Kushuka kwa takwimu rasmi za Ebola ni habari njema, lakini hatari bado ipo

Kupungua huko kunatokana na data bora zaidi, baada ya maabara kuweza kuwatenga wagonjwa wengi waliokuwa na homa lakini wakisumbuliwa na magonjwa mengine kama malaria, ambayo ni ya kawaida DRC.

Muhtasari

Skip Video and continue reading
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • xx
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Kushuka kwa takwimu rasmi za Ebola ni habari njema, lakini hatari bado ipo

    Wahudumu wa afya

    Chanzo cha picha, EPA

    Takwimu za hivi karibuni za Ebola kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinaonekana kutoa matumaini baada ya idadi ya visa kupungua kwa kiasi kikubwa.

    Awali, mamlaka zilikuwa zikizungumzia zaidi ya visa vinavyoshukiwa 1,000 na karibu vifo vinavyoshukiwa kuwa 250.

    Sasa zinaripoti takribani visa 380 vilivyothibitishwa nchini DRC, ikiwemo vifo 60, pamoja na visa vingine 15 vilivyothibitishwa na kifo kimoja nchini Uganda.

    Hata hivyo, tofauti muhimu ni kwamba sasa mamlaka zinazungumzia visa vilivyothibitishwa, badala ya vinavyoshukiwa kama ilivyokuwa awali.

    Kwa hiyo ni kosa kudhani kushuka kwa idadi kunamaanisha mlipuko huo umepungua hatari ghafla.

    Kupungua huko kunatokana na data bora zaidi, baada ya maabara kuweza kuwatenga wagonjwa wengi waliokuwa na homa lakini wakisumbuliwa na magonjwa mengine kama malaria, ambayo ni ya kawaida DRC.

    Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema mlipuko huo ulikuwa na “mwanzo wa haraka sana” lakini timu za kushughulikia sasa “zinaanza kuufikia”.

    Hata hivyo, mojawapo ya changamoto kubwa bado ni ufuatiliaji wa watu waliokaribiana na wagonjwa.

    Ni takriban asilimia 45 tu ya watu waliokaribiana moja kwa moja na mgonjwa wa Ebola wanafuatiliwa kwa sasa, kwa sehemu kutokana na eneo la chanzo cha mlipuko kuwa katika eneo lililoathiriwa na migogoro.

    Unaweza kusoma;

  2. Ukraine yasema imezishambulia meli tano zilizokuwa zikibeba mizigo haramu katika maji ya pwani ya maeneo yanayodhibitiwa na Urusi

    Mlipuko baharini

    Chanzo cha picha, Observator Antena1

    Ukraine imesema imezishambulia meli tano zilizokuwa zikibeba mizigo haramu katika Bahari ya Azov na katika maji ya pwani ya maeneo yanayodhibitiwa na Urusi.

    Kamanda wa vikosi vya droni vya Ukraine alisema meli hizo zilihusika na “wizi” wa nafaka za Ukraine, pamoja na kusafirisha mizigo ya kijeshi na mafuta.

    Mashambulizi hayo yanajiri wakati Rais wa Urusi Vladimir Putin akihutubia kongamano kubwa la kiuchumi mjini St Petersburg, siku moja baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kutoa wito wa mazungumzo ya ana kwa ana na kiongozi huyo wa Urusi kuhusu kumaliza vita.

    Wakati huohuo, Ukraine imethibitisha kuwa moja ya droni zake za majini ililipuka karibu na pwani ya Romania siku ya Ijumaa. Hakuna majeruhi walioripotiwa katika tukio hilo.

    Zelensky aliandika pamoja na wito wake wa hivi karibuni wa mazungumzo ya amani kwamba Warusi wamechoka na mashambulizi ya droni na makombora ya Ukraine, uhaba wa petroli na kupanda kwa bei ambako vita hivyo, vinavyoingia mwaka wa nne, vimesababisha.

    Ukraine imekuwa ikilenga mara kwa mara miundombinu ya kijeshi na nishati ndani ya Urusi ili kupunguza uwezo wake wa kupigana vita.

    Kuwasili kwa Putin mjini St Petersburg kunakuja siku moja baada ya Kyiv kufanya shambulizi la droni katika viunga vya jiji hilo.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Azerbaijan imethibitisha kuwa raia wake watano waliuawa katika mashambulizi dhidi ya meli mbili katika Bahari ya Azov.

    Haikubainisha ni nani aliyekuwa kwenye mipango ya mashambulizi hayo na ilibainisha kuwa meli hizo hazikuwa za Azerbaijan.

    Awali, Robert Brovdi, kamanda wa droni wa Ukraine, alitangaza kwamba meli tano “zinazozurura kinyume cha sheria” zilishambuliwa usiku katika bandari za Mariupol, Berdyansk na katika maji ya pwani ya maeneo ambayo Ukraine inaita “maeneo yanayokaliwa kwa muda”, sehemu za nchi hiyo ambazo kwa sasa zinadhibitiwa na Urusi.

    Alisema majina ya meli hizo tano, ambazo zilijumuisha meli za mizigo na meli za mafuta, yalifutwa na rada zao zikazimwa “kwa lengo la kuiba kimyakimya nafaka za Ukraine”, pamoja na “kusafirisha mizigo ya kijeshi na mafuta”. Wizara ya Mambo ya Nje ya Azerbaijan ilitaja majina ya meli mbili kuwa Nastra na Circon.

    Brovdi hakutaja uwepo wa vifo vyovyote.

    Unaweza kusoma;

  3. Mwanahabari wa Marekani akutwa na hatia kwa kufanya kazi kama wakala wa China

    Bendera

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanahabari wa Marekani ambaye alikuwa akiishi na kufanya kazi nchini China kwa zaidi ya muongo mmoja amekiri hatia katika mahakama ya Marekani kwa kufanya kazi kama wakala haramu wa Jamhuri ya Watu wa China (PRC).

    Thomas Weir Pauken II, 50, “alikiri kuwa sehemu ya njama ya kupata taarifa nyeti kutoka serikali ya Marekani” kwa niaba ya China, alisema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Marekani anayehusika na usalama wa taifa, John A. Eisenberg.

    Nyaraka za mahakama zinaonesha kuwa Pauken alikuwa akiishi China tangu mwaka 2010 na alikuwa amefanya kazi na mashirika kadhaa ya vyombo vya habari huko, ikiwa ni pamoja na China Central Television na Xinhua News.

    Kwa mujibu wa nyaraka hizo, Pauken alifanya kazi “kwa maelekezo na udhibiti wa watu aliowajua kuwa wanahudumu kwa niaba ya PRC” kuanzia mwaka 2019 hadi Februari mwaka huu.

    Miongoni mwa watu aliowasiliana nao ni mtu anayejulikana kama “Cathy”, ambaye Wizara ya sheria ya Marekani (DOJ) ilisema alimpa “maelekezo, ikiwa ni pamoja na kukutana na watu wanaoweza kuwa vyanzo vya taarifa za kijasusi”.

    Pauken na “Cathy” walitambulishwa na mtu aliyekuwa mwandishi wa hotuba wa Rais wa China Xi Jinping wakati wa “vita vya biashara kati ya Trump na China” mwaka 2017, kulingana na nyaraka za mahakama.

    DOJ ilisema mwanahabari huyo wa Marekani alipokea takribani dola 100,000 kutoka kwa “Cathy” kwa kazi hiyo.

    Pauken pia aliagizwa kusafiri mara kadhaa kati ya mwaka 2019 na 2025 kukutana na watu nchini Marekani ambao wangeweza kumpa taarifa za kuzipeleka kwa PRC.

    Mwanahabari huyo wa Marekani “alikusanya taarifa za kiintelijensia kuhusu watu aliolenga Marekani na kuzipeleka kwa wasimamizi wake wa ujasusi wa China,” alisema Mkurugenzi Msaidizi Roman Rozhavsky wa Kitengo cha Ujasusi na Usalama wa Ndani cha FBI.

    Rozhavsky aliongeza kuwa kesi hiyo ni mfano wa “hatua kubwa ambazo Chama cha Kikomunisti cha China kiko tayari kuchukua ili kudhoofisha taasisi zetu za kidemokrasia na kupunguza uhuru wetu wa kisiasa”.

    Pauken alifanya kazi na watu wengine wawili nchini China, wanaotambuliwa kama “William” na “Richard”, ambao walimwambia mwanahabari huyo kwamba ripoti alizowaandikia zilikuwa zikipelekwa Japan.

    Pia Pauken alitoa kwa kundi la watu kutoka Wuhan taarifa kuhusu Wizara ya Sheria ya Marekani (DoJ) na taarifa kuhusu teknolojia. Pia waliomba Pauken awasaidie kupata mtaalamu wa kuwasaidia katika kufanya ujasusi wa kimtandao.

    Baada ya kusikilizwa kwa kesi hiyo Alexandria, Virginia, wakili wa Pauken, Charles Burnham, alitoa taarifa kwa Politico iliyosema mteja wake anakubali kuwajibika na alikuwa akijaribu “kukuza uhusiano wa amani na kuendeleza sababu ya uhuru wa dini nchini China”.

    Pauken anatarajiwa kuhukumiwa tarehe 1 Septemba na anakabiliwa na adhabu ya juu ya kifungo cha miaka 10 jela.

    Unaweza kusoma;

  4. Hezbollah yakataa makubaliano mapya ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon

    Mlipuko

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kundi la wanamgambo la Lebanon la Hezbollah limekataa masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon yanayoungwa mkono na Marekani.

    Katika taarifa kali, kiongozi wa kundi hilo linaloungwa mkono na Iran, Naim Qassem, alisema mazungumzo hayo yalikuwa “yasiyo na faida” na “ya kudhalilisha” kwa Lebanon, na kwamba yamekataliwa kabisa na “sehemu kubwa za wananchi wa Lebanon”.

    Hatua hii inakuja baada ya Israel na Lebanon kutangaza kurejeshwa kwa makubaliano yao dhaifu ya kusitisha mapigano, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa maeneo ya “majaribio” ya usalama ndani ya Lebanon ambako wapiganaji wa Hezbollah hawataruhusiwa. Pia ilitaka Hezbollah kusitisha mashambulizi dhidi ya Israel.

    Donald Trump baadaye alisema kuwa alizungumza na Hezbollah na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kwamba maendeleo yalikuwa yanafanyika.

    Trump aliongeza: “Nadhani mtashuhudia mambo yakitokea huko.”

    “Itakuwa jambo zuri sana kama Lebanon ingepata amani. Lebanon imekuwa chini ya mashambulizi kwa miaka mingi na mara nyingi kama upande dhaifu, na itakuwa vizuri sana kama hilo lingeweza kumalizika,” alisema.

    Kabla ya kauli za Trump, kiongozi wa Hezbollah, ambayo haikushiriki katika mazungumzo hayo, alisema kwamba “usitishaji mapigano unaodhaniwa,” unaofasiriwa kama Hezbollah kusitisha mapigano na kuondoa wapiganaji wake kutoka mstari wa kusini na Israel, ni sawa na kujisalimisha na utafanikisha malengo ya Israel.

    Unaweza kusoma;

  5. Mke wa zamani wa mpwa wa mtawala wa Dubai ashikiliwa na polisi, waendesha mashtaka wasema

    Javadli

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Mke wa zamani wa mpwa wa mtawala wa Dubai amekamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi, mamlaka zimesema, wakati mvutano wa kisheria kuhusu malezi ya binti zao watatu ukiendelea kuongezeka.

    Ofisi ya Mashtaka ya Umma ya Dubai iliiambia BBC kuwa Zenab Javadli alikamatwa kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na baba wa watoto hao watatu, mume wake wa zamani, Sheikh Saeed bin Maktoum bin Rashid Al Maktoum.

    Familia na marafiki wa Javadli walikuwa wamepoteza mawasiliano naye tangu Jumanne usiku na walitoa tahadhari kuhusu aliko.

    Kwa karibu siku mbili, hakukuwa na taarifa yoyote kuhusu mahali alipo Javadli au watoto wake.

    Kwa miezi kadhaa, alikuwa akitoka nyumbani kwa nadra sana kwa sababu aliamini maafisa wa usalama walikuwa wakisubiri kuwachukua watoto wake na kumkamata.

    Kwa mujibu wa Ofisi ya Mashtaka ya Umma ya Dubai, mume wake wa zamani amedai kuwa aliteka nyara watoto wakati wa kikao cha kuwatembelea kilichoidhinishwa na mahakama.

    Mwaka jana, aliwasilisha malalamiko polisi akimshutumu kwa kuwateka nyara binti zao.

    Hilo lilitokea baada ya watoto hao kubadilishana mikono kati ya wazazi wao mara kadhaa, huku kila upande ukimshutumu mwingine kwa utekaji nyara.

    Hii ina maana kwamba watoto hao walikuwa wakipokezwa kati ya wazazi wao mara kadhaa, na kila mzazi alikuwa akimshutumu mwenzake kwa kuwateka nyara watoto hao.

    Javadli, aliyekuwa mwanamichezo wa viungo wa kimataifa, pia amekuwa akikabiliwa na uwezekano wa kukamatwa kwa tuhuma za uhalifu wa mtandaoni katika UAE baada ya kurusha moja kwa moja mtandaoni moja ya mizozo hiyo mwaka jana.

    Wakati huo, alieleza vitendo vyake katika ujumbe wa video kwa mwanasheria wa haki za binadamu wa Uingereza David Haigh, ambaye amekuwa akimtetea:

    “Nalijua kwamba hiyo ilikuwa ni nafasi ya mwisho kuwa na watoto wangu kwani wasingeniruhusu tena kuwaona. Kwa kweli nilihisi kwamba hiyo ilikuwa ni nafasi yangu ya mwisho, hivyo nikaingia mubashara na kuomba msaada.”

    Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi jioni, Ofisi ya Mashtaka ya Umma ya Dubai ilisema kuwa suala hilo bado linaendelea kuchunguzwa na liko chini ya taratibu za kisheria zinazoendelea.

    “[Sisi] tutaendelea kuchukua hatua zinazohitajika za kisheria kwa mujibu wa sheria zinazotumika, huku tukilinda ustawi na maslahi bora ya watoto,” iliongeza.

    Kwa upande wake, Haigh alitoa wito kwa UAE kumruhusu Javadli kupata mara moja huduma za wakili wake, ubalozi wake na familia yake, na aachiliwe arudi nyumbani kwake Dubai.

  6. Xi Jinping kukutana na Kim Jong Un katika ziara adimu Korea Kaskazini

    Xi Jinping

    Chanzo cha picha, POOL / AFP via Getty Images

    Rais wa China Xi Jinping atakutana na Kim Jong Un wiki ijayo katika ziara ya Korea Kaskazini, ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika takriban miaka saba, kulingana na vyombo vya habari vya serikali vya nchi zote mbili.

    Xi atakuwa Korea Kaskazini kuanzia tarehe 8 hadi 9 Juni kwa mwaliko wa Kim. Ziara yake ya mwisho Pyongyang ilikuwa mwaka 2019.

    Ziara hiyo inakuja wiki chache baada ya Xi kumpokea Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Beijing, nchi mbili ambazo zina ushawishi mkubwa katika sera za nje za Pyongyang.

    China ni mshirika muhimu wa kiuchumi na kisiasa wa Korea Kaskazini, ambayo inakabiliwa na vikwazo vikubwa vya kimataifa kutokana na mpango wake wa silaha za nyuklia na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

    China na Korea Kaskazini zina mpaka wa kilomita 1,400 na zimeunganishwa na mkataba wa ulinzi, wa pekee kwa China na nchi nyingine yoyote. Mkataba huo unahakikisha msaada wa pamoja ikiwa mojawapo itashambuliwa.

    Mwaka huu unaadhimisha miaka 65 ya mkataba huo.

    Kwa Kim, thamani ya ki-propaganda ya ziara ya Xi ni dhahiri. Korea Kaskazini imeboresha nafasi yake kimataifa baada ya janga la COVID-19 na kuingia katika vita vya Ukraine upande wa Urusi.

    Licha ya uhusiano wa karibu wa Beijing na Pyongyang na Moscow, Xi ana wasiwasi kuhusu uhusiano unaokua kati ya Kim na Putin.

    Lakini Beijing, ambayo ni mshirika mkubwa zaidi wa biashara wa Korea Kaskazini, bado ndiyo njia kuu ya uhai wa kiuchumi kwa Kim.

    Inatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuwa Kim atatafuta kuongeza biashara kupitia mpaka wa nchi kavu na kuongeza idadi ya watalii wa Kichina ili kujaza hoteli zake mpya za ufukwe na vituo vya skii vilivyojengwa hivi karibuni.

    Kim amekuwa akionesha kwa fahari silaha zake za nyuklia na makombora. Pia amekuwa akionesha mji mkuu Pyongyang kwa wageni wa heshima wanaotembelea nchi hiyo.

    Anataka dunia ijue kuwa mafanikio hayo yote yamepatikana bila kushinikizwa na Marekani au kuingia kwenye mazungumzo na Korea Kusini.

    Tangu Kim alipotangaza kusitisha juhudi za kuungana tena na Korea Kusini mnamo Desemba 2024, amewaita Wakorasia wa Kusini “adui wa kiapo” na amekata mawasiliano yote ya ngazi zote na Seoul.

    Juhudi za Seoul za kutafuta maridhiano zinaonekana kutokupokelewa vyema na Pyongyang.

    Unaweza kusoma;

  7. Takribani watu 50 wamekufa kwa kiu katika Jangwa la Sahara baada ya lori kuharibika

    Waathiriwa walizikwa katika makaburi ya pamoja na timu ya uokoaji iliyotumwa eneo hilo.

    Chanzo cha picha, Agadez governorate/Facebook

    Takribani watu 49 wamekufa kwa kiu katika eneo la mbali la Jangwa la Sahara kaskazini mwa Niger baada ya lori waliokuwa wakisafiria kuharibika, mamlaka zimesema.

    Kundi hilo lilikuwa likirejea kutoka Mali ambako walikuwa wamehudhuria sikukuu ya Kiislamu wakati walipoishiwa maji, wakibaki wamekwama zaidi ya kilomita 80 (maili 50) magharibi mwa Assamaka, kituo kikuu cha mpakani kati ya Niger na Algeria.

    “Wasafiri walijikuta wamenaswa katikati ya mazingira magumu sana ambapo joto kali na ukosefu wa vituo vya huduma hufanya uhai kuwa mgumu kupita kiasi,” ilisema taarifa ya Gavana wa Agadez.

    Watu wawili pekee ndio walinusurika, wakitembea zaidi ya kilomita 50 kuvuka jangwa hadi Assamaka, ambako walizitaarifu mamlaka.

    Lori hilo lilikuwa limeondoka katika mji wa Telhandek nchini Mali lakini likaacha njia, ilisema taarifa ya gavana huyo.

    Kwa siku kadhaa, dereva na abiria walijaribu mara kwa mara kulirekebisha gari hilo, lakini juhudi zao hatimaye hazikufanikiwa.

    “Wakiwa wamekosa maji na kushindwa kulirekebisha gari hilo licha ya juhudi za dereva, msaidizi wake na abiria, wasafiri walijikuta wamenaswa katikati ya mazingira magumu sana,” iliongeza taarifa hiyo.

    “Miili kadhaa ilipatikana chini ya lori lisilosogea na maeneo yaliyolizunguka.”

    Waathiriwa walizikwa katika makaburi ya pamoja na timu ya uokoaji iliyotumwa eneo hilo na mamlaka za eneo hilo.

  8. Mali watoa zawadi nono kwa atakayemkamata kiongozi wa kundi la al-Qaeda

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya kijeshi ya Mali inatoa dola milioni 3.5 kwa taarifa zitakazowezesha kukamatwa au kuuawa kwa Iyad Ag Ghaly. Serikali hiyo pia inatoa zawadi ndogo kwa washukiwa wengine, ikiwa ni pamoja na watu wanaotaka kujitenga kwa Tuareg.

    Kikosi tawala cha kijeshi nchini Mali kimetoa zawadi ya dola milioni 3.5 (kama euro milioni 3) kwa habari zitakazopelekea kukamatwa au kuuawa kwa Iyad Ag Ghaly, ambaye anaongoza tawi la Sahel la kundi la kigaidi la al-Qaeda lililoanzisha mashambulizi makubwa mnamo mwezi Aprili.

    Ghaly, chifu wa Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM), anasakwa na nchi kadhaa za eneo la Sahel barani Afrika, ambazo kadhaa zinatawaliwa kijeshi.

    Mwezi Aprili, JNIM iliungana na waasi wa Tuareg kuanzisha mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya serikali ya Mali katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja. Mashambulio mengine ya wakati huo huo yaliua watu kadhaa, akiwemo Waziri wa Ulinzi Sadio Camara.

    JNIM ndilo kundi kubwa zaidi la Kiislamu linalopigana na wanajeshi katika eneo la Sahel, ambapo makundi mengi ya Kiislamu yenye itikadi kali na wanaotaka kujitenga yanaendesha shughuli zake.

    Soma zaidi:

  9. Sudan, DR Congo ziko kwenye migogoro mikubwa zaidi duniani iliyopuuzwa - NRC

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ziko kwenye orodha ya migogoro ya wakimbizi iliyopuuzwa zaidi duniani, kundi la misaada la Wakimbizi la Norway limesema.

    Sudan, ambayo tangu 2023 imekumbwa na mzozo wa umwagaji damu kati ya majenerali wawili wapinzani wanaoshindania madaraka, ina zaidi ya watu milioni tisa waliokimbia makazi yao, taarifa ya shirika hilo ilisema.

    Shirika hilo liliongeza kuwa Wasudan wengine milioni nne wamekimbilia nchi jirani na karibu watu milioni 19.5, pia wanakabiliwa na njaa.

    "Ni jambo lisiloweza kufikirika kwamba mgogoro wa wakimbizi wa kiwango sawa na migogoro ya Syria na Ukraine katika kilele chake unaweza kuendelea kuwa mbaya zaidi bila kutambuliwa," mkuu wa NRC Jan Egeland alisema.

    Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako miongo ya vita na mlipuko wa Ebola umefanya hali kuwa mbaya zaidi.

    "Watu husahau kwamba kutakuwa na magonjwa ya mlipuko, harakati za uhamiaji, na upotezaji mkubwa wa maisha ya binadamu ikiwa hatuwekezi katika matumaini katika mabara mengine", Egeland amesema.

    Alisema kuwa Afrika iko upande wa Mediterania, wanakoenda likizo na ikiwa bara hilo litaathirila, pia nao watakabiliwa na madhara yake.

    Soma zaidi:

  10. Ethiopia: TPLF yahimiza hatua za kimataifa kuzuia vita vinavyokaribia

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Chama cha TPLF nchini Ethiopia, kimeonya kuwa taifa hilo linakabiliwa na hatari ya kuzuka kwa mzozo mkubwa na wenye madhara makubwa, huku kikitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kabla hali haijawa mbaya zaidi.

    TPLF imesema kupitia taarifa iliyotolewa jana Juni 4, wakati Ethiopia ikihitimisha uchaguzi wake mkuu wa 7, kuwa uchaguzi hauwezi kutatua mzozo wa kisiasa unaozidi kuongezeka nchini humo na kwamba changamoto za sasa za Ethiopia zinahitaji mazungumzo ya kitaifa yenye umoja na ya kuaminika yenye uwezo wa kushughulikia matatizo ya kimsingi ya kisiasa ya nchi hiyo.

    TPLF, ambayo hivi majuzi ilirejesha serikali ya eneo la kabla ya vita huko Tigray baada ya kuvunja utawala wa muda wa kikanda ulioanzishwa chini ya Mkataba wa Pretoria, imeishutumu serikali ya shirikisho kwa kuhujumu makubaliano hayo.

    Ukiwa umetiwa saini nchini Afrika Kusini mwaka 2022 ili kumaliza vita vya Tigray vilivyodumu kwa miaka miwili, mkataba huo "umeshindwa kwa kiasi kikubwa kufanya kazi," taarifa hiyo ilibainisha, na kuongeza kuwa hakuna masharti yake ya msingi ambayo yametekelezwa ipasavyo.

    Kulingana na TPLF, vikosi vya Ulinzi vya kitaifa vya Ethiopia vimeanzisha uhamasishaji mkubwa wa kijeshi kwenye mipaka ya Tigray, kuzunguka eneo hilo na kusababisha shida kubwa ya kijamii na kiuchumi na dhiki ya kisaikolojia miongoni mwa wakazi wake.

    Pamoja na mivutano hiyo, TPLF ilisisitiza dhamira yake ya kupata suluhisho kwa njia ya amani.

    Kundi hilo liliwahimiza wahusika wa kimataifa kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kuleta pande zote kwenye meza ya mazungumzo. "Hali hiyo inahitaji hatua za haraka, zilizoratibiwa na madhubuti ili kuanzisha mazungumzo ya kisiasa ya kuaminika kabla ya kuchelewa," taarifa hiyo ilionya.

    Iliongeza kuwa vita tayari vinaharibu maeneo ya Amhara na Oromia, na hatari ya makabiliano mapya yanayohusisha Tigray "inazidi kuongezeka."

  11. Wachunguzi Zanzibari wasema mwanamitindo wa Marekani Ashlee alijiua

    .

    Chanzo cha picha, social

    Polisi huko Zanzibar wamehitimisha kuwa mshawishi wa mitandao ya kijamii kutoka Marekani, Ashley Robinson, mwenye umri wa miaka 31, alifariki kwa kujiua kufuatia msongo wa mawazo, baada ya uchunguzi kuhusu kifo chake katika hoteli moja visiwani humo.

    Bi Robinson, ambaye pia alijulikana kama Ashlee Jenae, alifariki baada ya tukio lililotokea katika hoteli moja kisiwani huko tarehe 8 mwezi wa Aprili.

    Akitoa taarifa kuhusu matokeo ya uchunguzi huo Alhamisi, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Zuberi Chembera, alisema wachunguzi wamebaini bila shaka kwamba kifo cha Bi Robinson kilitokana na kujiua na kwamba hakuna mtu mwingine aliyehusika.

    "Kupitia maelezo ya mashahidi na uchunguzi wa vifaa vya mawasiliano vya marehemu na mchumba wake, tulibaini kuwa alikuwa na msongo wa mawazo. Ujumbe waliotumiana ulionyesha malalamiko ya mara kwa mara kuhusiana na hali ya maisha yake," Chembera aliwaambia waandishi wa habari mjini Zanzibar.

    Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuibuka kwa taarifa zinazokinzana kuhusu mazingira ya kifo chake.

    Katika matokeo yake ya awali, polisi walisema Robinson alijitoa uhai kufuatia kutofautiana na mchumba wake, Joseph McCann, 45. Hata hivyo, ripoti zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa huenda ndiye aliyemuua.

    Polisi baadaye walianzisha uchunguzi kamili na kuchukua pasipoti ya McCann na kumhoji kama sehemu ya taratibu za kawaida.

    Kulingana na wachunguzi, McCann na Bi Robinson waliingia katika jumba la kifahari la Zuri Hotel tarehe 6 Aprili na kutoelewana kulitokea kati ya wanandoa hao karibu saa sita mchana tarehe 8 Aprili, na kusababisha mzozo ambao haujatatuliwa.

    Wasimamizi wa hoteli waliarifiwa na kumhamisha McCann hadi Villa 65 huku juhudi zikiendelea kushughulikia hali hiyo.

    Polisi walisema alipatikana akiwa amejilingalinga kwenye chuma cha kutundika nguo kwa kutumia mkanda wa nguo unaotolewa kwa kawaida kwa wageni katika vyumba vya hoteli.

    Familia ya mshawishi na McCann hazijatoa maoni kuhusu matokeo ya polisi wa Zanzibar.

    Bi Robinson na McCann walikuwa wamesafiri hadi Tanzania kwa likizo na kusherehekea siku yake ya kuzaliwa tarehe 5 Aprili.

    Alimchumbia siku hiyo hiyo, siku nne kabla ya kifo chake.

    Mwili wa Bi Robinson baadaye ulirudishwa Marekani tarehe 24 Aprili, na ibada ya mazishi yake ilifanyika Mei 05 huko New Jersey.

    Soma zaidi:

  12. Chanjo ya 'kwanza duniani' iliyoundwa na Akili mnemba

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Akili mnemba imetumika kutengeneza aina ya chanjo "mpya" ambayo inaweza kuwa kinga dhidi ya idadi kubwa ya virusi na kuzuia magonjwa ya mlipuko, wasema watafiti.

    Timu katika Chuo Kikuu cha Cambridge inasema ni mara ya kwanza kwa sehemu muhimu ya chanjo kubuniwa kikamilifu na AI na kisha kujaribiwa kwa watu.

    Chanjo hiyo ilibuniwa ili kufanya kazi kwenye virusi vyote vya korona ambavyo vingejumuisha aina zote za Covid na virusi vinavyoambukiza wanyama, lakini pia vinaweza kuanzisha janga.

    Bado iko katika hatua za mwanzo, lakini timu tayari inatengeneza chanjo tofauti ambazo zinaweza kukabiliana na mafua na Ebola.

    Chanjo hufundisha miili yetu jinsi ya kugundua maambukizi ili kuongeza nafasi zetu za kupambana nayo.

    Lakini baadhi ya virusi vina ujuzi wa kubadilisha mwonekano wao - au kubadilika - kwa hivyo chanjo zinaweza kushindwa kufanyakazi haraka. Ndiyo maana chanjo za Covid na homa ya majira ya baridi zinahitaji kusasishwa mara kwa mara.

    "Siku zote tuko nyuma," alisema Profesa Jonathan Heeney, kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge, akiongeza kuwa "tunachojaribu kufanya ni kuwa mbele" na hadi sasa kuna uwezo wa kujikinga dhidi ya milipuko mipya au magonjwa ya mlipuko.

    Soma zaidi:

  13. Shule Kenya hazitafungwa mapema kwa likizo ya katikati ya muhula - Waziri

    .

    Chanzo cha picha, Shutterstock

    Katibu wa Wizara ya Elimu Kenya Prof. Julius Bitok ameondoa uwezekano wa shule kufungwa mapema kwa ajili ya mapumziko ya katikati ya muhula huku ghasia zikiendelea kushuhudiwa katika shule mbalimbali kote nchini.

    Waziri alisema wizara ya elimu imeingilia kati kwa ushirikiano na washikadau ili kujua tatizo liko wapi na kurejesha hali ya utulivu na kuongeza kuwa zaidi ya 90% zinaendelea na ratiba zao kama kawaida.

    Shule kadhaa zilizoathirika zimelazimika kufungwa kwa muda na kuongeza wasiwasi huku wanafunzi wa shule ya utumishi wanaoshukiwa kuchoma bweni na kusababisha vifo vya wenzao 16 wakiamriwa kuendelea kusalia rumande.

    Soma zaidi:

  14. Wananchi washambulia timu ya mazishi DRC, hofu ya Ebola kuenea yaongezeka

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka za afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), zimeeleza wasiwasi mkubwa baada ya wakazi wa eneo la Katana katika jimbo la Kivu Kusini kushambulia timu maalum ya mazishi ya waathirika wa Ebola.

    Tukio hilo lilitokea Jumatatu na kulazimisha wahudumu wa afya kuacha jeneza walilokuwa wakilisafirisha kutokana vurugu hizo.

    Kwa mujibu wa taarifa za wizara ya afya, mwili wa marehemu uliendelea kushughulikiwa na wananchi wa kawaida baada ya timu hiyo kuondoka. Hatua hiyo inatajwa kuwa hatari kubwa kwa sababu miili ya waathirika wa Ebola inaweza kuendelea kusambaza maambukizi ikiwa haitashughulikiwa kwa kufuata taratibu maalum za afya.

    Tukio hilo limeongeza changamoto katika juhudi za kudhibiti mlipuko wa aina ya Bundibugyo ya Ebola, huku kukiwa na taarifa za mashambulizi mengine dhidi ya wahudumu wa afya na timu za mazishi katika maeneo tofauti. Katika mji wa Bunia, jimbo la Ituri, watu kadhaa walijeruhiwa baada ya wakazi kushambulia timu ya wahudumu wa afya kwenye makaburi.

    Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa ukosefu wa imani kutoka kwa baadhi ya wananchi na upinzani dhidi ya hatua za kudhibiti ugonjwa huo vinaendelea kuathiri mapambano dhidi ya Ebola. Baadhi ya familia zimekuwa zikipinga taarifa rasmi za sababu za vifo vya ndugu zao, jambo linalochochea migogoro na wahudumu wa afya.

    Tangu mlipuko huu wa 17 wa Ebola nchini DRC kutangazwa Mei 15, jumla ya wagonjwa 363 wamethibitishwa kuambukizwa huku watu 62 wakifariki dunia. Maambukizi yameendelea kuongezeka katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, hali inayoongeza hofu ya kuenea zaidi kwa ugonjwa huo ikiwa hatua za kudhibiti maambukizi hazitaheshimiwa kikamilifu.

  15. Tetesi za soka: Diomande, Kroupi wazigonganisha Arsenal, PSG na Liverpool

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Arsenal wanakabiliwa na ushindani kutoka kwa Mabingwa wa Ulaya, Paris Saint-Germain, (PSG) katika harakati za kumsajili mshambuliaji Mfaransa Eli Junior Kroupi kutoka Bournemouth, pamoja na mshambuliaji wa Argentina Julian Alvarez anayechezea katika Atletico Madrid. (Independent)

    Liverpool inamtaka winga wa Ivory Coast, Yan Diomande, baada ya kuwasiliana na klabu ya RB Leipzig. Hata hivyo, klabu hiyo ya Ujerumani ina msimamo wa kutomuuza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19. (Athletic)

    PSG pia wanamfuatilia Diomande. Inadaiwa kuwa mchezaji huyo mwenyewe angependa zaidi kuhamia PSG kuliko sehemu nyingine yoyote. (Telefoot, via Mirror)

    Beki wa Chelsea, Marc Cucurella, anaangalia uwezekano wa kuondoka Stamford Bridge, huku Atletico Madrid ikijiandaa kutoa ofa yake ya kwanza kwa ajili ya nyota huyo wa Hispania. (Teamtalk)

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Brentford wamepeleka dau la £43m kwa ajili ya kumsajili winga wa Mjerumani Said El Mala kutoka FC Cologne. (Bild) Hata hivyo, El Mala hana nia ya kuhamia klabu hiyo ya Ligi Kuu England. (Sky Sports Germany)

    Juventus wanahitaji angalau £26m ili kumuachia beki wa pembeni wa Italia Andrea Cambiaso, ambaye anahusishwa pia na vilabu vya Chelsea na Barcelona. (Calciomercato)

    Mshambuliaji wa Serbia, Dusan Vlahovic ataondoka Juventus mwishoni mwa mwezi Juni baada ya kuamua kutosaini mkataba mpya na klabu hiyo ya Italia. (Football Italia)

    Juventus wameonyesha tena nia kumsajili mshambuliaji wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Ufaransa, Jean-Philippe Mateta. (Gazzetta dello Sport)

  16. Zelensky apendekeza mazungumzo ya ana kwa ana na Putin ili kumaliza vita vya Ukraine

    Z

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ametoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya ana kwa ana kati yake na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, katika juhudi mpya za kutafuta suluhisho la kumaliza vita vinavyoendelea kati ya nchi hizo mbili.

    Kupitia barua ya wazi aliyomwandikia Putin, Zelensky alisema kuwa ni muhimu viongozi hao wawili kukutana moja kwa moja ili kujadili njia za kurejesha amani.

    Katika barua hiyo yenye zaidi ya maneno 1,800, Zelensky alisisitiza kwamba amani ya kudumu inaweza kupatikana tu kupitia mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Ukraine na Urusi. Aliongeza kuwa haitakuwa sahihi kusubiri hadi Marekani irejee kuipa kipaumbele vita vya Ulaya baada ya kuelekeza nguvu zake kwenye migogoro mingine ya kimataifa, ikiwemo suala la Iran.

    Zelensky pia alipendekeza kusitishwa kwa mapigano kwa kipindi chote cha mazungumzo hayo ili kutoa mazingira mazuri ya kufikia makubaliano. Hata hivyo, Putin awali alikataa wazo la kusitisha mapigano kwa muda, akisisitiza kuwa bado kuna masuala muhimu yanayohitaji kujadiliwa kabla ya kufikiwa kwa makubaliano yoyote.

    Serikali ya Urusi imethibitisha kupokea barua hiyo na kusema kwamba rais wa Urusi atapewa taarifa kamili kuhusu yaliyomo kabla ya kutoa msimamo rasmi.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, pia alitoa maoni yake kuhusu pendekezo hilo, akisema kuwa itakuwa jambo jema ikiwa viongozi hao wawili watakutana uso kwa uso. Wakati huo huo, Zelensky alipendekeza kwamba mazungumzo hayo yaweze kufanyika katika nchi isiyoegemea upande wowote kama Switzerland au Turkey.

    Vita kati ya Urusi na Ukraine vilianza kwa uvamizi mkubwa wa Urusi mwezi Februari mwaka 2022 na vimesababisha maelfu ya vifo pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu. Licha ya majaribio kadhaa ya mazungumzo yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali, juhudi za kufikia usitishaji wa mapigano zimekuwa zikikwama. Pendekezo hili jipya la Zelensky linaonekana kuwa hatua nyingine muhimu katika kutafuta njia ya kumaliza mzozo huo wa muda mrefu.

  17. Karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo Juni 5, 2026