ya dola $6,730 — tayari ni kubwa kuliko bei ya dola $1,600 kwa tiketi kwa Kombe la Dunia la FIFA la 2022 huko Qatar.

Kufikia dirisha la mwisho la mauzo kuanzia Aprili, aina hiyo hiyo ya tiketi iligharimu $10,990.

Bei hizo zimesababisha hasira kubwa. Hata Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye ana uhusiano wa karibu na Infantino, aliambia New York Post kwamba hawezi kulipa takriban dola 1,000 ili kupata kiti cha kukaaa kwa ajili ya mchezo wa ufunguzi wa Marekani dhidi ya Paraguay mwezi ujao.

Kuzidisha tatizo hilo, FIFA mwezi wa Aprili ilizindua aina mpya kabisa ya tiketi zinazoitwa viti vya mbele. Ni viti vya mstari wa mbele katika uwanja wote, tiketi zimeuzwa kwa bei kubwa kwa viti hivyo.

Kiti cha mstari wa mbele kwenye jukwaa la chini kwa fainali kinagharimu zaidi ya dola $30,000.

Changamoto nyingine kubwa juu ya mauzo ya tiketi za Kombe la Dunia ni kwamba mashabiki hawawezi kuchagua kiti mwanzo mwa mchakato wa kununua tiketi.

Mashabiki wanapewa chaguzi za aina nne za tiketi; baadaye hupewa viti na FIFA. Hilo si jambo la kawaida nchini Marekani, ambapo mashabiki wamezoea kuchagua kiti wanachotaka wakati wa ununuzi.

Ramani za viti kwa viwanja vingi kama kile kilicho New Jersey inaonyesha tiketi za aina moja - au zile za gharama kubwa zaidi – ambazo ni viti vilivyoko mbele katika safu ya chini.

Hakuna njia ya kujua ni viti vingapi vilivyobaki katika sehemu yoyote - na mashabiki wengi walionunua tiketi hizo za bei ghali wamelalamika kwamba wamepata viti ambavyo hawajapendezwa navyo, kama vile nyuma ya kona.

Kombe hili la Dunia si mara ya kwanza FIFA kutumia mfumo huu wa tiketi mfumo huu, lakini ni mara ya kwanza kutoza bei kubwa hivyo, na kuzua hasira miongoni mwa mashabiki wanaohisi wametozwa ada kubwa kupita kiasi.

Vilevile FIFA ina haki ya kubadilisha kiti chako. Ina maana shabiki ambaye alidhani amenunua tiketi ya kukaa safu ya juu, anaweza kuishia katika kiti cha safu ya chini.

Fifa inasemaje?

Rais wa FIFA Gianni Infantino amejibu alipoulizwa kuhusu bei ya tiketi kuwa kubwa katika Kombe la Dunia: kwa kusema kwamba, wanaendana na hali ilivyo kwenye soko la Amerika Kaskazini.

Huo ndio uhalali ambao FIFA imeutumia kupandisha kwa kasi bei ya tiketi kwa Kombe la Dunia litakalofanyika Marekani, Mexico na Canada msimu huu wa joto ikilinganishwa na mashindano yaliyopita.

Pia rais Infantino ametetea gharama ya tiketi kwa kusema, inaonyesha hamu ya umma ya mashindano hayo.

FIFA inaendelea kuhalalisha bei zake za tiketi ikisema Kombe hili la Dunia linaweza kuipatia zaidi ya dola bilioni 11 kama faida, ikiwa ni pamoja na mikataba ya matangazo.

Wapenzi wa soka wanalalamika kuwa bei kubwa inageuza mchezo wa umma kuwa anasa ya matajiri pekee, ikiondoa usawa na ujumuishi. Huku mamlaka za kisheria nchini Marekani zikianzisha uchunguzi dhidi ya FIFA kwa madai ya unyonyaji na kutengeneza uhaba usio wa kweli wa tiketi ili kupandisha bei. Swali ni:

Je, unaweza kumudu Kombe la Dunia la 2026?