Moja kwa moja, Wagonjwa wa Ebola wa Nigeria na Kenya huenda walikutana Uganda

Maafisa wanasema wagonjwa hao walisafiri kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe nchini Uganda mnamo tarehe 3 Oktoba.

Muhtasari

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Rais Zelensky aishtumu Urusi kwa kutumia mabomu ya vishada dhidi ya Kyiv

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky
    Maelezo ya picha, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ameishtumu Urusi kwa kutumia makombora na mabomu ya vishada katika mashambulizi yaliyofanyika usiku wa kuamkia leo.

    Watu wanne wameuawa katika mashambulizi hayo mjini Kyiv na maeneo mengine, kulingana na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Ukraine. Zelensky amesema watu 34, wakiwemo watoto watano, pia wamejeruhiwa.

    Katika taarifa yake kwenye mtandao wa X, Zelensky amesema,“Usiku wa kuamkia leo, Warusi wametumia makombora matatu ya balistiki yenye vichwa vya mabomu ya vishada, miongoni mwa silaha nyingine, dhidi ya Kyiv.”

    Alisema sifa ya kipekee ya makombora hayo ni kwamba hulipuka hewani yanapofika karibu na shabaha, na kushambulia kila kitu ndani ya eneo lengwa.

    Mabomu ya vishada yamepigwa marufuku katika zaidi ya nchi 100 chini ya Mkataba wa Mabomu ya Vishada, uliopitishwa mwaka wa 2008. Silaha hizi hurusha vilipuzi vidogo katika eneo kubwa, hali inayoweza kusababisha mashambulizi kulenga maeneo ya raia.

    Hata hivyo, Urusi na Marekani si miongoni mwa nchi zilizosaini mkataba huo.

    Soma pia:

  2. Maandamano yazuka Tunisia baada ya kifo cha mwanaume aliyekuwa akizuiliwa na polisi

    .

    Polisi nchini Tunisia wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji katika eneo la Ettadhamen, viungani mwa mji mkuu,Tunis, baada ya kifo cha mwanamume aliyekuwa amezuiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

    Kumekuwa na makabiliano kati ya polisi na waandamanaji katika miji miwili ya kusini mwa Tunisia.

    Makabiliano ya hapo jana yametokea wakati nchi hiyo inakabiliwa na kuongezeka kwa mgogoro wa kiuchumi, kijamii na kisiasa, hali inayozidisha hofu ya kutokea kwa wimbi kubwa zaidi la maandamano kutokana na hasira za wananchi kuhusu kudorora kwa hali ya maisha na huduma duni za umma.

    Familia ya mwanamume huyo imesema alifariki kutokana na vitendo vya ukatili wa maafisa wa polisi baada ya kukamatwa. Familia hiyo imetaka mazingira ya kifo chake yafafanuliwe na waliohusika wawajibishwe.

    Hata hivyo, vyombo vya habari vya eneo hilo vimeripoti kuwa mwanamume huyo alifariki baada ya kumeza dawa za kulevya. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia bado haijatoa maoni kuhusu tukio hilo.

    Soma pia:

  3. Trump aishtumu Iran kwa kuchochea kupanda kwa bei ya mafuta

    .
    Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump ameishtumu Iran kwa kufanya kila juhudi kuongeza bei ya mafuta kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Bunge la Marekani.

    Trump amesema kuwa Iran inatunga taarifa kuhusu mashambulizi, mabomu ya baharini na matukio mengine katika Mlango Bahari wa Hormuz, akidai kuwa hatua hizo zinalenga kupandisha bei ya mafuta.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema kiasi cha mafuta kinachosafirishwa kupitia Mlango Bahari wa Hormuz kwa sasa ni kikubwa kuliko ilivyokuwa awali kabla ya kuanza kwa mzozo huo.

    Kauli hiyo inajiri huku Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran likitishia kulenga kambi za kijeshi za Marekani zilizoko Mashariki ya Kati iwapo jeshi la Marekani litaendelea kusindikiza meli zinazopita katika Mlango Bahari wa Hormuz.

    Iran imezuia usafirishaji wa meli katika njia hiyo muhimu kwa usambazaji wa nishati duniani tangu kuanza kwa vita tarehe 28 Februari, huku ikishambulia mara kwa mara meli zinazojaribu kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz bila idhini yake.

    Soma pia:

  4. Eneo la Tibet lashuhudia tetemeko kubwa la ardhi, zaidi ya watu 16 wamefariki

    .

    Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha 7 katika kipimo cha Richter, limetokea eneo la Nagqu, eneo kubwa la milima kaskazini mashariki mwa Lhasa, mji mkuu wa Tibet, hii ni kulingana taarifa za vyombo vya habari vya eneo hilo.

    Takriban watu 16 wamefariki dunia, huku idadi ya waliojeruhiwa ikifikia 65, wakiwemo watu 11 waliojeruhiwa vibaya.

    Mamia ya nyumba zimebomoka katika eneo hilo, barabara na huduma za umeme zimekatika katika maeneo yaliyoathiriwa.

    Kulingana na shirika la habari la serikali ya China,Xinhua, takriban nyumba 339 zimebomoka, huku tathmini ya kiwango cha uharibifu ikiendelea.

    Hili ndilo tetemeko la ardhi lililosababisha vifo vingi zaidi katika eneo hilo tangu mwaka wa 2023, ambapo watu 120 walifariki kufuatia tetemeko la ukubwa wa 6.2 katika mkoa jirani wa Gansu nchini China.

    Rais wa China, Xi Jinping, ametoa agizo la kuanzishwa kwa operesheni kubwa ya uokoaji kufuatia tetemeko hilo.

    Tibet ni mojawapo ya maeneo yanayofuatiliwa kwa karibu zaidi nchini China. Upatikanaji wa taarifa katika eneo hilo unadhibitiwa kwa kiasi kikubwa na serikali ya China, huku uandishi huru wa habari ukikabiliwa na vikwazo vingi.

    Soma pia:

  5. Tetesi za Soka Ulaya: Man United yatafuta kocha, Conte na Howe watajwa

    Eddie Howe
    Maelezo ya picha, Kocha wa Newcastle United, Eddie Howe

    Mkurugenzi wa ufundi wa Manchester United, Jason Wilcox, anaripotiwa kumpendelea aliyekuwa kocha wa Newcastle United, Eddie Howe, iwapo klabu hiyo itamfuta kazi Michael Carrick. (Talksport)

    Julian Nagelsmann ameibuka miongoni mwa makocha wanaopigiwa upatu kuchukua nafasi ya Michael Carrick Manchester United iwapo ataondoka, huku akiripotiwa kuvutiwa na kazi hiyo. (Telegraph - inahitaji usajili)

    Kocha wa Aston Villa, Unai Emery, pia ni miongoni mwa wagombea wanaotajwa kuchukua nafasi ya Carrick Manchester United. (i News)

    Manchester United imeanza mazungumzo na aliyekuwa meneja wa Chelsea na Tottenham, Antonio Conte, kuhusu uwezekano wa kurejea kwake katika Ligi Kuu ya England. (La Repubblica - kwa Kiitaliano)

    Manchester United huenda ikalazimika kulipa ada kubwa zaidi endapo itaammua kumchukua Fabian Hurzeler kutoka Brighton kuchukua nafasi ya Carrick. (Telegraph - inahitaji usajili)

    Hata hivyo, kocha wa Brighton, Hurzeler, haonekani kuwa na nia ya kujiunga na Manchester United iwapo nafasi hiyo itakuwa wazi. (Talksport)

    Arsenal inalenga kumsajili winga wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Hispania, Alex Baena (25), mshindi wa Kombe la Dunia, katika dirisha la usajili la Januari. (FootballTransfers)

    Arsenal pia inamfuatilia mshambuliaji wa Monza, Gustavo Varela (21), huku Napoli na Benfica nazo zikionyesha nia ya kumsajili nyota huyo wa Ureno. (Gazzetta dello Sport - kwa Kiitaliano)

    Bayer Leverkusen inamtaka beki wa Brazil, Gleison Bremer, na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 anaweza kuondoka Juventus mwezi Januari. (Gazzetta dello Sport - kwa Kiitaliano)

    Soma pia:

  6. Raia wa kigeni apigwa hadi kufa na umati wa watu Afrika Kusini

    Picha ya zamani ya maandamano ya March to March yakupinga wahamiaji
    Maelezo ya picha, Picha ya zamani ya maandamano ya March to March yakupinga wahamiaji

    Raia wa kigeni ameuawa kwa kupigwa na umati wa watu zaidi ya 50 katika mji wa Durban, Afrika Kusini, polisi wa eneo hilo wamesema.

    Kulingana na polisi, mwanamume huyo ambaye utambulisho wake haujafahamika, na anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 40, alisimamishwa kwanza na wanaume wawili kando ya barabara kabla ya kushambuliwa na kundi kubwa la watu. Aliaga dunia katika eneo la tukio.

    Polisi nchini Afrika Kusini wameanzisha uchunguzi kuhusu mauaji hayo, huku sababu ya shambulio hilo ikiwa bado haijabainika.

    Mauaji hayo yanajiri wakati kumekuwa na wimbi la maandamano dhidi ya wahamiaji nchini Afrika Kusini mwaka huu, huku baadhi ya maandamano yakigeuka kuwa ya vurugu.

    Mapema mwezi huu, maduka na magari yalichomwa moto mjini Durban na pia Soweto, karibu na mji wa Johannesburg.

    Msemaji wa polisi wa jimbo hilo, Robert Netshiunda, ameiambia BBC kuwa polisi hawawezi kuthibitisha sababu ya mauaji hayo ya Durban, na kwamba taarifa zaidi zitatolewa baada ya uchunguzi kufanywa.

    Aidha serikali ya Afrika Kusini, imewataka waandamanaji kuendesha maandamano yao kwa amani, huku pia ikikubali haja ya kufanya mageuzi katika mfumo wa uhamiaji.

    Kundi moja lililo nyuma ya maandamano hayo, la March and March, awali lilikuwa limetoa makataa ya tarehe 30 mwezi Juni kwa wahamiaji wote wasio na vyeti halali kuondoka Afrika Kusini.

    Soma pia:

  7. Trump: Musk amerejesha huduma ya Starlink kwa Ukraine

    Askari wa Ukraine akitumia kifaa cha intaneti ya satelaiti ya Starlink, kinachounganishwa na maelfu ya satelaiti za kampuni ya SpaceX.
    Maelezo ya picha, Askari wa Ukraine akitumia kifaa cha intaneti ya satelaiti ya Starlink, kinachounganishwa na maelfu ya satelaiti za kampuni ya SpaceX.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa Elon Musk amerejesha huduma ya mtandao wa satelaiti wa Starlink kwa Ukraine baada ya vikwazo vilivyoathiri mawasiliano ya vikosi vya Ukraine.

    Kauli hiyo imekuja baada ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kusema kuwa huduma za Starshield, mtandao wa kijeshi unaotegemea mfumo wa Starlink, zilikuwa bado hazijarejeshwa kikamilifu.

    Awali, Musk alikanusha madai kuwa alihusika katika kuvurugwa kwa huduma hiyo. Usumbufu huo ulitajwa kuathiri uwezo wa Ukraine kutumia ndege zisizo na rubani (droni) katika mashambulizi dhidi ya Urusi na katika kujilinda dhidi ya mashambulizi ya adui.

    Alipoulizwa kuhusu taarifa kwamba alimuomba Musk kuondoa vikwazo hivyo, Trump hakuthibitisha moja kwa moja madai hayo, lakini alisema: "Jambo muhimu ni kwamba huduma hiyo imerejeshwa."

    Utawala wa Trump pia umewahi kukanusha madai kwamba uliiagiza kampuni ya Musk kudhibiti huduma hiyo.

    Vikwazo hivyo vya mawasiliano vilikuja wakati Trump alipokuwa akimshinikiza Zelensky kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta ya Urusi, akidai kuwa mashambulizi hayo yalichangia kupanda kwa bei za nishati.

    Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani mwezi ujao, Trump ameondoa baadhi ya vikwazo dhidi ya Urusi na kuruhusu uagizaji wa dizeli kutoka Urusi kuingia katika soko la Marekani. Hatua hiyo imekosolewa na Ukraine pamoja na washirika wake wa Ulaya.

    Maelezo zaidi:

  8. Mke wa mwanadiplomasia wa Uswisi apatikana na Ebola Nigeria

    .

    Mke wa mwanadiplomasia wa Uswizi anayehudumu katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, ambaye nimzaliwa wa Uganda, ndiye mgonjwa anayepokea matibabu ya Ebola nchini Nigeria, Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Uswizi imesema.

    Katika taarifa yake kwa shirika la habari la Reuters, wizara hiyo imesemainaaminika kuwa mwanamke huyo aliambukizwa virusi hivyo alipokuwa akisafiri nchini Uganda.

    Mumewe, ambaye aliandamana naye katika safari hiyo, pia ametengwa kwa uangalizi wa kitabibu, lakini bado hajaonyesha dalili zozote za ugonjwa huo.

    Kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia magonjwa (Africa CDC) kinachunguza uwezekano wa mwanamke huyo kukutana na mgonjwa wa kwanza wa Ebola aliyethibitishwa nchini Kenya alipokuwa akisafiri kupitia Uganda mapema mwezi huu.

    Inaaminika kuwa wagonjwa hao wote wawili walipitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe nchini Uganda tarehe 3 mwezi Oktoba, ingawa hadi sasa hakuna uhusiano uliothibitishwa kati yao.

    Bado kuna maswali kuhusu mahali ambapo mwanamke huyo aliambukizwa virusi hivyo.

    Awali, Uganda ilisema kuwa mwanamke huyo alikuwa amesafiri hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambako mlipuko wa sasa wa Ebola umeenea. Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO), Africa CDC na Wizara ya Afya ya Nigeria zimesema hazijapokea taarifa zilizothibitishwa kuthibitisha safari hiyo.

    Mamlaka za Nigeria zimesema awali kuwa watu 44 ambao huenda walikutana na mwanamke huyo na kuathiriwa na virusi hivyo walikuwa wametambuliwa na kuagizwa kujitenga. Hata hivyo, maafisa wa Africa CDC walisema Alhamisi kuwa watu wengine zaidi walikuwa wametambuliwa, ingawa hawakutaja idadi hiyo mpya.

    Nchini Kenya, mamlaka za afya pia zimethibitisha kuwa watu wote 135 waliokutana na mgonjwa wa kwanza wa Ebola nchini humo wametambuliwa na kutengwa.

    Kenya imerekodi visa tisa vya Ebola vilivyothibitishwa hadi kufikia sasa, vinavyohusishwa na msafiri aliyesafiri kutoka DRC hadi Kenya kupitia Uganda.

    Waziri wa Afya wa Nigeria alisema Alhamisi kuwa mamlaka hazina ushahidi wowote unaoonyesha kuwa kisa cha Ebola kilichothibitishwa hivi karibuni nchini humo kimeenea katika jamii. Ameelezea kuwa ni kisa hicho kimoja tu ambacho kimedhibitiwa.

    Soma pia:

  9. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Ijumaa ya leo