Kila Mmarekani atapata dola 5,000 Republican ikishinda uchaguzi wa katikati ya muhula - Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amesema atampa kila Mmarekani mtu mzima dola 5,000 iwapo chama cha Republican kitashinda mihula yote miwili ya Congress katika uchaguzi wa katikati ya muhula utakaofanyika Novemba — mpango ambao unaweza kugharimu zaidi ya dola trilioni moja.
Ahadi hiyo ilitolewa katika hotuba yake kwenye mkutano wa kwanza kabisa wa chama hicho kufanyika katikati ya muhula wa urais nchini Marekani.
Trump hakutoa maelezo kuhusu mpango huo utakavyotekelezwa au utakavyofadhiliwa, akisema tu kuwa fedha hizo zitatakiwa kutumika nchini Marekani. Makamu wa Rais JD Vance ameihusisha mipango hiyo na mapato ambayo serikali ya Marekani imekusanya kupitia ushuru wa bidhaa unaotozwa na Trump.
Mpango huo umezua utata. Wademokrasia wameuita “ahadi tupu”, huku wengine wakihoji iwapo ahadi kama hiyo inaruhusiwa kisheria.
Huenda hii ikawa mara ya kwanza kwa rais wa Marekani kutoa ahadi ya malipo ya aina hiyo kwa Wamarekani, katika mazingira ya mwaka wa uchaguzi ambapo anawahimiza wananchi kujitokeza na kupiga kura.
Iwapo mpango huo unawezekana au la, haikuonekana kuwa jambo la msingi kwa wakati huo. Wazo hilo lilipokelewa kwa makofi na shangwe kubwa kwenye mkutano huo, huku Trump akionekana kufurahia mwitikio huo.
Kuna karibu Wamarekani watu wazima milioni 270, hivyo malipo ya dola 5,000 kwa kila mtu yangegharimu serikali ya Marekani takriban dola trilioni 1.3.
Maswali yameanza kuibuka kuhusu uwezekano wa kutekelezwa kwa mpango huo, hasa wakati bei za bidhaa nchini Marekani zikiendelea kupanda, kwa kiasi fulani kutokana na vita ya Marekani na Israel dhidi ya Iran ilioanza mwezi Februari.
Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran yamejumuisha kushambulia kambi za kijeshi za Marekani na washirika wake katika Ghuba. Hata hivyo, jambo muhimu zaidi ni kwamba Iran kwa kiasi kikubwa imefunga Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao hupitisha takriban theluthi moja ya biashara ya mafuta duniani pamoja na sehemu kubwa ya gesi asilia iliyoyeyushwa.
Kufungwa kwa njia hiyo kumesababisha mabadiliko makubwa ya bei ya mafuta duniani, huku Trump akikabiliwa na shinikizo kutoka ndani ya chama chake kumaliza vita hivyo.
Jumatano, rais huyo wa Marekani aliwaonya wafuasi wake kwamba vita hivyo havitamalizika hadi baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula, na kwamba bei ya mafuta haitashuka hadi wakati huo.
Alitoa kauli hiyo kabla ya hotuba yake huko Texas, na kuirudia katika mkutano wa chama chake, ambapo alisisitiza kuwa maumivu ya kiuchumi ya muda mfupi yanafaa kuvumiliwa ili kuzuia Tehran kutengeneza silaha za nyuklia.
Unaweza kusoma;








