Vifaa 10 vya kiteknolojia vya ajabu zaidi ambavyo mamilionea wanatarajiwa kununua mwaka huu

Chanzo cha picha, Mirumi
Tukio kubwa zaidi la teknolojia la mwaka limekamilika na kumalizika, na hizi hapa ni chaguo zetu za vifaa vya kiteknolojia vya ajabu zaidi vilivyotangazwa.
CES, maonesho makubwa zaidi ya teknolojia duniani, yamehitimishwa hivi karibuni baada ya kuonesha mkusanyiko wa kushangaza sana wa ubunifu wa kiteknolojia.
Hata hivyo, ingawa mwelekeo mkubwa ulikuwa kwenye maendeleo ya hivi karibuni ya akili mnemba (AI), magari yanayoruka na ubunifu wa kushangaza katika sekta ya afya, kulikuwa na maendeleo mengine mengi ambayo, tuseme tu, yalikuwa ya kuvutia kwa namna ya kipekee.
Bila shaka, tunazungumzia mkusanyiko usio na mwisho wa vifaa vya ajabu vilivyooneshwa kwenye maonesho hayo.
Baadhi yake vina manufaa ya kweli na vinatarajia kubadilisha maisha ya watumiaji, lakini vingine vitawaacha hata wapenda teknolojia waliodhamiria zaidi wakikuna vichwa vyao kwa mshangao, wakijiuliza vilitengenezwa kwa ajili ya nini.
Kuanzia kifaa cha huduma za afya kinachopima mate hadi mbwa roboti anayefanana na kiumbe aliyefufuka kutoka kwa wafu, CES 2025 imeanza kwa mtindo wa ajabu na usio wa kawaida kabisa.
End of Unaweza kusoma
Tombot Jenny

Chanzo cha picha, Tombot
Tombot ni wazo zuri lenye utekelezaji ambao, kwa kiasi fulani, unaweza kuonekana wa kutisha.
Ingawa picha iliyo hapo juu inaweza kukufanya ufikiri kwamba hiki ni kifaa kipya cha kiteknolojia kinachohusiana na taxidermy (uhifadhi wa wanyama waliokufa), kwa kweli ni mbwa roboti aliyebuniwa kutoa upendo na msaada wote unaoweza kupatikana kutoka kwa mtoto wa mbwa, bila usumbufu na majukumu yanayoambatana na kumtunza mbwa halisi.
Lengo ni kuwapatia urafiki watu wanaouhitaji lakini hawawezi kuutunza au kuurudisha kwa njia ya kawaida. Jenny, "mbwa" wa kwanza waliyemtengeneza, anaweza kuitikia unapomgusa, kutii amri za sauti na kutumia sauti halisi za mtoto wa mbwa ili kuiga mbwa wa kweli.
Kampuni inayotengeneza kifaa hiki inasema kwamba kinaweza kusaidia kupunguza msongo wa mawazo, upweke, wasiwasi na huzuni. Pia ni mbwa pekee duniani mwenye programu ya simu na anayepokea masasisho ya programu mara kwa mara.
Roborock Saros Z70
Roborock Saros Z70 inaonekana kama roboti kama yoyote ya kusafisha sakafu iliyowahi kutengenezwa, lakini ina tofauti moja ndogo: mkono wake wa juu wa kimakanika. Roboti hii inapozunguka ndani ya nyumba, mkono huo wa kimakanika hujitokeza na kuokota pamoja na kusogeza vitu vilivyo njiani, hivyo kuiwezesha kuendelea kusafisha maeneo yaliyokuwa yamezuiwa.
Itatambua soksi, viatu, tishu, taulo na vitu vingine vinavyoizuia kwa kutumia kamera na vihisishi. Lakini haiishii tu kuviondoa njiani, inaweza kufundishwa kuweka vitu katika maeneo tofauti. Kwa mfano, inaweza kukusanya nguo zako zote chafu na kuziweka sehemu moja, au kuweka taka kwenye pipa.
Ikiwa hivi ndivyo utawala wa roboti utakavyoonekana, basi sisi tuko tayari kuupokea!
Eli Health Hormometer
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mate ni kitu ambacho, kwa kushangaza, hakitumiki sana. Angalau katika ulimwengu wa afya na ustawi wa mwili: mate yaliyomo kinywani mwako yanaweza kutoa taarifa kuhusu viashiria mbalimbali vya afya, lakini ni mara chache sana tunapima mate yetu.
Eli Health inalenga kubadilisha hali hiyo kwa kutengeneza mfululizo wa vipimo vya kutumia nyumbani vinavyoweza kupima homoni zako. Kifaa hicho ni kidogo na hakihitaji kuchomwa au kukatwa mwili, na kinachoitwa "Hormometer" (ndiyo, hilo ndilo jina lake!) huwekwa mdomoni kwa sekunde chache ili kukusanya sampuli ya mate.
Baada ya hapo, taarifa hukusanywa na kutumwa moja kwa moja kwenye programu iliyopo kwenye simu janja yako, ambayo hukupa kipimo cha kiwango chako cha sasa cha cortisol, homoni inayosaidia mwili kukabiliana na msongo wa mawazo, na pia inayohusishwa na mambo kama shinikizo la damu na kimetaboliki.
Ni njia rahisi kwa wapenzi wa biohacking kufuatilia kila siku vipindi ambavyo kiwango cha cortisol hupanda na kushuka na kuwapa pia jambo jipya la kuwa na wasiwasi nalo.
Tanuri la Pizza la Model P

Chanzo cha picha, Current Backyard
Huenda kifaa hiki kikaonekana kama kifaa cha kuchezea cha mtoto, lakini kwa kweli, Current Backyard imezindua kile wanachodai kuwa ni mojawapo ya tanuri mahiri zaidi za pizza kuwahi kutengenezwa.
Tanuri hili limeidhinishwa kutumika ndani na nje ya nyumba, na lina Bluetooth pamoja na Wi-Fi. Lengo lake ni kuondoa usumbufu na kazi nyingi zinazohusika katika kutengeneza pizza.
Kwa kweli, tanuri hili ni mahiri kiasi kwamba linaweza kubainisha muda na halijoto sahihi ya kupikia kulingana na unene wa unga, idadi ya viambato vilivyowekwa kwenye pizza, pamoja na uzito wa jibini na mchuzi.
Kwa kuwa linatumia umeme kikamilifu, halitumii miali ya moto. Hii inamaanisha haliwezi kutoa ladha ileile ya pizza iliyochomwa kwenye moto inayopatikana kwa kutumia tanuri za jadi za pizza. Lakini kwa upande mwingine, linakuokoa kutokana na hatari ya kuchoma nyumba yako moto. Kwa maoni yetu,hayo ni mabadiliko yanayokubalika.
Yukai Engineering Mirumi

Chanzo cha picha, Yukai Engineering
Yukai Engineering ni kampuni ya aina yake. Wanatengeneza baadhi ya roboti za ajabu zaidi sokoni na katika ulimwengu ambao ghafla umejaa roboti za kustaajabisha na wakati mwingine za kutisha, huo ni ushindi mkubwa wa ubunifu.
Kifaa cha hivi karibuni katika orodha yao ni Mirumi. Kikiwa na muonekano unaofanana na mchanganyiko wa Ewok na Barbie, roboti hii ndogo ina mikono midogo inayoweza kuzungushwa kwenye mikoba au mikanda na hivyo kubebwa popote.
Ikishashikizwa kwenye begi, Mirumi inaweza kuonesha hali mbalimbali kama vile udadisi; kwa mfano, inaweza kugeuza kichwa chake kuelekea kitu kinachotembea au sauti kubwa. Pia inaweza kuonesha aibu mtu anapokikaribia, au kuonesha kutofurahishwa kwa kutikisa kichwa polepole.
Na lengo la haya yote ni nini? Kwa kweli, hakuna lengo maalumu. Lakini kwa kampuni ambayo tayari imetengeneza mito laini ya roboti yenye mikia, pamoja na mbwa roboti waliobuniwa kwa kusudi moja tu, kuuma kidole chako kidogo kidogo , kifaa hiki kipya kinaonekana kabisa kuwa sehemu ya familia hiyo.
Mbinu mahiri ya kupikia Sous Vide ya Figo

Chanzo cha picha, Figo
Kwa yule mtu ofisini kwako ambaye huwa haachi kuzungumza kuhusu vifaa vya kupikia visivyo vya lazima: sous vide inaweza kuwa shauku yako mpya.
Kwa wale ambao hamjui sous vide ni nini, ni mbinu ya kupikia ambapo chakula huwekwa kwenye mfuko kisha kupikwa taratibu sana ndani ya maji.
Huenda jambo hilo lisisikike la kuvutia sana, lakini mbinu hii huepuka matumizi ya mafuta ya ziada wakati wa kupika na husaidia kufikia na kudumisha kiwango maalumu cha joto. Katika ulimwengu wa upishi wa hali ya juu, sous vide ni jambo kubwa.
Figo Smart Sous Vide, iliyooneshwa kwa mara ya kwanza kwenye CES 2025, inachukua mbinu hii na kuongeza ubunifu mwingine: pamoja na kuwa mashine ya sous vide, inaweza pia kutumika kama friji ya muda.
Sawa, si kifaa cha kusisimua kiasi cha kuwa maarufu kama kikaangio (air fryer), lakini wazo lililo nyuma yake lina mvuto fulani. Weka chakula chako ndani ya mashine na uweke muda wa kupika. Hata kama muda wa kupika bado haujafika na mashine haitaanza kupika kwa saa kadhaa, chakula kitaendelea kuhifadhiwa katika halijoto ya friji.
Ni kweli, hiyo ni hali ya kupikia ambayo ni ya matumizi maalumu sana, lakini ni jambo ambalo sous vide mahiri inaweza kulishughulikia na kutoa matokeo mazuri sana.
L'oreal Cell BioPrint
L'Oréal imekuwa mojawapo ya chapa zinazovutia zaidi kufuatiliwa kwenye CES kwa miaka kadhaa sasa, huku ikiendelea kuunganisha teknolojia na urembo. Kwa mwaka 2025, kampuni hiyo ilichukua mwelekeo wa kuvutia kwa kutengeneza bidhaa ambayo, kwa mzaha, inaweza kukukosoa kwa kuthubutu kuzeeka.
Sawa, kwa kweli haifanyi hivyo hasa, L'Oréal imechagua njia ya upole zaidi. Ingawa si kwa kiwango kikubwa sana.
Cell BioPrint huchambua ngozi yako na kubaini jinsi inavyozeeka. Kisha hukupa ushauri kuhusu jinsi ya kuboresha mwonekano wa ngozi yako na ni viambato gani vinavyohitajika.
Mchakato huu hufanyika kwa kutumia tepu maalumu ya usoni, ambayo huwekwa kwenye mashine na kufanyiwa uchunguzi. Kisha kifaa hicho hupiga picha za uso wako na kukuuliza maswali machache.
Ni wazo la kuvutia, bila shaka. Lakini bila kufanyiwa majaribio na tafiti zilizopitiwa na wataalamu wa kisayansi, ni vigumu kujua kwa usahihi kiwango ambacho dhana hii mpya ya L'Oréal itakuwa sahihi.
Birdfy Bath Pro

Chanzo cha picha, Birdfy
Iwe wewe ni mpenda ndege wa kawaida tu au twitcher wa kweli (yaani, mtu anayependa sana kutazama ndege), huenda kifaa hiki kikakuvutia. Ni bafu la ndege lenye kamera iliyounganishwa.
Jambo hili limefanyika mara nyingi hapo awali, kwa hiyo kuna tofauti gani wakati huu? Akili mnemb. Hakuna mshangao hapo, lakini teknolojia hii inaleta jambo jipya. Kamera inaweza kutambua na kurekodi aina mbalimbali za ndege, na pia kukutengenezea matukio muhimu ya kila siku ambayo unaweza kuyatazama baadaye.
Kila mwezi pia utapokea ripoti inayoonesha idadi ya ndege waliotambuliwa, aina ya ndege adimu zaidi iliyonekana, pamoja na taarifa nyingine muhimu. Ikiwa uko tayari kupata taarifa hizi kwa kutumia AI kuwapeleleza ndege wanapooga, hilo ni suala lako.
Pawport
Pawport huenda ikawa kifaa cha mbwa kilichobuniwa kwa teknolojia nyingi kupita kiasi kuliko kifaa kingine chochote cha aina hiyo.
Kikionekana kana kwamba kilibuniwa kwa ajili ya mbwa wa Darth Vader, mlango huu wa wanyama unaoendeshwa kwa mota umeundwa kwa taa za neon na rangi nzito za giza. Bidhaa hii mpya inatajwa kuwa "mlango wa wanyama wa kufugwa wenye mvuto wa kipekee zaidi kuwahi kutengenezwa", hayo ni maneno yao, si yetu.
Kifaa hiki kinaweza kutambua mbwa anapokuwa karibu, na kufungua mlango moja kwa moja, kisha kuufunga mnyama huyo anapoondoka. Unaweza kuweka muda maalumu wa kutotoka nje, kukifunga au kukifungua kwa mbali, na kufuatilia muda ambao mnyama wako amekuwa nje.
Huenda kisiwafae kila mtu, lakini kwa watu wanaopenda teknolojia kupita kiasi, ni bidhaa ya kipekee kabisa.
Withings Omnia

Chanzo cha picha, Withings
Withings imegeuza teknolojia ya afya kuwa sanaa ya hali ya juu, kwa kutengeneza vifaa vya kufuatilia mwili vinavyoonekana kana kwamba vimetolewa moja kwa moja kutoka kwenye ulimwengu wa siku zijazo.
Kifaa kipya zaidi katika juhudi hizi kinaitwa Omnia. Kikichanganya kioo mahiri na mizani iliyounganishwa, kifaa hiki kinaweza kutengeneza mfano kamili wa mwili wa 3D, huku kikichanganua mwili wako kwa kutumia vihisishi ili kukupa taarifa za afya kila siku.
Kwa sasa, maelezo kamili kuhusu jinsi kinavyofanya kazi bado hayajawekwa wazi, lakini Withings inadai kwamba kifaa chake hiki kipya kinaweza kutoa taarifa na uchambuzi unaozingatia urefu wako, uzito, usingizi, shughuli za mwili, lishe na mambo mengine.
Taarifa zote hizi huoneshwa kwenye kioo ili kukupa picha kamili ya hali ya afya yako.
Kama ilivyo kwa karibu kila kifaa kingine cha kiteknolojia kinachopatikana kila mahali kwa sasa, kioo hiki pia kina msaidizi wa akili mnemba (AI), ambaye inadaiwa atatoa ushauri wa kihisia kwa wakati halisi na hata kukuwekea miadi na daktari unapohitaji.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi












