Nyota mchezaji wa zamani wa Marekani arejeshwa Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images
Mchezaji wa zamani wa raga wa Kenya na beki wa zamani wa ligi ya mpira wa miguu ya Marekani (NFL), Daniel Adongo, amerejeshwa nchini Kenya na Idara ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha ya Marekani (ICE) baada ya mamlaka za uhamiaji za Marekani kusema kuwa alizidisha muda wa kukaa nchini humo baada ya visa yake kuisha.
Adongo ambaye pia aliweka historia alipohamia kwenye soka la Marekani na kuchezea Indianapolis Colts.
Kwa mujibu wa ICE na taarifa za vyombo vya habari vya Marekani, Adongo, mwenye umri wa miaka 37, alifurushwa Marekani tarehe 20 Juni baada ya jaji wa uhamiaji kutoa amri ya kuondolewa nchini humo mnamo mwezi Machi.
Mamlaka zilisema uamuzi huo ulitokana na kubainika kuwa alikuwa ameendelea kubaki nchini Marekani baada ya muda wa visa yake kuisha mwaka 2016.
ICE ilisema kuondolewa kwa Adongo pia kulitokana na rekodi yake ya makosa ya uhalifu nchini Marekani, ikiwemo hukumu ya mwaka 2020 kwa kosa la uhalifu.
Idara hiyo ilisema Adongo alikuwa amewahi kukamatwa awali kwa tuhuma zilizojumuisha vitisho vya uhalifu, shambulio na tabia ya kuvuruga amani.
Hata hivyo, ICE haikuonyesha katika taarifa yake ikiwa visa hivyo vilipelekea kupatikana kwa hukumu nyingine za hatia.


























