Kituo cha siri cha nyuklia cha Iran ambacho Trump anatishia kukishambulia

    • Author, Reza Sabeti
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kauli za hivi karibuni za Rais wa Marekani Donald Trump za kutishia kushambulia kile kinachoitwa Mlima Pickaxe zimeelekeza tena macho ya dunia kwenye moja ya maeneo yenye usiri mkubwa katika mpango wa nyuklia wa Iran.

Akizungumza kuhusu taarifa kwamba Iran imehamisha mashine za kisasa za kurutubisha urani, zinazojulikana kama centrifuge, kwenda katika eneo hilo la chini ya ardhi, Trump alisema Marekani italishambulia eneo hilo "kwa nguvu kubwa sana, pengine hivi karibuni."

Mlima Pickaxe, unaojulikana pia kama Kolang Gaz La, uko karibu kilomita mbili kusini mwa kituo cha nyuklia cha Natanz katika jimbo la Isfahan. Iran inasema eneo hilo linajengwa kuchukua nafasi ya kituo cha kutengeneza na kukusanya centrifuge kilichoharibiwa baada ya mlipuko wa mwaka 2020, ambao Tehran iliutaja kuwa hujuma huku lawama zikielekezwa kwa Israel, ingawa Israel haijawahi kukiri kuhusika.

Baada ya mlipuko huo, aliyekuwa mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Ali Akbar Salehi, alitangaza mpango wa kujenga kituo kipya, kikubwa zaidi na cha kisasa ndani ya mlima. Kufikia mwisho wa mwaka 2020, ujenzi wa eneo hilo ulianza kuonekana kupitia picha za satelaiti.

Picha za hivi karibuni zinaonyesha milango kadhaa ya mahandaki kwenye pande tofauti za mlima, huku wataalamu wakiamini kuwa kutokana na urefu wake wa zaidi ya mita 1,600 juu ya usawa wa bahari, huenda ndani yake kukiwa na ngazi nyingi za mahandaki ya chini ya ardhi. Hata hivyo, ukubwa halisi wa kituo hicho haujulikani kwa sababu hakuna mkaguzi wa kimataifa aliyeruhusiwa kuingia.

Baada ya vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel mwaka 2025, Iran iliimarisha ulinzi wa eneo hilo kwa kujenga ukuta unaozunguka karibu eneo lote la kituo.

Mnamo Februari 2026, picha za satelaiti zilizochambuliwa na Taasisi ya Institute for Science and International Security (ISIS) zilionyesha kuwa milango ya kuingilia mahandaki ya kituo hicho ilikuwa imeimarishwa.

Moja ya picha hizo ilionyesha kile kilichoonekana kuwa saruji mpya iliyomwagwa katika eneo la moja ya milango ya kuingilia, hatua iliyotafsiriwa kuwa sehemu ya kuimarisha ulinzi wa miundombinu hiyo ya chini ya ardhi.

Ingawa tathmini za wataalamu zinaonyesha kuwa kituo hicho bado hakijaonekana kuanza kufanya kazi kikamilifu.

Picha za satelaiti za Julai 9, 2026 zinaonekana kuonyesha kuwa baadhi ya milango ya kuingilia katika mahandaki ya Pickaxe Mountain bado ilikuwa wazi na inaweza kufikika.

Wakati huo huo, picha nyingine za satelaiti zinaonyesha kuwa hakukuwa na dalili kubwa za ujenzi upya katika vituo vya nyuklia vya Natanz, Fordow na Isfahan, ambavyo vilishambuliwa na Marekani pamoja na Israel.

Mnamo Julai 22, 2026, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisisitiza kuwa hakuna shughuli zozote za nyuklia zinazofanyika katika Pickaxe Mountain.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Institute for Science and International Security, eneo hilo lina nafasi ya kutosha kuweka kitengo kidogo cha kurutubisha urani kinachotumia centrifuge za kisasa, ambazo zina uwezo wa kuzalisha kiwango sawa cha urani iliyorutubishwa kwa kutumia mashine chache zaidi na katika eneo dogo. Hata hivyo, taasisi hiyo inasema haina ushahidi unaothibitisha kuwa mifumo hiyo ya centrifuge imewekwa katika eneo hilo.

Aidha, Taasisi ya Marekani ya Institute for Science and International Security inaamini kuwa eneo hilo linaweza kuwa na nafasi ya kuweka kituo kidogo cha kurutubisha urani kwa kutumia centrifuge za kisasa au kuhifadhi vifaa nyeti vya mpango wa nyuklia.

Taasisi hiyo pia imewahi kudokeza uwezekano wa shughuli zinazohusisha urani ya metali, ambayo inaweza kutumika katika utengenezaji wa silaha za nyuklia, lakini imesema haina ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.

Kwa upande mwingine, wataalamu wanasema picha za satelaiti hazionyeshi alama zinazotarajiwa kuonekana katika ujenzi wa kinu cha nyuklia, kama vile minara ya kupooza mitambo, mabwawa ya kuhifadhi mafuta ya nyuklia yaliyotumika, au mtandao mkubwa wa usambazaji wa maji.

Kwa sasa, hakuna ripoti rasmi ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, wala ushahidi uliothibitishwa wa kijasusi au picha za satelaiti unaothibitisha kuwa Pickaxe Mountain inatumika kwa shughuli za kutengeneza silaha za nyuklia.

Changamoto kubwa ni kwamba wakaguzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki hawajaruhusiwa kuingia katika eneo hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Rafael Grossi, amesema wakaguzi wanapaswa kuruhusiwa kufika mapema kabla ya vifaa vya nyuklia kuingizwa, lakini Iran inasema hilo si lazima hadi pale shughuli za nyuklia zitakapoanza rasmi.

Akizungumza na kipindi cha Newsday cha BBC World Service, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, Rafael Grossi, alisema ''wakaguzi walipaswa tayari kuwa wamepewa ruhusa ya kuingia katika kituo hicho''.

Kwa mujibu wa tathmini ya hivi karibuni ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, kufikia Juni 13, 2025, siku ya kwanza ya vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel, Iran ilikuwa na kilo 440.9 za urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 60, hatua moja tu kabla ya kufikia kiwango cha asilimia 90 kinachohitajika kutengeneza silaha za nyuklia. Ni katika kipindi hicho ndipo wakaguzi wa shirika hilo walipopoteza uwezo wa kufikia vituo vya nyuklia vya Iran.

Wakati huo, shirika hilo lilikuwa linajua kuwa sehemu kubwa ya urani hiyo ilitolewa katika vituo vya Fordow na Natanz, lakini halikuwa na uhakika kwamba bado ilikuwa imehifadhiwa katika maeneo hayo.

Mwaka 2026, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Rafael Grossi, alisema zaidi ya kilo 200 za urani zinaaminika kuwa bado zilikuwepo ndani ya kituo cha chini ya ardhi kilichopo Isfahan.

Kwa sasa, Pickaxe Mountain imeendelea kuwa kitovu cha uvumi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Licha ya tahadhari na wasiwasi kutoka Marekani na washirika wake, hakuna ushahidi wa umma uliothibitishwa unaoonyesha kuwa eneo hilo linatumika kutengeneza silaha za nyuklia.

Marekani iliwahi kushambulia kituo cha nyuklia cha Fordow kwa kutumia bomu la GBU 57, bomu lenye uzito wa tani 13.6 lililoundwa kupenya tabaka za udongo, miamba na zege lililoimarishwa kabla ya kulipuka.

Hata hivyo, wataalamu wanasema mafanikio ya shambulizi la aina hiyo hutegemea aina ya mwamba, kina cha kituo kilicholengwa na pembe ya shambulizi. Shambulizi dhidi ya Fordow lilifanyika baada ya miaka kadhaa ya ukusanyaji wa taarifa za kijasusi uliofanywa kwa ushirikiano kati ya Marekani na Israel.

Mwanasayansi wa masuala ya nyuklia kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts, Matthew Sharp, aliliambia gazeti la Wall Street Journal kuwa Marekani haiwezi kutarajia mafanikio sawa ikiwa itashambulia Pickaxe Mountain, kwa sababu kituo hicho kinakadiriwa kuwa na kina kikubwa zaidi na muundo wake wa ndani haujulikani vizuri.

Iwapo vifaa vya nyuklia vitakuwa vimehifadhiwa katika sehemu za ndani kabisa za Pickaxe Mountain, ni vigumu kutathmini kama mashambulizi ya anga yataweza kuviharibu.

Hata hivyo, mashambulizi yanaweza kuharibu milango ya mahandaki, njia za kuingia, pamoja na mifumo ya umeme na uingizaji hewa, na hivyo kuchelewesha au kuzuia matumizi ya baadaye ya kituo hicho.

Wataalamu wanasema milango ya mahandaki pamoja na njia za kuingia ndizo zinaweza kuwa sehemu dhaifu zaidi na hivyo kuwa rahisi kulengwa.

Hali hiyo inaweza kueleza kwa nini Donald Trump ameendelea kulitaja Pickaxe Mountain katika matamshi yake ya hivi karibuni, kwani kina chake, ulinzi wake mkubwa na uwezekano wa kuwa na nafasi muhimu katika mpango wa nyuklia wa Iran vimeifanya kuwa moja ya maeneo yanayofuatiliwa kwa karibu na maafisa wa Marekani.