Je, chai, kahawa au maji ya moto vinaongeza hatari ya saratani?

    • Author, Michelle Roberts
    • Nafasi, Digital health editor
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kunywa vinywaji kama chai na kahawa mara kwa mara kwenye halijoto kali sana huongeza hatari ya saratani ya bomba la chakula au korodani, inayojulikana kama saratani ya umio, kwa mujibu wa utafiti wa Uingereza.

Watafiti wanasema matokeo hayo, kutoka kwa utafiti wa takriban watu milioni moja, yanafanya hili kuwa jambo kubwa zaidi hadi sasa, katika kubaini uhusiano huo.

Katika utafiti huo, watu waliokunywa vinywaji vyao "vya moto sana" walikuwa na hatari ya kupata saratani mara tatu zaidi kuliko wale wanaokunywa chai au kahawa ambayo sio moto sana au vuguvugu, ingawa wataalamu wanasisitiza kwamba nafasi za jumla za kupata saratani hii ni ndogo.

Kinywaji cha moto kwa mvuke kinaweza kuharibu utando wa seli wa bomba la chakula kuelekea tumboni.

Vinywaji vya moto vinavyochoma

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Oxford na kuchapishwa katika jarida la *International Journal of Cancer*, unafafanua kinywaji chochote chenye joto la nyuzi joto 65 au zaidi kuwa ni "cha moto sana" na chenye uwezekano wa kuleta hatari.

Kunywa vinywaji vya moto mara sita au zaidi kwa siku pia huongeza hatari hiyo, kulingana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wanaume na wanawake 977,282 wa umri wa kati.

Ingawa kuongeza maziwa kunaweza kupunguza joto la vinywaji kidogo, chai au kahawa yenye maziwa bado inaweza kuwa na joto kali mno, watafiti wanasema.

Chai inayotayarishwa mara tu maji yanapochemka kikamilifu huwa na joto linalokaribia kiwango cha kuchemka, yaani nyuzi joto 100. Inapomiminwa kwenye kikombe, joto hilo hupungua hadi kufikia takriban nyuzi joto 90 au 95.

Ushauri uliotolewa ni kusubiri kwa dakika chache kabla ya kunywa ili kinywaji hicho kipoe na kufikia kiwango cha joto salama zaidi.

Shirika la Cancer Research UK linasema ni vigumu kubainisha muda kamili ambao kinywaji cha moto kinapaswa kuachwa ili kipoe.

"Lakini ikiwa una wasiwasi, tunashauri usubiri hadi kiwe katika hali nzuri ya kunyweka badala ya kukinywa kikiwa bado cha moto sana," shirika hilo lilisema.

Mtafiti mkuu Dkt. Keren Papier alisema utafiti uliofanywa Amerika Kusini,ambako watu wengi hunywa kinywaji cha mitishamba cha moto sana kiitwacho *mate*tayari umeonyesha uhusiano kama huo kati ya vinywaji vya moto na saratani ya umio.

Hata hivyo, alisema, "Utafiti zaidi unahitajika sasa ili kubaini viwango kamili vya joto la vinywaji vinavyohusishwa na hatari hii iliyoongezeka."

Utafiti mwingine uliohusisha vijana 118 waliojaribu aina mbalimbali za kahawa nyeusi uligundua kuwa wengi wao waliona vinywaji hivyo kuwa vya moto kupita kiasi pale tu joto lake lilipofikia nyuzi joto 70 au zaidi.

Kulingana na mtengenezaji mmoja wa vikombe vya kahawa , kiwango bora cha joto kwa kahawa ya moto wakati wa safari ni kati ya nyuzi joto 49 na 60.

Iwapo mtengenezaji wa kahawa anataka kahawa hiyo ibaki na joto kwa muda mrefu zaidi,kama mteja akiomba iwe ya moto zaidi inaweza kutolewa ikiwa na joto la zaidi ya nyuzi joto 82, kwa mujibu wa kampuni ya MTPak Coffee.

Hatari ndogo kwa ujumla

Watafiti wanadokeza kuwa takriban kisa kimoja au viwili kati ya kila visa 10 vya saratani ya umio vinaweza kuepukika iwapo watu wataacha kunywa vinywaji vya moto sana.

Saratani ya umio ya aina ya *squamous cell* ni nadra, ikiathiri maelfu kiasi ya watu kwa mwaka. Nchini Uingereza, takriban asilimia 1 ya watu wako katika hatari ya kupatikana kuwa na aina hii ya saratani wakati fulani katika maisha yao.

Hivyo, hata kama vinywaji vya moto kupita kiasi vinaweza kuongeza hatari, uwezekano wa mtu kupata saratani hiyo bado ni mdogo.

Pia kuna sababu nyingine, kama vile uvutaji sigara, ambazo huleta hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya umio.

Fiona Osgun kutoka shirika la Cancer Research UK, lililofadhili utafiti huo, alisisitiza: "Njia muhimu zaidi za kupunguza hatari ya aina hii ya saratani ni kutovuta sigara na kupunguza unywaji wa pombe."

Dalili za saratani ya umio zinaweza kujumuisha kiungulia, tatizo la usagaji wa chakula au maumivu ya koo au kifua, pamoja na kupungua kwa uzito.