Ndani ya 'dhehebu' la Epstein, na simulizi za wanawake aliowanyanyasa kwa miaka mingi

Wiki moja tu baada ya kifo cha Jeffrey Epstein, aliyekuwa amehukumiwa kwa makosa ya unyanyasaji wa kingono, Anya ambalo si jina lake halisi alifungua mlango wa nyumba yake jijini New York na kumkuta Mark Epstein, kakake Jeffrey Epstein, akiwa mlangoni mwake na kumwambia ahame eneo hilo.
Mark Epstein amekanusha kuwa na ufahamu wowote kuhusu vitendo au makosa ya ndugu yake.
Anya anasema kuwa alipoondoka katika nyumba hiyo, alipoteza si tu mahali pa kuishi, bali pia alianza kutoka kwenye jinamizi ambalo lilikuwa limemnasa kwa miaka mingi.
"Bado ninajaribu kukubaliana na ukweli kwamba nilinyanyaswa kwa miaka mingi," anasema Anya.
Kulingana naye, ingawa kwa nje alionekana kuwa huru, kwa uhalisia alikuwa amefungwa na minyororo isiyoonekana.
Katika mahojiano nadra na BBC, Anya ameelezea maisha yake kama mmoja wa "wasaidizi" wa Jeffrey Epstein na kufafanua jinsi Epstein alivyoweza kudumisha ushawishi na udhibiti wa waathiriwa wake kwa miaka mingi.
Kwa mujibu wa Anya, "wasaidizi" hao walikuwa kundi la wanawake takribani 12. Anasema Jeffrey Epstein aliwapatia makazi, aliwahitaji wawe tayari kumhudumia saa zote za mchana na usiku, na aliwanyanyasa kingono mara kwa mara.
Anya anasema wanawake hao walivutiwa mwanzoni na ahadi za uongo na nafasi za kazi ambazo hazikuwepo. Hata hivyo, polepole Epstein alichukua udhibiti wa karibu kila sehemu ya maisha yao, akitumia udhaifu au hali yoyote ya hatari aliyogundua kwa kila mmoja wao na kuwatawala.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Anaelezea kuwa Epstein alidhibiti fedha zao, aliamua ni watu gani walioruhusiwa kukutana nao, na aliendelea kudhoofisha hali yao ya kujiamini kupitia udhalilishaji wa kisaikolojia.
Kulingana na Anya, Epstein alikuwa na msisimko wa kupindukia kuhusu miili ya wanawake, na hata alimlazimisha kufanyiwa upasuaji ambao haukuwa wa lazima na ambao ulimwacha na ulemavu.
Maelezo ya Anya kuhusu mbinu ambazo Jeffrey Epstein alitumia kuwatawala waathiriwa wake yanaendana na ushahidi uliotolewa na Sarah Klein, aliyekuwa mmoja wa wasaidizi wake, mbele ya Kamati ya Bunge la Marekani ya Uangalizi mapema mwaka huu.
Sarah Klein alisema Epstein alijionyesha kama mtu aliyekuwa akiwaokoa na kuwasaidia wasaidizi wake.
"Alikuwa na uwezo wa kipekee wa kuvunja uwezo wako wa kufanya maamuzi kwa kujitegemea na kukunyima hisia ya uhuru na uwezo wa kujiamulia mambo. Hilo lilikufanya umtegemee zaidi na zaidi," alisema.
Dkt. Tara Quinn-Cirillo, mwanasaikolojia wa kitabibu ambaye amefanya kazi na waathiriwa wa udhibiti wa kulazimishwa anasema imani ya kwamba watoto pekee ndio walio katika hatari ya kukumbwa na mbinu hizo si sahihi.
"Watu wazima pia wanaweza kuwa waathiriwa wa mchakato wa kudanganywa na kutayarishwa ili kunyanyaswa mtu yeyote anaweza kuwa katika hatari ya kuathiriwa na tabia za aina hii."
Mpango uliopangwa kwa umakini
Baada ya Jeffrey Epstein kukamatwa mwaka wa 2008 kwa kosa la kumnyanyasa kingono msichana mwenye umri mdogo aliyekuwa amemshawishi kwenda nyumbani kwake kwa ahadi ya kazi ya ukandaji mwili,anadaiwa kubadili mbinu zake. Kuanzia wakati huo, alianza zaidi kuwalenga wanawake wazima, wengi wao wakitoka Urusi na nchi nyingine za Ulaya Mashariki.
Hata hivyo, Anya anasema yeye na wanawake wengi walioingizwa kwenye mtandao huo bado walikuwa na mwonekano wa wasichana wadogo.
Anya alikulia nchini Urusi muda mfupi baada ya kuanguka kwa utawala wa kikomunisti. Anasema wazazi wake waliokuwa wakali walimfundisha kwamba, "Njia pekee ya kufanikiwa ni kupitia elimu."
Lakini nafasi za ajira zilikuwa chache. Licha ya kuwa na shahada ya chuo kikuu, aliondoka Urusi kwenda kutafuta maisha kama mwanamitindo.
Anasema alifanya kazi barani Ulaya akihusishwa na kampuni maarufu za kifahari kama Fendi na Chanel.
Wakati huo alikuwa na marafiki, watu waliomuunga mkono, na familia ambayo aliweza kuitembelea nchini Urusi wakati wowote alipotaka.
Anya anasema, aliingia katika mtandao wa Jeffrey Epstein akiwa na umri wa miaka ishirini na kitu, baada ya kutembelea wakala wa wanamitindo mjini Paris na kukutana na Daniel Siad, aliyekuwa akisaka vipaji vya uanamitindo.
Anya anasema Siad alimpongeza kwa uerevu wake, akimwambia kuwa si jambo la kawaida katika sekta ya uanamitindo. Baadaye alimwambia angemtambulisha kwa rafiki yake aliyekuwa na ushawishi mkubwa na uhusiano mpana katika tasnia ya mitindo, Jeffrey Epstein.

Chanzo cha picha, US Department of Justice
Anya anasema alitumia miaka mingi akijiuliza nini kingetokea kama asingetembelea wakala huo wa wanamitindo siku ile. Hata hivyo, sasa anaamini kwamba alilengwa tangu mwanzo.
"Yote yalikuwa yamepangwa mapema," anasema, akimtaja Daniel Siad kuwa " mfanyabiashara wa usafirishaji haramu wa watu."
Jina la Daniel Siad linaonekana mara nyingi katika nyaraka zinazohusiana na Jeffrey Epstein, zilizochapishwa na serikali ya Marekani mwezi Januari.
Wakili wa Siad alisema hakuweza kupatikana kutoa maoni, lakini Siad amewahi kusema hapo awali kwamba hakuwa na ufahamu kuhusu tishio lolote kutoka kwa Epstein.
Anya anasema alikutana kwa mara ya kwanza na Jeffrey Epstein katika nyumba yake kubwa ya vyumba 18 mjini Paris, iliyokuwa imepambwa kwa picha za Epstein akiwa pamoja na watu mashuhuri, akiwemo Bill Clinton na viongozi wengine wa dunia.
Anasema uwepo wa wanawake wengine wawili ndani ya nyumba hiyo mmoja kutoka Urusi na mwingine aliyekuwa mpenzi wa Epstein wakati huo kutoka Ulaya Mashariki ulimfanya ajisikie salama.
Kwa mujibu wa Anya, Epstein alimwomba avue nguo ili aweze "kukagua" mwili wake kwa madai ya kazi ya uanamitindo.
Anya anasema alipokuwa amesimama akiwa amevaa nguo za ndani pekee, Epstein alimwambia kuwa "hakuwa katika umbo zuri," alimtaka "aanze kufanya mazoezi," na akamwita "mvivu."

Chanzo cha picha, Getty Images
Anya anasema haikuwa jambo la ajabu kusikia maoni kama hayo katika sekta ya uanamitindo, hivyo aliamini madai ya Epstein kwamba kama angejitahidi, angemtambulisha kwa watu sahihi ambao wangeweza kumsaidia kujenga taaluma yake.
Anasema Epstein alimuuliza maswali kuhusu familia yake, mambo aliyopenda na malengo yake maishani.
"Aliniuliza unataka kufanikisha nini maishani, kwa nini uliingia kwenye uanamitindo na ni mambo gani ni muhimu kwako."
Anya anasema katika ulimwengu wa mitindo, si kawaida watu kuulizwa maswali ya aina hiyo.
Wanawake wengine kadhaa pia wameiambia BBC kwamba Epstein alipenda kujua mambo yaliyokuwa muhimu kwao ili baadaye aweze kuyatumia kuwatawala na kuwashinikiza.
Anya anasema pia Epstein alijibu moja kwa moja hofu aliyokuwa nayo.
Anakumbuka Epstein akimwambia:
"Naona wewe ni mwerevu na una mashaka na kila kitu. Sitashiriki mapenzi na wewe."
Kwa mujibu wa Anya, maneno hayo yalimfanya ajisikie salama zaidi.
"Nilijiambia, Mungu wangu, huyu mtu ni wa kipekee. Anaonekana kuelewa tabia yangu vizuri sana."
Mchakato wa polepole wa kujenga imani
Lakini, kwa mujibu wa Anya, huo ulikuwa mwanzo tu wa mchakato wa kudanganywa na kuandaliwa ulioendelea kwa miezi kadhaa, hadi akanaswa katika mtandao wa ahadi zisizotimizwa na udanganyifu uliopangwa kwa makini.
Anya anasema kwa karibu mwaka mmoja alifanya mazoezi kupita kiasi ili kupata umbo la mwili ambalo Epstein alitaka.
Kwa mujibu wake, Leslie Graff, aliyekuwa msaidizi mkuu wa Epstein na msimamizi wa ratiba zake za kila siku, alikuwa akimtaka mara kwa mara atume taarifa za jinsi anavyoendelea kupitia barua pepe. Pia anasema Epstein alimshinikiza kutuma picha zake, na alipomwomba atume picha za uchi alimwambia, "Usione aibu."
Hatimaye, Anya anasema Epstein alipanga akutane na Faith Kates, mmoja wa waanzilishi wa wakala wa wanamitindo wa Next Management, kama alivyokuwa ameahidi.
Kwa mujibu wa Anya, mkutano huo haukudumu zaidi ya dakika 30, na mwisho wake aliambiwa kwamba Epstein angemjulisha matokeo baadaye.
Anya anasema baadaye Epstein alimwambia kwamba wakala wa Next Management alikataa kumpa kazi kwa sababu "hakuwa mzuri vya kutosha kwa soko la New York," na tena akamwambia kuwa "hakuwa katika umbo zuri."

Chanzo cha picha, Getty Images
Anya anasema hali hiyo ilimvunja moyo sana.
Baadaye, Epstein alimwomba aende Palm Beach, Florida, ambako alikuwa akitumikia kifungo chake akiwa kwenye utaratibu wa kuruhusiwa kutoka gerezani mchana na kurejea baadaye (work release).
Kwa mujibu wa Anya, Epstein alidai kuwa kukamatwa kwake kulitokana na msichana aliyemdanganya kwa kutumia kitambulisho bandia.
Anya anasema ili kumuona Epstein, alilazimika kuandika jina lake kwenye daftari lililokuwa likisimamiwa na askari wa polisi aliyevaa sare.
Anasema Epstein alimpeleka katika chumba kilichokuwa nyuma ya jengo hilo, ambako alimnyanyasa kingono kwa mara ya kwanza.
Wanawake wengine wasiopungua wawili pia wameeleza kwamba Epstein aliwanyanyasa kingono katika kipindi hichohicho alipokuwa akitumikia kifungo chake.
Anya anasema baada ya tukio hilo, Epstein alitoka naye nje ya chumba na, huku wasaidizi wengine wakisubiri nje, alitania kwamba Anya alikuwa "mwenye aibu sana."
Anasema watu wote walicheka, jambo lililomfanya ajihisi mwenye hatia.
"Nilijiambia, 'Labda hakuna jambo baya lililotokea. Labda mimi ndiye niliyetafsiri vibaya kilichotokea,'"
anasema Anya.
Anaongeza:
"Labda ni kutokana na malezi yangu ya Kirusi au ukali wa wazazi wangu, lakini nilihisi huenda tatizo lilikuwa kwangu, si kwake."
Anya anasema ni baada tu ya nyaraka zinazohusiana na Epstein kutolewa hadharani ndipo alipotambua kilichokuwa kimemtokea.
Kwa mujibu wa barua pepe zilizomo kwenye nyaraka hizo, licha ya kukutana ana kwa ana na Faith Kates wa wakala wa wanamitindo wa Next Management, ombi lake lilikuwa limekataliwa mwaka mmoja kabla ya mkutano huo.
Anya anasema baadaye aligundua kwamba Epstein alimuweka katika hali ya kusubiri kwa miezi kadhaa, akimshawishi kwa ahadi zisizotimia. Kwa maelezo yake, huo ulikuwa "mchakato wa hali ya juu na uliopangwa kwa umakini wa kumnasa mwathiriwa." Baada ya kumweka katika mazingira ya udhaifu akiwa mbali na familia yake, Epstein alitumia fursa hiyo kumnyanyasa.
Dkt. Tara Quinn-Cirillo anasema mchakato wa polepole ambao Anya ameuelezea ulilenga kutomfanya mwathiriwa atambue hatari mapema.
"Ni kama ndege za kivita zinazotengenezwa ili zipite bila kugunduliwa na rada."
Katika taarifa kwa BBC, wakili wa Faith Kates amesema madai kwamba mteja wake alijua kuhusu mtandao wa usafirishaji haramu wa watu wa Epstein au alihusika nao ni "ya uongo kabisa na yanachafua jina lake."
Wakili huyo pia amesema madai kwamba Epstein ndiye alikuwa anapaswa kumjulisha Anya uamuzi wa wakala huo ni " ya uongo na yasiyokuwa na ushahidi."
Taarifa hiyo ilisema kuwa Next Management ilifanya maamuzi yake yenyewe kuhusu kuwapokea au kuwakataa wanamitindo na haikuhitaji idhini ya Epstein kufanya maamuzi hayo.
Iliongeza kuwa si jambo la ajabu kwa mwanamitindo kutathminiwa na baadaye kukataliwa, hata zaidi ya mara moja.
Next Management pia ilisema haikuwa na uhusiano wowote na Jeffrey Epstein na kwamba vitendo vinavyodaiwa kufanywa na Faith Kates vilikuwa vya binafsi.
Anya anasema Epstein aliendelea kumfanya aamini kwamba bado angeweza kupata mafanikio katika uanamitindo kwa kuendelea kumpa matumaini ya kazi.
Alimtambulisha kwa Jean-Luc Brunel, mwanzilishi wa wakala wa wanamitindo wa MC2, lakini hakumweleza kwamba alikuwa mmoja wa wafadhili wa kifedha wa kampuni hiyo.
Ofisi za MC2 mjini Miami na New York zimefungwa. Mwanzilishi wa tawi lililosalia nchini Israel pia amewahi kusema kwamba hakuwa na uhusiano wowote na Epstein.
Anya anasema hakupata kazi nyingi kupitia wakala huo. Badala yake, meneja wake alimwambia aende Palm Beach kwa kile alichoelezwa kuwa ni "kazi maalumu." Hata hivyo, anasema hakukuwa na kazi yoyote ya uanamitindo, na safari hizo zilisababisha tu kuendelea kunyanyaswa na Epstein.
Baada ya muda, Anya anasema Epstein alimwambia kwamba nafasi yake ya kufanikiwa katika uanamitindo ilikuwa ndogo na kwamba sekta hiyo haikuwa tena na fursa nyingi kama zamani.
Kisha, kwa mujibu wa Anya, Epstein alimwambia:
"Njoo unifanyie kazi. Nitakufundisha jinsi ulimwengu halisi wa biashara unavyofanya kazi. Utasafiri na utakutana na watu muhimu kutoka kila kona ya dunia."

Chanzo cha picha, Miami Herald via Getty News
Anya anasema hali hiyo ilimvunja moyo sana.
Baadaye, Epstein alimwomba aende Palm Beach, Florida, ambako alikuwa akitumikia kifungo chake akiwa kwenye utaratibu wa kuruhusiwa kutoka gerezani mchana na kurejea baadaye .
"Alinialika kufanya kazi naye"
Badala yake, Anya anasema muda wake mwingi uliishia kusubiri Jeffrey Epstein ampatie kazi, huku wakati huohuo akimkosoa na kumdhalilisha kwa kumwambia "hafanyi chochote."
Wakati mwingine alimpa kazi rahisi tu, kama kujibu simu, kuwaelekeza wageni kwenye chumba cha mikutano au kutangaza kuwasili kwa wageni.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Anya, wasaidizi walitakiwa wawe tayari kupatikana saa zote za mchana na usiku.
Anasema siku moja alitoka kwenda kula chakula cha mchana na kukutana na mtu, lakini Epstein "alikasirika sana," akimpigia simu mara kwa mara na kumwambia hakuwa na haki ya kuondoka nyumbani bila ruhusa yake.
Kwa wakati huo, Anya anasema alikuwa amekuwa akimtegemea Epstein kwa karibu kila kitu.
Anasema alipougua na kuhitaji matibabu, Epstein alimwambia:
"Mimi ndiye bima yako ya afya."
Anya hakuwa na akaunti ya benki wala nyaraka zilizohitajika ili kukodisha nyumba yake mwenyewe. Hata hivyo, anasema Epstein alimfukuza mara kadhaa kutoka kwenye nyumba aliyokuwa akiishi Manhattan na kumwambia:
"Nenda ukajitafutie mahali pa kuishi."
Kwa mujibu wa Anya, vitendo hivyo vilikuwa sehemu ya mbinu za Epstein za kumdhibiti na kumfanya azidi kumtegemea.
Anya pia anasema Epstein alianza kumpa mshahara mdogo miaka kadhaa baadaye, na hilo lilifanyika tu kwa sababu masharti ya visa yake yalihitaji awe na ajira rasmi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mtandao wa unyanyasaji
Anya anasema sehemu iliyokuwa ngumu na ya kumuumiza zaidi wakati alipokuwa chini ya ushawishi wa Jeffrey Epstein ni kwamba alilazimika kuwashawishi wanawake wengine kuingia katika mtandao huo.
Akiwa amejawa na hisia, anasema kila mmoja wa "wasaidizi" alitakiwa kumtambulisha angalau mwanamke mmoja mwingine kwa Epstein, na kwamba alipendelea walenge wanawake vijana waliokuwa na umri unaokaribiana na wao.
"Ukiingia katika mzunguko huo, haijalishi umeingiza mtu mmoja au watu kumi; unahisi kwamba tayari wewe ni sehemu ya mfumo huo," anasema.
Anya anasema ameamua kuvunja ukimya wake sasa ili watu waelewe vizuri jinsi wanawake walivyonaswa katika mtego wa Epstein, na kwamba mtandao wake haukuhusisha tu unyanyasaji na usafirishaji haramu wa watoto, bali pia uliwalenga wanawake watu wazima, akiwemo yeye mwenyewe.
"Alikuwa ameunda mtandao mkubwa wa watu na mahusiano uliomwezesha kuendelea kuwanyanyasa waathiriwa wake," anasema Anya.
Anaongezea "Unapowaona watu kama Bill Gates wakija nyumbani kwake kwa chakula cha jioni na kumsalimia kwa kupeana mkono, unajiuliza, 'Mimi ni nani hadi nihoji hili? Mimi ni nani hadi nipinge?' Mahusiano hayo na kuungwa mkono kwake na watu wenye ushawishi vilifanya vitendo vyake vionekane vya kawaida na vya kuaminika."
Baadaye, Anya na Sarah Klein walipokea fidia kutoka Mfuko wa Fidia kwa Waathiriwa wa Jeffrey Epstein, ulioanzishwa kutoa msaada wa kifedha kwa manusura wa unyanyasaji. Ili kustahili fidia hiyo, waombaji walitakiwa kuwasilisha ushahidi unaothibitisha madai yao.
"Alipokuwa bado hai, sikuwahi kumweleza mtu yeyote kilichokuwa kimenitokea," anasema Anya.
Sasa ana matumaini kwamba simulizi yake inaweza kumsaidia hata mwanamke mmoja tu kutambua dalili za uhusiano wa unyanyasaji na kuutoroka.
"Mimi si mtu wa kipekee. Nilifanikiwa tu kupata nguvu ndani yangu zilizoniwezesha kupambana na kunusurika katika hali hiyo. Ikiwa mimi niliweza, basi wengine pia wanaweza."















