Maharamia wateka meli nyingine karibu na pwani ya Somalia
Mamlaka za baharini zinaonya kuhusu tishio kwa meli zinazopita katika pwani ya Somalia baada ya meli ya mizigo kukamatwa katika kitendo kinachoshukiwa kuwa cha uharamia.
Kituo cha Biashara za Baharini cha Uingereza (UKMTO) kimeongeza kiwango cha tishio katika eneo hilo baada ya watu kuiteka meli na kuilekeza iende kwenye maji ya eneo la Somalia siku ya Jumapili.
Meli nne zimetekwa katika matukio yanayoshukiwa kuwa ya uharamia katika wiki iliyopita ikiwemo meli ya uvuvi na meli ya mafuta.
Miaka mitatu iliyopita uharamia ulikuwa umetoweka katika eneo hili la Bahari ya Hindi ambalo hapo awali lilikuwa maarufu kwa utekaji nyara.
"Kutokana na tishio la uharamia meli zinashauriwa kusafiri kwa tahadhari," UKMTO ambayo inahusika na masuala ya usalama baharini imesema katika taarifa yake.
UKMTO ilisema katika taarifa kwamba utekaji nyara huo wa siku ya Jumapili ulitokea maili sita kutoka Garacad, Somalia. Hakuna maelezo zaidi yaliyoripotiwa.
UKMTO pia ilitoa onyo kuhusu utekaji nyara mwingine kando ya pwani ya Mareeyo, kaskazini mwa Somalia uliotokea tarehe 21 Aprili.
Maharamia pia waliteka nyara meli ya mafuta, Honour 25, ikiwa na wafanyakazi 17 iliyokuwa ikisafiri karibu na pwani ya Somalia Aprili 22, kulingana na maafisa kadhaa wa usalama waliozungumza na BBC .
UKMTO pia iliripoti kwamba meli ya uvuvi yenye bendera ya Somalia ilitekwa Alhamisi.
Watu wawili wenye silaha pia walijaribu kupanda meli ya mizigo kutoka kwenye boti ndogo siku ya Alhamisi, UKMTO iliripoti, ingawa walishuka baada ya wafanyakazi wa meli hiyo kufyatua risasi za onyo.
Kati ya mwaka 2005 na 2012, maharamia kutoka Pembe ya Afrika walipata kati ya dola milioni 339 (£266m) na dola milioni 413 (£325) kwa kuwashikilia mateka wafanyakazi na kudai malipo ya fidia, kwa mujibu wa makadirio ya Benki ya Dunia.
Pia unaweza kusoma: