Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, nchi za Kiarabu zinatarajia nini katika mazungumzo ya Marekani na Iran?
Kulikuwa na hali ya afueni miongoni mwa nchi za Baraza la Ushirikiano wa Ghuba (GCC) wakati Marekani na Iran zilipokubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa wiki mbili tarehe 8 Aprili.
Tangazo hilo lilimaanisha kusitishwa kwa muda kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran ambayo yalikuwa yakilenga miundombinu ya kijeshi na kiraia katika nchi hizi.
Mwitikio wa nchi wanachama wa GCC umekuwa sawa katika mambo mengi, hasa wito wao wa kawaida wa kufikia suluhisho la muda mrefu na kuhakikisha kupita kwa bure kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Wakati huo huo, Umoja wa Falme za Kiarabu umechukua sauti kali zaidi katika kulaani Tehran. Kinyume chake, Oman imechukua msimamo tofauti, zaidi katika kuikosoa Washington na kujihusisha moja kwa moja na Tehran.
Swali kuu sasa ni iwapo makubaliano yoyote kati ya Marekani na Iran yanaweza kutoa kile ambacho nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba hatimaye zinataka.
Qatar
Jibu la Qatar limejikita katika kupunguza mivutano, ushirikiano wa kikanda, na kulinda mtiririko wa nishati duniani.
Majid Al-Ansari, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, alisema katika mkutano na waandishi wa habari Aprili 14 kwamba kipaumbele cha haraka cha Doha ni "kuimarisha usitishaji mapigano... na kuwa amani ya kudumu."
Doha pia imetoa wito wa kuwepo kwa mfumo mpana wa "kikanda" wa mazungumzo ambayo yatajumuisha mataifa ya Ghuba na nchi zilizounganishwa kwenye eneo hilo kupitia "minyororo ya ugavi."
Moja ya matakwa makuu ya Qatar ni kulinda usalama wa baharini. Bw. Ansari alielezea kuendelea kwa biashara kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz kama "muhimu kwa usalama wa kimataifa" na akakataa matumizi ya kifungu hicho kama "chombo cha shinikizo au mazungumzo."
Katika mkutano mwingine na waandishi wa habari mnamo Aprili 21, alisema kuwa kuhakikisha usafirishaji kwenye njia hii ni "jukumu la pamoja" kwa nchi zote, sio jukumu la nchi moja pekee.
Qatar pia imeunga mkono juhudi zinazoendelea za upatanishi na kuzungumzia "uratibu wa hali ya juu" na Pakistan, Marekani na wapatanishi wengine, ingawa haijatoa maelezo zaidi.
Saudia
Licha ya malengo ya Dira ya 2030 ya kuleta mseto wa uchumi wa Saudia, mafuta yanasalia kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa nchi hiyo.
Hatari ya kuendelea kwa migogoro inaweza kuhatarisha zaidi mchakato wa mabadiliko ya uchumi wa nchi.
Ingawa vita hivyo vimefichua vikwazo vya makubaliano ya 2023 kati ya Saudi Arabia na Iran, yaliyosimamiwa na China, nchi hizo mbili zimedumisha mawasiliano ya kidiplomasia.
Hata hivyo, ripoti kwamba Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman ameihimiza Washington kuendelea kuishambulia Iran zinaonyesha kuwa Riyadh huenda ikapendelea ushindi wa kijeshi.
Mohammed bin Salman alionya mwaka 2018: "Ikiwa Iran itapata bomu la nyuklia, tutafuata njia hiyo hiyo haraka iwezekanavyo."
Wasiwasi mwingine wa Riyadh ni uungaji mkono wa Tehran kwa vikosi vya wakala wa kikanda, haswa Houthis katika nchi jirani ya Yemen.
Nchi hii ya Ghuba ya Uajemi huenda ikapoteza mojawapo ya njia zake muhimu za kusafirisha mafuta ikiwa Wahouthi watatekeleza tishio lao la kufunga Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab.
Bahrain
Bahrain iliunga mkono kusitishwa kwa mapigano na kufungua tena sehemu ya Mlango-Bahari wa Hormuz. Nchi hiyo ilitoa wito wa "kukomeshwa mara moja na kikamilifu kwa mashambulizi yote ya chuki na yasiyochochewa ya Iran."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Bahrain ilisisitiza tarehe 8 Aprili ulazima wa kupatikana "suluhisho la kudumu ambalo litahakikisha Tehran haipati silaha za nyuklia" na pia kuzuia uwezo wake wa kutengeneza silaha nyinginezo.
Nchi hiyo pia ilitoa wito wa kukomeshwa kwa "matumizi ya vikosi vya wakala" vya Iran na "uingiliaji kati wake wa kikanda."
Manama alitoa wito wa kuwepo kwa makubaliano ambayo yatahakikisha "usalama wa urambazaji wa kimataifa wa baharini na angani," ikiwa ni pamoja na katika Mlango-Bahari wa Hormuz, na kusisitiza haja ya "uthabiti wa usambazaji wa nishati na mtiririko huru wa biashara ya kimataifa."
Bahrain pia iliitaka Tehran kulipa "fidia kamili, yenye ufanisi na ya haraka... kwa uharibifu na majeraha yaliyosababishwa na mashambulizi yake."
Kuwait
Kuwait iliunga mkono usitishwaji wa mapigano Aprili 8, ikiunga mkono juhudi za upatanishi, ikisema mchakato huo unapaswa kuleta makubaliano ya kina na ya kudumu ambayo yanaimarisha usalama wa kikanda.
Kuwait ilitoa wito kwa Iran na washirika wake kusitisha mara moja vitendo vya uhasama, kuheshimu mamlaka ya nchi, na kujiepusha na "vitendo vinavyodhoofisha uthabiti wa kikanda."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait Sheikh Jarrah Jaber Al-Ahmad Al-Sabah alipinga juhudi za Iran kudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz, akisema njia hiyo ya maji iko chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa 1982 wa Sheria ya Bahari, ambao unahakikisha haki ya kupita.
Katika mkutano wa kimataifa kuhusu mkondo wa bahari mnamo Aprili 17, Kuwait ilisisitiza haja ya kuzidisha juhudi za kulinda usalama wa baharini na kuhakikisha kuwa Iran inafuata sheria za kimataifa.
Kuwait pia ililaani matumizi ya Iran ya makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani kulenga miundombinu na mali za kimkakati katika nchi za Ghuba ya Uajemi.
Umoja wa Falme za Kiarabu UAE
Miongoni mwa nchi za GCC, Umoja wa Falme za Kiarabu umechukua msimamo mkali zaidi wa kukosoa Iran, ikiishutumu Tehran kwa "uchokozi usio na msingi na usio halali." Abu Dhabi pia imekataa vikali simulizi ya Iran kwamba mashambulizi yake yalikuwa ya kulipiza kisasi.
Katika jibu la tahadhari kwa usitishaji vita, UAE ilitoa wito wa "uwazi zaidi" ili kuhakikisha "dhamira kamili ya Iran ya kukomesha mara moja uhasama wote katika eneo na ufunguzi kamili na usio na masharti wa Mlango-Bahari wa Hormuz."
Abu Dhabi pia ilitoa wito wa "hatua kamili" juu ya "uwezo wa nyuklia wa Tehran, makombora ya balestiki, ndege zisizo na rubani, nguvu za kijeshi na washirika wake na vikundi vya kigaidi vilivyounganishwa."
Pia imetoa wito wa kukomeshwa kwa "vita vya kiuchumi vya Iran na uharamia katika Mlango wa bahari wa Hormuz."
Anwar Gargash, mshauri wa rais wa UAE, pia alidai fidia kutoka kwa Iran katika taarifa iliyochapishwa kwenye Mtandao wa X mnamo Machi 29.
Abu Dhabi ilitishia kuungana na juhudi za Marekani za kuulinda mlango wa bahari huo ili "kukabili utawala ambao umekuwa tishio kuu kwa usalama wa Ghuba ya Uajemi."
Oman
Oman, ambayo ina historia ndefu ya upatanishi kati ya Washington na Tehran, siku zote imekuwa mtetezi mkali zaidi wa kudorora kwa pande zote mbili na imefuata njia hii ndani ya mfumo wa sera yake ya nje ya "urafiki kwa wote na adui kwa yeyote."
Muscat pia imekuwa na misimamo mikali zaidi dhidi ya Marekani miongoni mwa wanachama wa GCC, kiasi kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Busaidi, baada ya kuanza mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, alionyesha kutofurahishwa na Washington kwa kuvuruga mazungumzo ya kabla ya vita.
Akihutubia Marekani, alisema: "Hivi sio vita vyenu." Matamshi yake yamekuja huku kukiwa na uvumi kwamba Israel ndiyo iliyochangia uamuzi wa Donald Trump kuishambulia Iran.
Muscat inasawazisha uanachama wake katika Baraza la Ushirikiano la Ghuba na uhusiano wake na Iran.
Oman ilikaribisha usitishwaji wa mapigano, lakini ilitaka "kukomeshwa kwa kudumu kwa hali ya vita" katika eneo hilo.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa Oman na Iran zinafanyia kazi itifaki ya pamoja ya kufuatilia usafiri wa baharini katika Mlango wa bahari wa Hormuz.
Mnamo Aprili 4, maafisa wakuu wa Omani na Irani walijadili "chaguo zinazowezekana za kuhakikisha mtiririko wa trafiki" kwenye njia ya maji.