Moja kwa moja, Maziko ya Mfalme Oyo wa Tooro Uganda yaanza huku mzozo wa urithi ukiendelea
Ibada ya Mazishi ya Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi wa Nne, aliyewahi kuwa mtawala mwenye umri mdogo zaidi duniani, yafanyika katika kanisa kuu la dayosisi ya St.John Cathedral Uganda, Mfalme Oyo atazikwa leo katika makaburi ya kifalme ya Ufalme wa Tooro, magharibi mwa Uganda.
Maziko ya Mfalme Oyo:Hotuba ya Binti Mfalme Ruth Nsemere Komuntale katika sherehe ya maziko ya mfalme wa Tooro Uganda
Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati akitoa hotuba yake ya mwisho ya kumuaga mdogo wake, Binti Mfalme Ruth Nsemere Komuntale alielezea miezi ya mwisho kabla ya kifo cha Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi III.
Alielezea kwa ufupi wakati ambapo saratani ya Mfalme Oyo iligunduliwa. Saratani ya mdogo wake ilianza kujitokeza katikati ya mwezi Oktoba 2025, alipogunduliwa kuwa na saratani ya aina ya *Angiosarcoma* aina adimu na kali sana ya saratani inayotokea kwenye utando wa mishipa ya damu na mishipa ya limfu.
Alisema kuwa Mfalme alitumia zaidi ya mwaka mmoja kutafuta matibabu kwa ajili ya baadhi ya dalili alizokuwa nazo akiwa nchini Uganda, lakini saratani yake haikugunduliwa mapema vya kutosha.
Wakati akipata matibabu baadaye nchini Marekani, Mfalme aliomba hali yake iwekwe siri ili kuepuka kuzua hofu ndani ya ufalme.
Katika kuhitimisha hotuba yake, Binti Mfalme aliwataka watu wote kuwa makini na miili yao na kujijali wenyewe pia.
Mkutano wa Delhi kuamua mustakabali wa muungano wa BRICS
Chanzo cha picha, Getty Images
Viongozi wa dunia, akiwemo Rais wa Urusi Vladimir Putin, Rais wa China Xi Jinping, na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, wamekusanyika Delhi kwa ajili ya mkutano wa kilele wa BRICS.
Kundi hilo liliundwa kwa lengo la kuwa na nguvu ya usawa dhidi ya Marekani na Ulaya Magharibi, lakini vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati vimeibua nyufa ndani yake.
Mkutano huo ni fursa kwa BRICS kudhihirisha nafasi yake kama nguvu ya kisiasa na kiuchumi inayoweza kukabiliana na Magharibi, lakini pia ni jaribio kubwa kwa umoja wake.
Migogoro ya kimataifa imefichua migawanyiko mikubwa, kwa mfano, Falme za Kiarabu zimekuwa zikilengwa na mashambulizi kadhaa ya ndege zisizo na rubani na makombora kutoka Iran mwaka huu.
Mikutano ya BRICS katika kipindi cha miezi sita iliyopita haijazaa taarifa ya pamoja, jambo linalodaiwa kusababishwa na kutokubaliana sana kuhusu Iran na namna ya kushughulikia mizozo inayohusiana na Israel.
Suala jingine ni Donald Trump, vitisho vyake vya ushuru wa biashara vinafanya iwe muhimu zaidi kwa wanachama wa BRICS kuungana ili kuleta uwiano, lakini wakati huo huo, kukabiliana naye kunaweza kuwa na gharama kubwa.
Ikulu ya Marekani imeelezea baadhi ya mapendekezo ya BRICS kama yenye msimamo wa "kupinga Marekani," na nchi nyingi zitakuwa na tahadhari dhidi ya kumkasirisha rais huyo wa Marekani.
Katika Picha: Ibada ya maziko ya Mfalme Oyo Nyimba katika kanisa la St John's Cathedral
Ibada ya mazishi ya kumuaga Mfalme Oyo Nyimba yaanza rasmi katika kanisa la St. John's Cathedral nchini Uganda.
Familia, jamaa na marafiki wamehudhuria katika ibada hiyo huku shughuli za misa zikianza rasmi.
Maelezo ya picha, Mwili wa Mfalme Oyo ukipokelewa katika kanisa ambalo ibada ya wafu itafanyika.
Maelfu ya waombolezaji walijipanga kando ya barabara wakati mwili wa Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi wa Nne, Omukama wa Tooro, ukisafirishwa katika safari yake ya mwisho kuelekea Ikulu ya Karuziika.
Sherehe za kimila ziliambatana na kila hatua ya msafara huo, kwa heshima ya utawala wake wa takriban miaka 31.
Saudi Arabia yasitisha kwa tahadhari shughuli za bomba la mafuta la Mashariki-Magharibi
Chanzo cha picha, Copernicus Sentinel-3/Reuters
Bomba la mafuta la Mashariki-Magharibi la Saudi Arabia, ambalo limekuwa likilengwa na mashambulizi ya droni kutoka Iraq, limezidi kuwa muhimu tangu kuzuka kwa vita Mashariki ya Kati kati ya Marekani na Israel upande mmoja na Iran upande mwingine.
Bomba hilo la Petroline linaanzia katika maeneo ya mafuta ya Abqaiq, katika Mkoa wa Mashariki wa Saudi Arabia, hadi bandari ya Yanbu, magharibi mwa nchi hiyo. Lina urefu wa takriban kilomita 1,200 na ni njia kuu mbadala ya kusafirisha mafuta ya Saudi Arabia kwenda katika masoko ya dunia, bila kupitia Mlango wa Hormuz.
Kwa mujibu wa kampuni za usafirishaji na wachambuzi, katika miezi michache iliyopita bomba hilo limekuwa likisafirisha mapipa milioni nne hadi tano ya mafuta kwa siku, sawa na asilimia nne hadi tano ya usambazaji wa mafuta duniani.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi Arabia (SPA), mabomba hayo yana uwezo wa kusafirisha takriban mapipa milioni saba ya mafuta kwa siku.
Saudi Arabia imetangaza mara kadhaa katika miezi ya hivi karibuni kuwa maeneo yake, hususan miundombinu ya nishati, yamelengwa katika mashambulizi ambayo inasema yalifanywa na makundi nchini Iraq yenye uhusiano na Tehran.
Tetesi za soka Ulaya: Richarlison bado anaweza kuondoka Spurs
Chanzo cha picha, Getty Images
Klabu
kadhaa bado zinamuwania mshambuliaji wa Brazil, Richarlison, mwenye umri wa
miaka 29, baada ya mpango wake wa kuondoka Tottenham na kujiunga na Vasco da
Gama kuvunjika. (UOL - in
Portuguese)
Philippe
Coutinho, aliyewahi kuichezea Brazil, amekubali kutumia miezi mitatu katika
klabu ya Santos. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34, aliyewahi kucheza
Liverpool na Aston Villa, anatafakari iwapo ataendelea na soka baada ya kuwa
mchezaji huru tangu Februari, alipoondoka Vasco da Gama. (Globo - in
Portuguese)
Manchester
United inamfuatilia kwa karibu beki wa kushoto wa Bournemouth na timu ya taifa
ya Ufaransa, Adrien Truffert, mwenye umri wa miaka 24, ambaye thamani yake
inakadiriwa kuwa pauni milioni 60.(Teamtalk)
Liverpool
bado inamtaka kiungo wa Inter Milan, Aleksandar Stankovic, mwenye umri wa miaka
21, baada ya kuulizia uwezekano wa kumsajili katika dirisha la usajili la
majira ya joto. (Teamtalk)
Crystal
Palace bado haijakata tamaa ya kumsajili beki wa kati wa Brest, Raphael Le
Guen, mwenye umri wa miaka 20, ambaye ilijaribu kumsajili katika dirisha la
usajili lililopita. (Ouest-France
via SportWitness)
Liverpool
bado inamuwania winga wa Ufaransa, Michael Olise, mwenye umri wa miaka 24,
lakini Bayern Munich haina mpango wa kumuuza katika dirisha la usajili la
Januari. (Christian Falk)
Lamine
Camara sasa ameelekeza nguvu zake katika klabu ya Monaco baada ya mpango wa
siku ya mwisho wa usajili wa kiungo huyo wa Senegal, mwenye umri wa miaka 22,
kujiunga na Chelsea kuvunjika. Camara amesema, “Labda fursa nyingine
zitajitokeza.” (ESPN)
Jadon
Sancho hatarajiwi kujiunga na klabu mpya hivi karibuni, huku winga huyo wa
zamani wa England, mwenye umri wa miaka 26, akiendelea kutathmini chaguo zake
baada ya kuondoka Manchester United mwezi Juni. (Football
Insider)
Lazio
na Parma zimejiunga na Everton katika kuonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji
wa zamani wa Argentina, Mauro Icardi, mwenye umri wa miaka 33, ambaye ni
mchezaji huru baada ya kuondoka Galatasaray mwishoni mwa msimu uliopita. (Corriere
dello Sport - in Italian)
Malaga inazingatia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa
zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Ufaransa, Anthony Martial,
mwenye umri wa miaka 30, ambaye ni mchezaji huru baada ya kuondoka klabu ya
Monterrey ya Mexico mwezi Juni. (Mundo Deportivo - in Spanish)
Maziko ya Mfalme Oyo wa Tooro Uganda yaanza huku mzozo wa urithi ukiendelea
Chanzo cha picha, Reuters
Mwili wa marehemu Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi wa Nne, aliyefariki dunia mwezi uliopita akiwa na umri wa miaka 34, umesafirishwa kutoka Ikulu ya Karuzika hadi Kanisa Kuu la dayosisi ya St. John mjini Fort Portal.
Maelfu ya waombolezaji,baadhi wakiwa wamevalia kanzu nyeupe na mavazi ya gome la mti, pamoja na viongozi wa taasisi za kitamaduni na watu mashuhuri wengine,wamekusanyika katika ikulu hiyo na kanisa kuu kuhudhuria shughuli ya kumuaga mfalme huyo kwa mara ya mwisho.
Mfalme Oyo alifariki dunia nchini Marekani mwezi uliopita, ambako alikuwa akipatiwa matibabu ya saratani.
Baadaye atazikwa leo Jumamosi katika eneo la makaburi ya kifalme huko Karambi.
Hujambo na Karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja.