Kenya yaomba radhi kwa Warundi, yaahidi kuwalinda

Chanzo cha picha, Abraham Korir Sing'Oei / Facebook
Serikali ya Kenya imewaomba radhi raia wa Burundi wanaoishi nchini humo, baada ya baadhi yao kusema walitishwa au kutendewa vibaya.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kauli ya Rais wa Kenya, William Ruto, kuhusu raia wa kigeni wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo.
Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Korir Sing’Oei, Jumatatu alitembelea Ubalozi wa Burundi jijini Nairobi kuomba msamaha kwa wageni.
Sing’Oei amesema uamuzi wa serikali unawalenga raia wa kigeni wanaofanya biashara ndogo ndogo bila vibali, na si raia wote wa kigeni.
Amewataka Warundi kubaki watulivu, akisema serikali itaongeza idadi ya maafisa wa usalama katika maeneo yenye idadi kubwa ya Waburundi, yakiwemo Bahati na Muthurwa jijini Nairobi, ili kuwakinga dhidi ya vitisho au unyanyasaji.
Ameongeza kuwa wale wanaotaka kubaki Kenya watasaidiwa kujisajili na kupata nyaraka zinazohitajika. Wale wenye vibali vya kufanya biashara wataruhusiwa kuendelea na shughuli zao.
Sing’Oei amesema maono ya Kenya ni kuona Waafrika wote, hasa wanaoishi Afrika Mashariki, wakiishi pamoja kama ndugu.
Mamia ya Warundi walikuwa wamekusanyika katika ubalozi huo wakiomba hati za kusafiria ili kurejea nchini kwao kutokana na hofu waliyonayo.
Pia Unaweza Kusoma;























