Moja kwa moja, Mashambulizi ya Wahouthi yazua hofu ya mzozo mpana zaidi Mashariki ya Kati na uharibifu wa uchumi duniani

Wapiganaji wa kundi la Houthi nchini Yemen wanadai kushambulia meli katika Bahari ya Shamu—hatua inayotishia kuzidisha hali tete tayari iliyopo Mashariki ya Kati.

Muhtasari

  • Mataifa ya Kiarabu yapinga kuingia msikiti Al Aqsa kwa waziri wa Israel mwenye msimamo mkali.
  • Mashambulizi ya Wahouthi yazua hofu ya mzozo mpana zaidi Mashariki ya Kati na uharibifu wa uchumi duniani

Moja kwa moja

Lizzy Masinga

  1. Trump: 'Tutagharamia uharibifu wa meli kwa kutumia mali za Iran zilizozuiliwa nchini Marekani'

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Rais Donald Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social siku ya Alhamisi jioni: "Taarifa hii ichukuliwe kuwa tangazo rasmi hadi hapo taarifa nyingine itakapotolewa kwamba, kuanzia sasa na kuendelea, uharibifu wowote kwa meli, mizigo, au chochote kinachohusiana navyo, utalipwa kwa kutumia mali za Iran zinazomilikiwa na kudhibitiwa na Marekani.

    Uharibifu huo unaweza kuwa mkubwa sana, lakini hata hivyo, huu ndio uamuzi wa haki na usawa zaidi."

    Hata hivyo, matumizi ya mali za Iran zilizopo Marekani yanahitaji idhini ya mamlaka za kisheria na mahakama.

    Katika kesi zilizopita, kama vile maombi kutoka kwa manusura wa mashambulizi ya kigaidi ambayo Iran iliyaunga mkono au kuhusika nayo, mahakama za Marekani mara kwa mara zimeamua dhidi ya Iran na kusema kuwa haina haki ya kisheria ya kuamua kesi za aina hiyo.

    Bw. Trump pia aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi kuwa huenda akaamuru shambulio kubwa sana dhidi ya Iran siku ya Ijumaa asubuhi, shambulio ambalo rais huyo wa Marekani alilielezea kuwa "lisiloweza kulinganishwa" na mashambulizi ya awali.

  2. Marekani yatoza ushuru kwa mataifa kadhaa ya washirika wa biashara

    Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani imetangaza ushuru mpya kwa washirika wake 60 wa kibiashara, wanaowakilisha sehemu kubwa ya bidhaa zinazoingizwa nchini humo, kwa madai kwamba hawajachukua hatua za kutosha kukomesha ajira za kulazimishwa.

    Ushuru huo, unaoanzia asilimia 10 hadi 12.5, unazihusu nchi na maeneo muhimu ya kiuchumi, ikiwemo Uingereza, China, Umoja wa Ulaya, Canada, Japan na India.

    Unaanza kufanya kazi Ijumaa, baada ya ushuru wa muda wa asilimia 10 uliowekwa mapema mwaka huu kumalizika.

    Hatua hiyo ni mwendelezo wa mvutano wa vita vya kibiashara uliochochewa tena na Rais wa Marekani Donald Trump baada ya kurejea madarakani mwaka jana.

    Mapema mwaka huu, Mahakama Kuu ya Marekani iliamua kuwa ushuru mwingi uliowekwa duniani chini ya mamlaka ya dharura ulikuwa umeanzishwa kinyume cha sheria.

    Tangu uamuzi huo, Trump amekuwa akitafuta njia nyingine za kutekeleza sera yake kuu ya biashara.

    Mwezi uliopita, Ikulu ya Marekani ilipendekeza ushuru wa asilimia 10 hadi 12.5 kwa bidhaa kutoka mataifa kadhaa, ikidai hayafanyi juhudi za kutosha kukabiliana na ajira ya kulazimishwa.

    Siku ya Alhamisi, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani, Jamieson Greer, alisema ushuru huo utaanza kutekelezwa kwa maelekezo ya Rais Trump.

    Katika taarifa yake alisema hatua hiyo italenga kurekebisha ukiukwaji wa haki za binadamu na biashara isiyo ya haki, huku ikilenga kuboresha ustawi wa wafanyakazi duniani.

    Ushuru huo mpya utawahusu washirika 60 wakuu wa biashara wa Marekani, ambao kwa pamoja wanachangia asilimia 99.4 ya bidhaa zote zinazoingizwa nchini humo, kwa mujibu wa mamlaka za Marekani.

    Ofisi ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani ilisema kuwa Rais Donald Trump ameifanya marufuku ya uagizaji wa bidhaa zinazozalishwa kwa kutumia ajira ya kulazimishwa kuwa sehemu muhimu ya makubaliano ya biashara ya pande mbili na mataifa mengine.

    Kwa mujibu wa ofisi hiyo, hadi sasa washirika 10 wa kibiashara wamekubali kuweka marufuku hiyo katika makubaliano yao na Marekani, huku mataifa mengine yakichukua hatua kama hizo kufuatia uchunguzi uliofanywa katika wiki za hivi karibuni.

    Mataifa ambayo yameahidi kutunga na kutekeleza kikamilifu marufuku ya bidhaa zinazotokana na ajira ya kulazimishwa yatatozwa ushuru wa asilimia 10. Nchi ambazo hazijatoa ahadi hiyo zitatozwa ushuru wa juu zaidi wa asilimia 12.5.

    Mwakilishi wa Biashara wa Marekani, Jamieson Greer, alisema ameridhishwa na hatua za haraka zilizochukuliwa na baadhi ya washirika wa biashara kupiga marufuku bidhaa zinazozalishwa kwa ajira ya kulazimishwa, na akaeleza kuwa anatarajia kuhakikisha hatua hizo zinatekelezwa ipasavyo.

    Unaweza kusoma;

  3. Mlinzi wa J.D. Vance asimamishwa kazi kwa kuvujisha taarifa nyeti

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Shirika la Ulinzi wa Viongozi wa Marekani (US Secret Service) limetangaza kuwa mmoja wa maafisa wa kikosi cha ulinzi cha Makamu wa Rais J.D. Vance amesimamishwa kazi na anachunguzwa kwa madai ya kuvujisha taarifa nyeti.

    Maelezo kuhusu taarifa hizo zinazodaiwa kuvujishwa hayajawekwa wazi, lakini Anthony Guglielmi, msemaji wa shirika hilo, alisema afisa huyo anakabiliwa na uwezekano wa uchunguzi wa kijinai kuhusiana na madai ya kuhatarisha usalama wa operesheni na taarifa.

    "Tabia yoyote inayoweza kuhatarisha usalama wa mtu anayelindwa haitavumiliwa," aliongeza. Ikulu ya Marekani imekataa kutoa maoni kuhusu uchunguzi huo.

    Hata hivyo, mtandao wa MS Now uliripoti wiki iliyopita, ukirejelea vyanzo vinavyofahamu suala hilo, kwamba baadhi ya wanachama wa kikosi cha ulinzi cha Bw. Vance hawakuridhishwa na safari za familia yake. CNN iliripoti kuwa kusimamishwa kazi kwa afisa huyo kulihusiana na kuchapishwa kwa ripoti hiyo.

    Kulingana na MS Now, baadhi ya maafisa walikuwa wameonyesha kutoridhika katika majadiliano ya ndani kuhusu mipango ya safari za familia ya J.D. Vance, ikiwa ni pamoja na safari iliyopangwa ya helikopta ya kijeshi kumpeleka mtoto mdogo wa Makamu wa Rais kwenye mazoezi ya gofu, pamoja na safari za familia yake kutafuta nyumba katika eneo la Washington, D.C. BBC bado haijaweza kuthibitisha ripoti hizi kwa njia huru.

  4. Mataifa ya Kiarabu yapinga kuingia msikiti Al Aqsa kwa waziri wa Israel mwenye msimamo mkali

    .

    Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    Nchi nane za Kiarabu na Kiislamu zimelaani vikali kuingia kwa waziri wa Israel na walowezi katika Msikiti wa Al-Aqsa kupitia taarifa ya pamoja.

    Mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE), Jordan, Misri, Qatar, Uturuki, Pakistan, na Indonesia walitoa taarifa ya pamoja wakilaani vikali kitendo cha Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel, na walowezi wa Israel kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa.

    Taarifa hiyo, iliyotolewa jioni ya Alhamisi, Agosti 2, ilieleza kuwa kitendo hiki ni ukiukaji wa wazi wa hali ya kihistoria na kisheria ya Msikiti wa Al-Aqsa na uchokozi usiokubalika ambao unaweza kusababisha kuongezeka kwa mivutano katika eneo hilo.

    Nchi hizo nane pia zilisisitiza yafuatayo:

    Haja ya kuheshimu mamlaka ya usimamizi ya Jordan juu ya maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo mjini Jerusalem;

    Kupinga jaribio lolote la kubadilisha hadhi ya kihistoria na kisheria ya Msikiti wa Al-Aqsa;

    Haja ya kusitisha vitendo vya uchokozi na vya upande mmoja ambavyo vinaweza kuhatarisha usalama na utulivu wa eneo hilo;

    Kuzingatia sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Jerusalem. Taarifa hiyo ilitolewa baada ya Itamar Ben-Gvir kuingia katika eneo la Msikiti wa Al-Aqsa akiwa na mamia ya walowezi wa Israel, kitendo ambacho kimelaaniwa vikali na Wapalestina, Jordan, pamoja na nchi kadhaa za Kiarabu na Kiislamu.

  5. Mashambulizi ya Wahouthi yazua hofu ya mzozo mpana zaidi Mashariki ya Kati na uharibifu wa uchumi duniani

    .

    Chanzo cha picha, NASA Worldview/Reuters

    Wapiganaji wa kundi la Houthi nchini Yemen wanadai kushambulia meli katika Bahari ya Shamu, hatua inayotishia kuzidisha hali tete tayari iliyopo Mashariki ya Kati.

    Kwa kulazimisha meli kurejea nyuma kutoka kwenye mlango mwembamba wa bahari wa Bab el-Mandeb, wametishia kukatiza njia kuu ya usafiri wa baharini inayounganisha Ulaya na Asia.

    Haya yanajiri huku mashambulizi kati ya Marekani na Iran yakiendelea, na wakati ambapo makubaliano ya kuendeleza sekta ya nyuklia ya Saudi Arabia yakizua hofu ya mbio za silaha.

    Kwa sasa, mwaka wa 2026 unadhihirika kwa masikitiko kuwa mmoja wa miaka yenye vurugu na machafuko makubwa kwa baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati.

    Kwa usiku 13 mfululizo, Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) imefanya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran.

    "Vituo vya amri ya kijeshi vya Iran, ghala za kuhifadhia ndege zisizo na rubani (drones), mitandao ya mawasiliano, vituo vya ufuatiliaji wa pwani, na uwezo wa kijeshi wa baharini ili kudhoofisha zaidi tishio linaloletwa na Iran kwa mabaharia raia na meli za kibiashara zinazopita katika Mlango-Bahari wa Hormuz," ilisema Centcom katika taarifa yake usiku wa Alhamisi.

    Nchi za Kiarabu za Ghuba ambazo kwa kawaida ni maeneo tulivu yenye uhalifu mdogo na kodi nafuu sasa zinapaswa kujifunza kuishi huku zikikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa jirani yao mwenye silaha nyingi ng'ambo ya bahari: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

  6. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja