Kundi la JNIM lasema linataka kudhibiti mji wa Bamako, nchini Mali
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ikionyesha machafuko yaliyoshuhudia nchini Mali
Kundi la kigaidi la JNIM linalojihusisha na kundi na Al Qaeda nchini
Mali, limeeka kizuizi katika mji mkuu wa taifa hilo Bamako.
Kundi la JNIM lilisema kuwa hakuna mtu atakayeruhusiwa kuingia katika
mji huo baada ya kufunga barabara kuu zinazoingia mjini Bamako.
Rais wa mpito wa taifa hilo jenerali Assimi Goita amekutana na viongozi
wakuu wa usalama wa taifa hilo kujaribu kudhibiti hali huku kukiwa na hofu kuwa
serikali ya kijeshi ya taifa hilo huenda isiwe na nguvu ya kudhibiti makundi
yaliyojihami na makundi ya kigaidi ambayo sasa yanadhibiti maeneo kadhaa nchini
humo.
Urusi nayo imesisitiza kuwa wanajeshi wake watasalia nchini Mali
kuendelea kuisaidia taifa hilo kupambana na makundi ya kigaidi na yenye itikadi
kali.
Awali kundi la waasi la Tuareg lilikuwa limewataka wanajeshi wa Urusi
kuondoka nchini humo.
Vikosi vya usalama Uganda vyatuhumiwa kuwaua raia wasio na silaha - ripoti
Chanzo cha picha, EPA
Swahibu Ibrahim,
BBC Kampala
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limevishutumu vikosi vya usalama vya Uganda kwa kuwaua raia, kuwakamata kiholela na kuwatesa wafuasi wa upinzani katika kipindi cha kuelekea na baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 15 Januari nchini humo.
Katika taarifa iliyotolewa leo, shirika hilo limesema takriban watu 16 huenda waliuawa kati ya Januari 15 na Januari 18 na wanajeshi na polisi kwa kutumia nguvu zisizo halali.
Inasemekana kuwa waathiriwa hawakuwa na silaha na hawakuwa na tishio lolote.
BBC imewasiliana na mamlaka ya Uganda kupata maoni.
Dhuluma hizo zinazodaiwa kuwalenga wafuasi wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP), kinachoongozwa na Bw. Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu Bobi Wine ambaye sasa amejihami nchini Marekani.
Amnesty inasema ilinakili matukio 10 ya matumizi ya nguvu kukabili upinzani katika wilaya kadhaa, ikiwa ni pamoja na Butambala, Bulenga na Luwero katikati mwa Uganda.
Katika kisa kimoja, wanajeshi waliripotiwa kuvamia nyumba ya mwanasiasa wa upinzani usiku wa uchaguzi na kuwapiga risasi watu saba waliokusanyika hapo.
Mashahidi waliiambia shirika hilo kwamba hakuna hata mmoja wa waathiriwa aliyekuwa na silaha.
Ripoti za ukaguzi wa maiti zilizokaguliwa na Amnesty zilithibitisha kwamba watu kadhaa walifariki dunia kutokana na majeraha ya risasi.
Rais Ruto amzawadia mwanariadha wa Kenya Sabastian Sawe
Chanzo cha picha, IKULU
Rais wa Kenya William Ruto leo amemzawadia shujaa wa mbio za marathon Sebastian Sawe gari jipya alilochagua likiwa na nambari maalum zilizo na muda wake wa kuvunja rekodi wa mbio za marathon 1:59:30 pamoja na pesa taslimu takriban £45,000 (Shilingi milioni 8 za Kenya) kama utambulisho wa mafanikio yake ya kihistoria katika riadha.
Sawe mwenye umri wa miaka 30 aliyeandikisha historia katika mbio za Marathon ya London tarehe 26 April kwa kuandikisha muda wa saa 1.59.30, alituzwa shilingi milioni 8 za Kenya kwa ushindi huo na pia ametakiwa kuchaguwa gari la chaguo lake litakalonunuliwa na Rais Ruto.
Sawe alikabidhiwa nambari ya usajili wa gari iliyoandkiwa 1.59.30 akielezwa kuwa ni ishara ya gari lolote alitakalo atanunuliwa na Rais kama bahshishi
Mbali na fedha kutoka kwa Rais, Mwanariadha huyo pia alivuna shilingi milioni 7.1 kutoka kwa usimamizi wa London Marathon kwa kuvunja rekodi ya mbo hizo na isitoshe na marupuru ya shilingi milioni 42.3.
Inakadariwa akichanganya na fedha za malipo ya biashara kwa ushirikiano wake na kampuni ya michezo ya adidas, huenda Sawe akakusanya jumla ya shilingi milioni 129 za Kenya kwa ufanisi wake.
Rais Ruto alisifu nidhamu na azma ya Sawe, akielezea utendakazi wake kama wakati wa fahari ya kitaifa ambayo inaimarisha ubabe wa Kenya katika mbio za masafa marefu.
Kwa furaha na bashasha mwanariadha huyo aliyetekwa na hisia nyingi za furaha alikosa maneno ya kujieleza huku akiahidi kuwa atazidi kushamiri katika riadha hizo akilenga kuendelea kuipaisha bendera ya Kenya katika riadha za kimataifa.
‘'Asante sana Rais Ruto kwa ualishi huu,nashkuru kupata fursa hii ya kuiwakilisha Kenya,naahidi kuwa huu ni mwanzo nitajia juhudi nizidi kufanya vyema na kushinda dhahabu,'’alisema Sawe
Chanzo cha picha, IKULU
Kutokana na ufanisi huo,Rais William Ruto ameahidi kuwa serikali yake itawapa fedha maalum washindi wote wa riadha watakaowakilisha Kenya katika mashindano ya kimataifa.Alisema‘
Mshindi wa dhahabu tutampa shilingi milioni tatu, fedha milioni mbili na shaba milioni moja ili kwapa motisha wa talanta zao na pia kuwawezesha kimaendeleo ya maisha,’'alimaliza.
Waziri wa michezo nchini Kenya Salim Mvurya amesema Serikali itaboresha maslahi ya wanamichezo nchini kwa kuwekeza katika miundo mbinu sahihi ikiwemo viwanja.
Sebastian Sawe alianza kushiriki kwenye riadha za Maradhon mwaka 2024 tu akishinda marathon ya Valencia kwa muda wa saa 2.2.05.
Mashindano ya Marathon ya London ni marathon yake ya nne tu kushiriki na amefanikiwa kweka rekodi ya dunia .
Marekani bado haijalipa malimbikizo ya ada yake, asema mkuu wa WHO
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus
Marekani bado haijalipa malimbikizo ya ada yake ya uanachama katika Shirika la Afya Duniani, mkuu wa WHO alisema Jumatano, kwa nia ya Washington kuondoka kwa masharti ya kulipa.
Katibu mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema anatumai Marekani italipa ada inayodaiwa -- sharti lililojiwekea la kujiondoa katika shirika hilo.
Rais wa Marekani Donald Trump, aliporejea madarakani Januari 2025, alitoa notisi ya kuiondoa Marekani katika shirika hilo.
Marekani ilikuwa mfadhili mkubwa wa bajeti ya WHO.
'Sikutarajia': Mwanariadha wa Kenya Sabastian Sawe akaribishwa nyumbani kwa shangwe
Chanzo cha picha, EPA
Mwanariadha wa Kenya Sabastian Sawe amerejea nyumbani baada ya kuwa mwanamume wa kwanza kukimbia marathon chini ya saa mbili.
Mafanikio yake ya ajabu katika mbio za London Marathon siku ya Jumapili yamepokelewa kwa fvifijo na nderemo nchini Kenya, ambapo maafisa walimkaribisha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Wazazi wake pia walikuwepo kumpokea.
Sawe alimaliza mbio hizo chini ya saa mbili kwa muda wa 01:59:30.
Wazazi wa Sawe waliendesha gari kwa saa sita kutoka nyumbani kuja kumpokea mwana wao alipotua.
Ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways ambayo Sawe alisafiria kurejea nyumbani ilipokelewa kwa heshma maalum ilipotua, huku wacheza densi na wanamuziki wakitumbuiza.
Kurudi nyumbani kwa Sawe kulikuwa wakati wa fahari kubwa kwake binafsi, kwa familia yake, na pia kwa taifa la Kenya.
Trump atoa ramani ya Mlango-Bahari wa Hormuz, akiuita 'Mlango-Bahari wa Trump'
Chanzo cha picha, Truth Social
Rais Donald Trump amechapisha ramani ya Mlango-Bahari wa Hormuz kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii, Truth Social, baada ya kuuita jina la "Mlango Bahari wa Trump".
Trump amewahi kuetumia neno "Trump Strait" wakati wa hotuba, na kusema kwa mzaha kwamba vyombo vya habari vinaweza kufikiria kuwa ni "kosa la kukusudia," lakini kila mtu anajua sio sana mimi kukosea.
Taarifa zameibuka Marekani imetayarisha mpango wa wimbi la mashambulizi "mafupi na yenye nguvu" dhidi ya Iran katika hatua inayolenga kuvunja mkwamo katika mazungumzo na Tehran, tovuti ya habari ya Axios iliripoti.
Huku hayo yakijiri Spika wa Bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf amebeza vitisho vilivyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bisent dhidi ya Tehran.
Kuna uwezekano wa kizuizi cha Marekani dhidi ya bandari za Iran na usafirishaji wake kuendelezwa kwa miezi kadhaa.
Iran inavuruga usafiri kupitia Mlango Bahari wa Hormuz ambapo takriban thuluthu moja ya mafuta na gesi ya dunia hupita katika nyakati za kawaida.
Vizuizi hivyo vinaendelea kuwepo licha ya kusitishwa kwa mapigano kwa muda.
Ibada ya mazishi ya Ashlee Jenae kufanyika Jumanne nchini Marekani
Chanzo cha picha, Ashlee Jenae / Instagram
Na Alfred Lasteck,
BBC Dar es Salaam
Mwili wa mwanaharakati wa mtandaoni, Ashly Robinson, anayefahamika zaidi mtandaoni kama Ashlee Jenae, unatarajiwa kuagwa Jumatatu na Jumanne na kisha kufuatiwa na ibada ya mazishi itakayofanyika katika jimbo la New Jersey, nchini Marekani.
Ashlee alifika visiwani Zanzibar akisherehekea siku yake ya kuzaliwa Aprili 05, ambapo pia mchumba wake, Joseph McCann alimposa wakati wa safari hiyo.
Moja ya wanafamilia wa karibu ameiambia BBC kuwa maandalizi ya mazishi yaaendelea na kwamba jamaa, marafiki na mashabiki wa Ashlee watapata fursa ya kushiriki katika zoezi la kuaga mwili pamoja na kuwa katika ibada ya mazishi.
“Mipango ya mazishi tayari imetangazwa,” alisema mwanafamilia huyo.
Mwanzoni mwa juma, ripoti za baadhi ya vyombo vya habari zilieleza kuwa mwili wa Ashlee Jenae ulirejeshwa kutoka Tanzania na kukabidhiwa kwa familia yake Ijumaa iliyopita.
Mamlaka za Zanzibar hazijathibitisha kurejeshwa kwa mwili huo nchini Marekani.
Hata hivyo alipotafutwa na BBC, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Zuberi Chembera, alieleza kuwa kwa muda huo wasingeweza kutoa taarifa zozote zinazohusiana na kinachoendelea.
“Hatuwezi kutoa maoni kwa sasa. Tutatoa taarifa tutakapokuwa tayari,” alisema.
Hapo awali, Polisi visiwani humo waliiambia BBC kuwa kifo cha Ashlee kilitokea baada ya jaribio la kutaka kujiua.
Mpaka sasa bado haijafahamika iwapo mpenzi wake, Joseph McCann, bado yupo Zanzibar.
McCann pia hajatoa kauli yoyote ya hadharani kuhusu chochote kinahusiana na kifo cha Ashlee.
Aprili 14, polisi kisiwani humo walisema pasipoti ya McCann ilizuiliwa na kwamba alikuwa akihojiwa.
Aprili 28, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani haikuweza kuthiithibitishia BBC iwapo mwili huo ulirejeshwa nchini Marekani, wala haikutoa maelezo kuhusu McCann au hata uchunguzi unaoendelea.
“Maswali kuhusu uchunguzi wowote, fuatilieni kwenye mamlaka husika (Zanzibar),” Wizara hiyo iliieleza BBC kupitia ujumbe wa barua pepe.
Siku chache kabla ya kifo chake, mwanaharakati huyo aliweka picha mnato na picha mjengeo za safari yake, ikiwemo moja iliyopigwa katika jumba moja la kuhifadhi wanyama pori lililopo mkoani Kilimanjaro, Kaskazini mwa Tanzania.
Mafuta yanapanda bei ya juu zaidi tangu 2022
Chanzo cha picha, Costfoto/NurPhoto via Getty Images
Bei ya
mafuta inaendelea kupanda kwa kasi ikifikia kiwango cha juu zaidi tangu vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran
vilipoanza mwishoni mwa Februari mwaka huu.
Hii ni baada ya ripoti kuibuka kuwa jeshi la Marekani linatarajiwa kumuarifu Rais Donald Trump kuhusu mipango mipya ya kuchukua hatua katika vita vya Iran.
Kamandi Kuu ya Marekani imetayarisha mpango wa wimbi la mashambulizi "mafupi ya nguvu" dhidi ya Iran katika hatua inayolenga kuvunja mkwamo katika mazungumzo na Tehran, tovuti ya habari ya Axios iliripoti.
BBC imewasiliana na Kamandi Kuu ya Marekani na Ikulu ya White House kupata maoni.
Bei ya mafuta ghafi ilivuka kwa muda hadi dola za marekani 120 kwa pipa huku kukiwa na wasiwasi kuhusu muda ambao mzozo huo utaendelea
Hali
hii pia inakuja baada ya taarifa kuibuka kwamba Rais wa Marekani Donald Trump
alijadiliana na kundi la wakuu wa kampuni za nishati Jumanne kuhusu uwezekano
wa kuendeleza kwa miezi kadhaa kizuizi cha Marekani dhidi ya bandari za Iran na
usafirishaji wake.
Iran
inavuruga usafiri kupitia Mlango Bahari wa Hormuz ambapo takriban thuluthu moja
ya mafuta na gesi ya dunia hupita katika nyakati za kawaida.
Vizuizi
hivyo vinaendelea kuwepo licha ya kusitishwa kwa mapigano kwa muda.
Arsenal na Atletico zatoka sare ligi ya mabingwa Ulaya
Chanzo cha picha, Getty Images
Arsenal na Atletico Madrid walifunga penalti kila
mmoja katika sare ya mkondo wa kwanza iliyojaa matukio ambayo yalisawazisha
nusu fainali yao ya Ligi ya Mabingwa.
Viktor Gyokeres alishinda na kufunga mkwaju wa
penalti kwa wageni dakika moja tu kabla ya kipindi cha mapumziko baada ya
kuangushwa katika eneo hatari na beki David Hancko.
Lakini Julian Alvarez alisawazisha bao hilo dakika
11 baada ya kipindi cha pili baada ya Ben white kuunawa mpira katika eneo la
ulinzi wa Arsenal
Mchezaji wa akiba Eberechi Eze alifikiria
kujishindia penalti alipokanyagwa na beki wa wa Atletico Madrid Hancko ndani ya
eneo hatari lakini uamuzi huo
ulibatilishwa baada ya ukaguzi wa VAR.
Mchezo huo ulianza kwa kishindo huku kukiwa hakuna
upande wowote unaotaka kuona lango la mwenzake
Lakini baada ya Gyokeres kuweka The Gunners mbele,
Atletico Madrid walianza kipindi cha pili kwa kuzidisha presha.
Ademola Lookman alimlazimisha David Raya kuokoa
kabla ya Gabriel Magalhaes kuokoa shambulio laAntoine Griezmann huku wenyeji wakitafuta bao la kusawazisha.
Atletico walipata penalti wakati mkwaju wa Marcos
Llorente kutoka pembeni mwa eneo la goli ulipogonga mguu wa Ben White na kugusa
mkono wake.
Habari za hivi punde, 'Milipuko kadhaa' yaripotiwa kisikika Tehran
Vahid Online, Jukwaa maarufu la habari za kidijitali linaloendeshwa na mwanaharakati wa Iran na mwanablogu Vahid, muda mfupi uliopita limechapisha jumbe kadhaa zinazoripoti milipuko ya kusikia mjini Tehran.
Walioshuhudia tukio hiloi wameiambia mtandao huo wa habari kwamba milipuko hiyo ilisikika katika sehemu ya mashariki ya mji mkuu, katika wilaya za Tehran-Pars na Hakimiyah.
Baadhi ya watu walieleza milipuko hiyo kama "shughuli za kupambana na ndege za kivita."
BBC haijafanikiwa kuthibitisha usahihi wa ripoti hizo.
Katika siku chache zilizopita, maafisa wa serikali za mitaa na wa kikanda nchini Iran wameripoti kufanya shughuli za kuharibu vilipuzi ambavyo havijalipuka vilivyosalia baada ya mapigano, lakini watu wanafananisha milipuko ya Alhamisi asubuhi katika eneo la mashariki mwa Tehran na sauti ya mashambulizi ya ndege za kivita.
Shambulio dhidi ya wanaume wawili wa Kiyahudi mjini London ni ugaidi- Polisi
Chanzo cha picha, UGC
Wanaume wawili Wayahudi wamechomwa visu katika eneo la Golders Green, kaskazini mwa London, katika tukio lililotangazwa na polisi kuwa la kigaidi.
Wanaume hao wawili, waliotajwa kama Shilome Rand na Moshe Shine, walipatiwa matibabu katika eneo la tukio na sasa wako katika hali thabiti hospitalini, kulingana na Polisi.
Polisi wamesema mwanaume mwenye umri wa miaka arobaini na mitano, raia wa Uingereza aliyezaliwa Somalia, alipigwa kwa bunduki ya umeme yaani Taser na polisi kabla ya kukamatwa kwa tuhuma za jaribio la mauaji. Mshukiwa huyo kwa sasa yuko rumande.
Waziri Mkuu Keir Starmer amesema shambulio hilo la chuki dhidi ya Wayahudi ni la kusikitisha sana, akiongeza kuwa “Mashambulizi dhidi ya jamii yetu ya Kiyahudi ni mashambulizi dhidi ya Uingereza.”
Polisi wamesema maafisa wao waliitikia tukio hilo Jumatano baada ya kupokea taarifa kuwa watu walikuwa wamechomwa visu.
Mshukiwa huyo pia alijaribu kuwachoma visu maafisa waliokuwa wamefika eneo la tukio, lakini hakuna aliyejeruhiwa.
Polisi walitoa picha za tukio hilo kutoka kamera zilizovaliwa na maafisa, ambapo wanasikika wakimwamrisha mshukiwa mara kadhaa alale chini kabla ya kumshambulia kwa Taser, na kisha kumuamuru aachie kisu.
Imeelezwa kuwa mshukiwa huyo alikuwa na historia ya vurugu kubwa na matatizo ya afya ya akili.
Wachunguzi wanaamini mshukiwa huyo huyo alihusika katika tukio jingine la awali katika eneo hilo.
Mkuu wa Polisi wa Kupambana na Ugaidi nchini Uingereza, Laurence Taylor, baadaye alitangaza rasmi tukio hilo kuwa la kigaidi.
Rabbi Mkuu Ephraim Mirvis, ambaye anawakilisha jamii kubwa zaidi ya Wayahudi nchini Uingereza, amesema tukio hilo “linathibitisha kuwa ukiwa Myahudi unaoonekana wazi, hauko salama na hatua zaidi zinahitajika.”
Shambulio hilo linakuja chini ya wiki moja baada ya jaribio la uchomaji moto dhidi ya ukuta wa kumbukumbu eneo la Golders Green, na zaidi ya mwezi mmoja tangu magari ya wagonjwa yanayoendeshwa na shirika la matibabu la Kiyahudi Hatzola kuchomwa moto.
Comey ajisalimisha kufuatia madai ya kumtishia Trump maisha katika chapisho la Instagram
Chanzo cha picha, Getty Images
Mkurugenzi wa zamani wa shirika la upelelezi la Marekani, FBI, James Comey, amejisalimisha kwa mamlaka ili kukabiliana na mashtaka yanayodai kuwa picha aliyosambaza kwa muda mfupi kwenye mitandao ya kijamii ilikuwa tishio kwa maisha ya Rais wa Marekani Donald Trump.
Kesi hiyo inatokana na chapisho la mwaka 2025 kwenye Instagram lililowekwa na Comey, lililokuwa na picha ya magamba ya baharini yaliyopangwa kuunda maneno “86 47”. ni istilahi ya mtaani inayomaanisha “kuondoa”, na waendesha mashtaka wanadai kuwa inahamasisha vurugu dhidi ya Trump, rais wa 47.
Comey alikanusha mashtaka akisema hakujua maana ya namba hizo, na ameshutumu upande wa mashtaka kwa kuwa na nia za kisiasa.
Hii ni mara ya pili kwa Wizara ya Sheria kumfungulia mashtaka ya jinai Comey, ambaye ni mkosoaji wa muda mrefu wa Trump.
Comey hakuweka ombi la kujitetea wala kuzungumza wakati alipofikishwa mahakamani kwa muda mfupi katika jimbo la Virginia.
Wakili wake, Patrick Fitzgerald, alisema mkurugenzi huyo wa zamani atataka kesi ifutwe kwa misingi ya mashtaka ya kuchagua na yenye nia ya kulipiza kisasi — akidai alilengwa kwa sababu ya kuzungumza dhidi ya Trump.
Jaji Fitzpatrick alikataa juhudi za Wizara ya Sheria kuweka masharti ya kuachiliwa kwa Comey, akisema hayakuwa ya lazima, kwa mujibu wa CBS News.
Waendesha mashtaka wamemshtaki Comey kwa kujua na kwa makusudi kutoa tishio la kuondoa maisha ya — na kusababisha madhara ya kimwili kwa — rais, na pia kusambaza tishio hilo kati ya majimbo.
Kila shtaka lina adhabu ya juu ya hadi miaka 10 jela.
Katika taarifa ya video Jumanne, Comey alisema ana nia ya kupambana na mashtaka hayo.
Chapisho lake la awali la Mei 2025 lilikuwa na picha ya magamba ya baharini ufukweni yaliyopangwa kuonyesha “86 47”, likiwa na maelezo: “Mpangilio mzuri wa magamba ya baharini wakati wa matembezi yangu ufukweni.”
Comey alifuta picha hiyo baada ya malalamiko ya umma.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mashtaka dhidi ya Comey Jumatano, Trump alimuita “mtu fisadi”.
“Niseme yeyote anayejua kuhusu uhalifu, anajua 86. Ni istilahi ya magenge ya uhalifu inayomaanisha muue. Magenge hutumia neno hilo wanapotaka kumuua mtu, wanasema ‘86 huyo’.
Watu kama Comey ni tishio kubwa sana, nadhani, kwa wanasiasa na wengine,”
Baadhi ya wataalamu wa sheria — pamoja na wabunge — wamehoji uzito wa mashtaka hayo.
Comey alifutwa kazi na Trump katika muhula wake wa kwanza baada ya kuanzisha uchunguzi kuhusu uingiliaji wa Urusi katika uchaguzi wa urais wa Marekani wa 2016.
Tangu wakati huo, Trump amekuwa akitaka mara kwa mara kufunguliwa mashtaka dhidi yake — na mashtaka ya sasa ni jaribio la pili la utawala kufanya hivyo.