WARIDI WA BBC: 'Miaka 7 bado ninasubiri mwanangu kuniita mama'

    • Author, Na Martha Saranga
    • Nafasi, BBC SWAHILI
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

"safari yangu ilikuwa ngumu, yenye miiba, yenye mateso, kwasababu baada ya kujifungua mtoto wangu, nikagundua ana changamoto wa utindio wa ubongo, kwahiyo yale machozi ya furaha ya kupata mtoto yaligeuka kuwa machozi ya uchungu sasa, kwasababu ni kitu kigumu kukipokea, lakini namshukuru Mungu amenitengeneza kuwa chombo hodari."

Ndivyo anavyoanza kusimulia Rehema Simfukwe muimbaji wa nyimbo za injili nchini Tanzania ambaye safari yake ya uzazi na malezi ya watoto wake watatu akiwemo Dorcas 7, aliyezaliwa na changamoto ya utindio wa ubongo haikuwa rahisi.

"Ndani ya moyo wangu mimi na mume wangu, tulikuwa tuna matarajio mengi sana, kwa mtoto wetu akikua, unajua hiyo hali kwa mtu yeyote yule… lakini kwangu ilikuwa tofauti. Alisimulia Rehema kwa hisia

Rehema ambaye kupitia nyimbo kama Chanzo, Ndiyo yako na Nina ushuhuda alijizolea umaarufu katika anga la muziki wa injili Afrika mashariki tangu mwanzoni mwa mwaka 2020 anasema wakati wote huo alikuwa akipambana na huzuni na uchungu uliotokana na kutokubali hali ya mwanae wa kwanza.

'Nilitabasamu jukwaani kuficha huzuni yangu'

"Kwanza sikuwa nakubali kwamba mwanangu ana changamoto, na hata watu walipokuwa wakiniuliza Dorcas yuko wapi? Nawaambia tu Dorcas yuko shule, yuko shule mbona hatumuoni? Nawaambia yuko kwa bibi yake, yupo shule ya bweni (boarding). "

''Nilisimama jukwaani nikaimba kwa ujasiri na furaha wakati mwingine lakini nilijikaza na kuficha huzuni yangu''

Wakati ninarekodi wimbo wa Chanzo nakumbuka kilikuwa kipindi cha COVID19, mikusanyiko ilikuwa imepigwa marufuku na tuliishi kwa tahadhari kubwa, niliwaambia wanakikundi wenzangu tukutane ili kurekodi wimbo huo baada ya kufanya mazoezi' nilijitahidi kukwepa maswali na kufurahi ili kutoonesha huzuni yangu.

Rehema anasema alitumia mbinu zote kuficha tu hali ya binti yake akiamini kuna isku atakuwa sawa na ataweza kutoka nae hadharani. Maswali mengi ya watu yalimfanya awajibu tu ili kuwaridhisha.

Anasema kila alipomwangalia binti yake haikumuingia akilini kwa vipi awe katika hali hiyo.

Hakuikubali changamoto hiyo kirahisi hadi pale alipopata usaidizi wa kitaalamu na ushauri nasaha kutoka hospitali na kwa baba na mama yake ambao ni wahudumu wa afya jijini Dar es salaam ambao hawakuchoka kuzungumza na kumsaidia katika malezi ya binti yake.

"Niliwaza mtoto wangu mbona hatoi udenda? Mbona hafanyi hiki? Kwahiyo kichwani mwangu nilikuwa na picha fulani niliyojiwekea kuwa mwanangu hawezi kuwa hivi''

'Si kweli kwamba tumezaa misukule'

Jamii yetu bado haina elimu ya kutosha kuhusiana na tatizo la utindio wa ubongo. Anasimulia Rehema kwamba baada ya kujivika ujasiri na kukubali hali ya binti yake aliweza kuzingatia ushauri wa kitaalamu aliopatiwa na kuamua kuyagusa hasa maisha ya wanawake wenye changamoto kama yake.

Rehema anasema wanawake aliokutana nao na kuwasaidia wanamuambia kauli nyingi walizokutana nazo zilizowavunja moyo.

'Kauli kama tumezaa misukule, tulikuwa tunatafuta utajiri tukakosea masharti mtoto ndio ametoka hivi' hii ni potofu kabisa

Kauli kama hizo hazifai na mara zote nimewashauri wanawake wenye watoto wenye changamoto zozote za kiafya kutozingatia kauli zinazoshusha utu wetu au watoto wetu.

Si kweli kwamba watoto wenye utindio wa ubongo wamerogwa.

Tunajifunza kumuamini Mungu kwani ndie mpaji wetu. Ninawafundisha kumshukuru Mungu kwa zawadi hii ya watoto aliyotupa.

Nimekuwa nikiwaambia wanawake kuwa watoto hawa ni darasa Mungu ametupa tujifunze ili tukaisaidie jamii.

Kuna watoto ambao wana utindio wa ubongo ambao hawawezi kujisogeza kabisa, kuna wengine wanaweza kufanya hiki au kile wanahitaji msaada na wakipata msaada stahiki kwa wakati wanaweza kumudu vitu fulani fulani kuliko kuwakatia tamaa na kuwaacha au kuwaficha.

Mimi nimekuwa daraja la kuwakutanisha wanawake ambao wana changamoto hii hapa jijini Dar es salaam.

Nimegusa maisha ya watoto 80 kupitia kituo cha Dorcas

Ule uchungu na chachu ya kusema hapana, lazima nifanye kitu kwasababu nimeona kuna pengo, hilo pengo lipo, kwenye jamii yetu.

Kituo cha Dorcas homecare initiative kilizaliwa kama utani tu, na nimekuwa nikipokea msaada kutoka kwa watanzania na makundi mbalimbali ya watu wenye mapenzi mema na kizazi hiki.

Ninaguswa na maisha ya wanawake wenzangu waliokwama kimaisha na hata kukimbiwa na wenzi kutokana na kupata mtoto mwenye utindio wa ubongo.

Kuna wanawake wameacha kazi, wameacha biashara na hata wengine kuacha masomo lakini kupiti akituo chetu tumewatia moyo na kuwatafutia namna ya kuzipigania ndoto zao tena ili maisha yaendelee.

Rehema anasema kuna watoto ambao wana utindio wa ubongo na wanaweza kwenda shule, kuna watoto wana utindio wa ubongo na wanaweza kujisogeza kutoka hapa kwenda pale, lakini pia kuna watoto wenye utindio wa ubongo ambao hata kuongea hawawezi, hata kuita mama hawawezi, nimesubiri mtoto wangu aniite mama huu ni mwaka wa saba na hajawahi kuniita hata mama, kwahiyo unaona?

Kuna watoto hao wa aina hiyo amba oni ngumu kuelewa hisia zao, wanahitaji uangalizi wa karibu sana, kwahiyo nikawa najiuliza kwahiyo ina maana mtoto wa aina kama Dorcas nani atamchukua?

Kwahiyo hapo nikajenga swali, na nikaanza kufanya utafiti, mama yangu aliponipokea wakati napata muda wa kwenda kazini nikaanza kutoka, nikaanza kujifunza, nikaanza kuona kuwa kama nikipokelewa mtoto hata kwa muda mfupi, ninaweza kufikia ndoto yangu.

Kwahiyo kutokea hapo ndio nikaanza kujenga ujasiri kwamba lazima nifanye kitu kwaajili ya wazazi wengine wenye watoto wa aina kama wa Dorcas."

Niliwatafuta kupitia usaidizi wa serikali za mitaa na kuwapata.

Nilikusudia kuwasaidia kumi tu lakini sasa ninao 80 katika kituo cha Dorcas homecare initiative.